Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 7 February 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 50....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

‘Mungu asema: Watu hawa huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami. Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni, mkaelewe! Kitu kinachomtia mtu unajisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu unajisi.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?” Lakini yeye akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakupanda, utangolewa. Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni.”
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Babuloni
1Neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kwa njia ya nabii Yeremia kuhusu nchi ya Babuloni na nchi ya Wakaldayo:
2“Tangazeni kati ya mataifa,
twekeni bendera na kutangaza,
Msifiche lolote. Semeni:
‘Babuloni umetekwa,
Beli ameaibishwa.
Merodaki amefadhaishwa;
sanamu zake zimeaibishwa,
vinyago vyake vimefadhaishwa.’
3“Kwa maana, taifa kutoka kaskazini limefika kuushambulia; litaifanya nchi yake kuwa uharibifu. Hakuna atakeyeishi humo; watu na wanyama watakimbia mbali.
Kurudi kwa Israeli
4“Siku hizo na wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, watu wa Israeli na watu wa Yuda watakusanyika pamoja na kurudi wakilia huku wananitafuta mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. 5Watauliza njia ya kwenda Siyoni, huku nyuso zao zimeelekea huko, wakisema, ‘Njoni!’ Nao watajiunga na Mwenyezi-Mungu katika agano la milele ambalo kamwe halitasahauliwa.
6“Watu wangu walikuwa kondoo waliopotea; wachungaji wao wamewapotosha, wakawageuza kuelekea milimani; walitembea toka mlima hadi kilima, wakasahau zizi lao. 7Watu wote waliowakuta waliwaua, na maadui zao wamesema, ‘Hatuna hatia sisi’, maana hao wamemkosea Mwenyezi-Mungu aliye malisho yao ya kweli; Mwenyezi-Mungu ambaye ni tegemeo la wazee wao!
8“Kimbieni kutoka Babuloni! Tokeni nje ya nchi ya Wakaldayo, muwe kama mabeberu mbele ya kundi. 9Maana, mimi nitachochea mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini washambulie Babuloni. Watajiandaa kuishambulia Babuloni na kuiteka. Mishale yao ni kama shujaa hodari asiyerudi mikono mitupu. 10Nchi ya Wakaldayo itaporwa, na hao watakaoipora wataridhika. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
Kuanguka kwa Babuloni
11“Enyi waporaji wa mali yangu!
Japo mnafurahi na kushangilia,
mnarukaruka kama mtamba wa ng'ombe anayepura nafaka,
na kulia kama farasi dume,
12nchi yenu ya kuzaliwa itaaibishwa;
hiyo nchi mama yenu itafedheheshwa.
Lo! Babuloni itakuwa ya mwisho kati ya mataifa,
itakuwa nyika kame na jangwa.
13Kwa sababu ya ghadhabu yangu Mwenyezi-Mungu,
Babuloni haitakaliwa kabisa na watu,
bali itakuwa jangwa kabisa;
kila atakayepita karibu nayo atashangaa
ataizomea kwa sababu ya majeraha yake.
14“Enyi nyote wapiga mishale stadi,
shikeni nafasi zenu kuuzingira mji wa Babuloni;
upigeni, msibakize mshale hata mmoja,
maana umenikosea mimi Mwenyezi-Mungu.
15Upigieni kelele za vita pande zote,
sasa Babuloni umejitoa ukamatwe.
Ngome zake zimeanguka,
kuta zake zimebomolewa.
Ninalipiza kisasi juu ya Babuloni
Basi jilipizeni kisasi,
utendeeni kama ulivyowatenda wengine.
16Zuieni watu wasipande mbegu Babuloni,
wala wasivune wakati wa mavuno.
Kutokana na upanga wa udhalimu,
kila mmoja atawarudia watu wake
kila mmoja atakimbilia nchini mwake.
17“Israeli ni kondoo wanaowindwa na kufukuzwa na simba. Kwanza waliangamizwa na mfalme wa Ashuru, na sasa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, amevunjavunja mifupa yake. 18Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nitamwadhibu mfalme wa Babuloni na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru. 19Nitawarudisha Waisraeli nchini mwao, nao watakula mavuno yatakayolimwa juu ya mlima Karmeli na Bashani na watatosheka kwa chakula kutoka milima ya Efraimu na Gileadi. 20Siku hizo na wakati huo, uovu utatafutwa nchini Israeli, lakini hautapatikana; dhambi itatafutwa nchini Yuda, lakini haitapatikana; maana mimi nitawasamehe wale ambao nimewabakiza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21“Pandeni, mwiendee nchi ya Merathaimu,
nendeni kuishambulia;
washambulieni wakazi wa Pekodi
na kuwaangamiza kabisa watu wake.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
Fanyeni kila kitu nilichowaamuru.
22Kelele za vita zinasikika nchini,
kuna uharibifu mkubwa.
23Jinsi gani huo mji uliokuwa nyundo ya dunia nzima
unavyoangushwa chini na kuvunjika!
Babuloni umekuwa kinyaa
miongoni mwa mataifa!
24Ewe Babuloni, nilikutegea mtego ukanaswa,
wala hukujua juu yake;
ulipatikana, ukakamatwa,
kwa sababu ulishindana nami Mwenyezi-Mungu.
25Nimefungua ghala yangu ya silaha,
nikatoa humo silaha za ghadhabu yangu,
maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi
nina kazi ya kufanya
katika nchi ya Wakaldayo.
26Njoni mkamshambulie kutoka kila upande;
zifungueni ghala zake za chakula;
mrundikieni marundo ya nafaka!
Iangamizeni kabisa nchi hii;
msibakize chochote!
27Waueni askari wake hodari;
waache washukie machinjoni.
Ole wao, maana siku yao imewadia,
wakati wao wa kuadhibiwa umefika.
28“Sikiliza! Wakimbizi na watoro kutoka nchi ya Babuloni wanakuja kutangaza huko Siyoni jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyolipiza kisasi kwa ajili ya hekalu lake.
29“Waiteni wapiga mishale waishambulie Babuloni. Pelekeni kila mtu ajuaye kuvuta upinde. Uzingireni mji pasiwe na yeyote atakayetoroka. Ulipizeni kadiri ya matendo yake yote; utendeeni kama ulivyowatendea wengine, maana kwa kiburi ulinidharau mimi Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli. 30Kwa hiyo, vijana wake watauawa katika mitaa yake, na majeshi yake yote yataangamizwa siku hiyo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
31“Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
napigana nawe ewe mwenye kiburi,
maana siku yako ya adhabu imefika,
wakati nitakapokuadhibu umewadia.
32Mwenye kiburi atajikwaa na kuanguka,
wala hapatakuwa na mtu wa kumwinua.
Nitawasha moto katika miji yake,
nao utateketeza kila kitu kandokando yake.”
33Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Watu wa Israeli wanakandamizwa; hali kadhalika na watu wa Yuda. Wale waliowachukua mateka wamewabana sana na wanakataa kuwaachia. 34Lakini mimi, Mkombozi wao ni mwenye nguvu. Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina langu. Hakika nitatetea kisa chao ili nilete amani katika nchi yao, lakini taabu kwa wakazi wa Babuloni.
35“Kifo kwa Wakaldayo,
kwa wakazi wa Babuloni
na maofisa na wenye hekima wake!
36Kifo kwa waaguzi,
wanachotangaza ni upumbavu tu!
Kifo kwa mashujaa wake,
ili waangamizwe!
37Kifo kwa farasi wake na uharibifu kwa magari yake,
kifo kwa majeshi yake yote ya kukodiwa,
ili wawe na woga kama wanawake!
Uharibifu kwa hazina zake zote
ili zipate kuporwa.
38Ukame uyapate maji
ili yapate kukauka!
Maana Babuloni ni nchi ya sanamu za miungu,
watu ni wendawazimu juu ya vinyago vyao.
39“Kwa hiyo wanyama wa porini, mbwamwitu pamoja na mbuni, watakaa Babuloni. Hapatakaliwa kamwe na watu vizazi vyote vijavyo. 40Kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyoiangamiza miji ya Sodoma na Gomora na miji ya jirani, vivyo hivyo hapatakuwa na mtu yeyote atakayeishi humo. Naam, hakuna mtu yeyote atakeyekaa huko. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
41“Tazama! Watu wanakuja kutoka kaskazini;
taifa lenye nguvu na wafalme wengi
wanajitayarisha kutoka miisho ya dunia.
42Wameshika pinde zao na mikuki;
ni watu wakatili na wasio na huruma.
Vishindo vyao ni kama mvumo wa bahari,
wamepanda farasi.
Wamejipanga tayari kwa vita,
dhidi yako wewe Babuloni!
43Mfalme wa Babuloni amesikia habari zao,
nayo mikono yake ikawa kama kamba.
Ameshikwa na dhiki na uchungu kama mama anayejifungua.
44“Tazama, mimi nitakuwa kama simba anayechomoza kutoka msitu wa mto Yordani na kuingia kwenye malisho mazuri: Mimi Mwenyezi-Mungu nitawafukuza ghafla watu wake kutoka kwake. Nami nitamweka huko kiongozi yeyote nitakayemchagua. Maana, ni nani anayeweza kulinganishwa nami? Nani awezaye kunishtaki? Ni mchungaji gani awezaye kunipinga? 45Kwa hiyo, sikilizeni mpango ambao mimi Mwenyezi-Mungu nimepanga dhidi ya Babuloni pamoja na mambo niliyokusudia kuitendea nchi ya Wakaldayo: Hakika watoto wao wataburutwa na kuchukuliwa; kweli kutakuwa na mshangao mkubwa katika makao yao. 46Kwa kishindo cha kutekwa kwa Babuloni dunia itatetemeka, na kilio chake kitasikika miongoni mwa mataifa mengine.”


Yeremia50;1-46

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: