Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 28 April 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Danieli 2...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

“Wao walitujibu hivi: ‘Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na dunia, na tunaijenga upya nyumba ambayo ilikuwa imejengwa na kumalizika hapo awali na mfalme mmoja mkuu wa Israeli.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Lakini kwa kuwa babu zetu walimkasirisha Mungu wa mbingu, yeye aliwatia mikononi mwa mfalme Nebukadneza wa Babuloni, Mkaldayo, aliyeiharibu nyumba hii na kuwapeleka watu uhamishoni huko Babuloni.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Lakini mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wake mfalme Koreshi wa Babuloni alitoa amri nyumba hii ya Mungu ijengwe upya.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

Ndoto ya mfalme Nebukadneza
1Mnamo mwaka wa pili wa utawala wake, mfalme Nebukadneza aliota ndoto, akawa na wasiwasi sana rohoni hata usingizi ukamtoweka. 2Taz Mwa 41:8 Basi, mfalme akaamuru waganga, walozi na wachawi wa Wakaldayo waletwe ili wamfasirie ndoto yake. Wote wakaja na kusimama mbele yake.
3Mfalme Nebukadneza akawaambia, “Niliota ndoto, nayo inanipa wasiwasi, nami nataka nijulishwe tafsiri yake.” 4Wale Wakaldayo wakamwambia mfalme kwa Kiaramu, “Uishi, ee mfalme! Tusimulie ndoto yako nasi watumishi wako tutakufasiria.”
5Mfalme akawaambia, “Nimetoa kauli yangu kamili: Ikiwa hamtanijulisha ndoto yenyewe na maana yake, mtangolewa viungo vyenu kimojakimoja, na nyumba zenu zitabomolewa. 6Lakini mkiniambia hiyo ndoto na maana yake, nitawapa zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi, nijulisheni ndoto hiyo na maana yake!” 7Wao wakamjibu mara ya pili, “Mfalme, tusimulie ndoto hiyo, nasi watumishi wako tutakufasiria.” 8Hapo mfalme akawakatiza kwa kusema, “Najua kweli kwamba mnajaribu kupoteza wakati kwa kuwa mnaona kwamba nilikwisha toa kauli yangu kamili, 9kwamba msiponijulisha ndoto hiyo, adhabu yenu ni moja. Mmepatana kunidanganyadanganya na kunilaghailaghai huku muda unapita. Niambieni ndoto hiyo, nami nitajua kuwa mnaweza kunijulisha maana yake.” 10Wale Wakaldayo wakamjibu: “Mfalme, hakuna mtu yeyote duniani awezaye kutimiza matakwa yako. Hakuna mfalme yeyote, hata awe mkuu na mwenye nguvu kiasi gani aliyepata kuwauliza waganga au walozi au Wakaldayo jambo kama hilo. 11Jambo unalouliza, ee mfalme, ni gumu. Hakuna mtu anayeweza kukufunulia isipokuwa miungu peke yake ambayo haikai miongoni mwa wanaadamu.” 12Kusikia hivyo, mfalme Nebukadneza alikasirika na kughadhibika sana, akaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waangamizwe. 13Basi, tangazo likaenea kuwa wenye hekima wote wauawe; Danieli na wenzake, nao pia wakatafutwa ili wauawe.
Mungu amfunulia Danieli ndoto
14Basi, Danieli, kwa tahadhari na busara, alimwendea Arioko, mkuu wa kikosi cha walinzi wa mfalme na ambaye alipewa jukumu la kuwaua wenye hekima wa Babuloni, 15akamwuliza, “Kwa nini amri ya mfalme ni kali hivyo?” Hapo Arioko akamsimulia Danieli kisa chote. 16Ndipo Danieli alipomwendea mfalme na kumwomba ampe muda ili aweze kumjulisha mfalme maana ya ndoto yake.
17Kisha, Danieli akarudi nyumbani, akawajulisha wenzake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo. 18Aliwaambia wamwombe Mungu wa mbinguni awaonee huruma kuhusu fumbo hilo, ili wao wasiangamie pamoja na wenye hekima wengine wa Babuloni. 19Ndipo Danieli alipofunuliwa fumbo hilo usiku katika maono. Naye Danieli akamshukuru Mungu wa mbinguni, 20akasema,
“Na litukuzwe milele na milele jina lake Mungu.
Hekima na nguvu ni vyake.
21Hubadilisha nyakati na majira,
huwaondoa na kuwatawaza wafalme.
Wenye busara huwapa hekima,
wenye maarifa huwaongezea ufahamu.
22Hufunua siri na mafumbo,
ajua kilichoko gizani,
mwanga wakaa kwake.
23Kwako, ee Mungu wa wazee wangu,
natoa shukrani na kukusifu,
maana umenipa hekima na nguvu,
umetujulisha kile tulichokuomba,
umetujulisha kile kisa cha mfalme.”
Danieli aifasiri ndoto
24Basi, Danieli akamwendea Arioko aliyekuwa ameteuliwa kuwaangamiza wenye hekima wa Babuloni, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babuloni, ila nipeleke mimi mbele ya mfalme, nami nitamweleza maana ya ndoto yake.”
25Basi, Arioko akampeleka Danieli mbele ya mfalme kwa haraka na kumwambia, “Nimempata mtu fulani miongoni mwa mateka wa Yuda anayeweza kukufasiria ndoto yako, ee mfalme.” 26Mfalme akamwuliza Danieli, ambaye pia aliitwa Belteshaza, “Je, unaweza kunijulisha ndoto niliyoota na maana yake?” 27Danieli akamjibu mfalme, “Hakuna wenye hekima, wachawi, waganga wala wanajimu wanaoweza kukujulisha fumbo hilo lako. 28Lakini, yuko Mungu mbinguni ambaye hufumbua mafumbo, naye amekujulisha, ee mfalme Nebukadneza, mambo yatakayotukia siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyokujia kichwani mwako ulipokuwa umelala ni haya: 29Kwako ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani mwako, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotukia baadaye; naye Mungu afumbuaye mafumbo, alikuonesha yale yatakayotukia. 30Lakini mimi sikufumbuliwa fumbo hili kwa sababu nina hekima kuliko wanaadamu wengine, bali ili wewe mfalme, upate kujulishwa maana ya ndoto yako na kujua mawazo yako.
31“Katika ndoto yako, ee mfalme, uliona sanamu kubwa, yenye nguvu na iliyongaa sana, imesimama mbele yako. Sanamu hiyo ilikuwa ya kutisha mno. 32Kichwa cha sanamu hiyo kilikuwa cha dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha na tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba. 33Miguu yake ilikuwa ya chuma na nyayo zake zilikuwa za mchanganyiko wa chuma na udongo wa mfinyanzi. 34Ukiwa bado unaangalia, jiwe lilingoka lenyewe, bila kuguswa, na kuipondaponda miguu ya shaba na udongo wa mfinyanzi ya ile sanamu, na kuivunja vipandevipande. 35Mara kile chuma, udongo wa mfinyanzi, shaba, fedha na dhahabu, vyote vikavunjika vipandevipande na kuwa kama makapi ya mahali pa kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperushia mbali kisibakie hata kipande kimoja. Lakini lile jiwe lililoivunja ile sanamu likageuka kuwa mlima mkubwa na kuijaza dunia yote.
36“Hiyo ndiyo ndoto yako, ee mfalme. Na sasa tutakupa maana yake. 37Wewe, ee mfalme, mfalme wa wafalme! Mungu amekupa ufalme, uwezo, nguvu na utukufu! 38Amekupa mamlaka juu ya wanaadamu wote, wanyama wa porini na ndege wote wa angani, kokote kule waliko. Wewe ndiwe kile kichwa cha dhahabu! 39Baada yako utafuata ufalme mwingine, lakini ufalme huo utakuwa dhaifu. Huu utafuatwa na ufalme wa tatu unaofananishwa na shaba; huo utaitawala dunia yote. 40Baada ya falme hizo, utafuata ufalme mwingine imara kama chuma. Na kama vile chuma kivunjavyo na kupondaponda vitu vyote, ndivyo ufalme huo utakavyovunjavunja na kusagilia mbali falme zilizotangulia. 41Uliona pia kuwa nyayo na vidole vya sanamu hiyo vilikuwa nusu udongo wa mfinyanzi na nusu chuma. Hii ina maana kwamba ufalme huo utagawanyika; lakini utakuwa na kiasi fulani cha nguvu za chuma kwa sababu kulikuwa na chuma kilichochanganyikana na udongo wa mfinyanzi. 42Kama ulivyoona, vidole vyake vya miguu vilikuwa nusu chuma na nusu udongo wa mfinyanzi, na hii inamaanisha kwamba ufalme huo utakuwa na nguvu kiasi fulani na udhaifu kiasi fulani. 43Hii inamaanisha kwamba watawala wa ufalme huo watachanganyikana kwa kuoana na watu wasio wa taifa lao, lakini hawatafaulu kuchanganyikana kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi. 44Wakati wa wafalme hao, Mungu wa mbinguni ataanzisha ufalme ambao kamwe hautaangamizwa. Watu wengine hawataushinda na kuutawala ufalme huo, bali ufalme huo utaziponda na kuzikomesha falme zilizotangulia, nao utadumu milele. 45Uliliona jiwe lililongoka lenyewe toka mlimani, bila kuguswa, na jinsi lilivyoivunja vipandevipande ile sanamu iliyotengenezwa kwa chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu. Ee mfalme, Mungu Mkuu amekufunulia mambo yatakayotukia baadaye. Mimi nimekusimulia. Ndoto yako ni ya kweli na maana yake ni halisi.”
Mfalme amtuza Danieli
46Ndipo mfalme Nebukadneza alipoanguka kifudifudi na kumsujudia Danieli na kuamuru wamtolee Danieli tambiko na ubani. 47Mfalme akamwambia Danieli, “Hakika, Mungu wako ni Mungu wa miungu na Bwana wa wafalme, na ndiye afumbuaye mafumbo kwa sababu umefaulu kunifumbulia fumbo hili.” 48Kisha mfalme Nebukadneza akamtunukia Danieli heshima kubwa, akampa zawadi nyingi kubwakubwa, na kumfanya mtawala wa mkoa wote wa Babuloni, na mkuu wa wenye hekima wote wa Babuloni. 49Danieli akamwomba mfalme, naye mfalme akawaweka Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa wasimamizi wa mambo ya utawala ya mkoa wa Babuloni. Lakini Danieli akabakia katika jumba la mfalme.



Danieli2;1-49

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: