Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 21 February 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 3...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Tena, Yesu akasema, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


1Akaniambia, “Wewe mtu, kula unachopewa; kula kitabu hiki kisha uende ukawaeleze Waisraeli.”
2Kwa hiyo nilifumbua kinywa changu, naye akanilisha hicho kitabu. 3Halafu akaniambia, “Wewe mtu, kula kitabu hiki ninachokupa, ujaze tumbo lako.” Basi, nilikula kitabu hicho, nacho kikawa kitamu mdomoni kama asali.
4Kisha akaniambia, “Wewe mtu, waendee Waisraeli, ukawaambie maneno yangu. 5Sikutumi kwa taifa lenye lugha ngeni na ngumu, bali kwa Waisraeli. 6Sikutumi kwa mataifa mengi yenye lugha ngeni na ngumu ambayo huifahamu. Kwani ningelikutuma kwa watu kama hao, hakika wao wangekusikiliza. 7Lakini Waisraeli hawatakusikiliza, kwani hawana nia ya kunisikiliza mimi. Watu wote wa Israeli ni wenye kichwa kigumu na moyo mkaidi. 8Nimekufanya uwe mgumu dhidi yao, na kichwa chako kitakuwa kigumu dhidi ya vichwa vyao vigumu. 9Kama almasi ilivyo ngumu kuliko jiwe gumu, ndivyo nilivyokufanya uwe kichwa kigumu. Usiwaogope wala usitishwe na nyuso zao, kwani hao ni watu waasi.”
10Tena aliniambia, “Wewe mtu, maneno yote nitakayokuambia yatie moyoni mwako, na uyasikilize kwa makini. 11Kisha nenda kwa watu wako waliopelekwa uhamishoni, ukawaambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi. Waambie hata kama watakusikiliza au watakataa kukusikiliza.”
12Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama ya tetemeko kubwa. “Na usifiwe utukufu wa Mwenyezi-Mungu mbinguni.” 13Pia nilisikia sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yalipokuwa yanagusana, pamoja na sauti ya mgongano wa yale magurudumu kandokando yao. 14Basi, roho ya Mungu ikaninyanyua juu na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na ukali rohoni mwangu, nao mkono wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa na nguvu juu yangu.
15Nikawafikia wale watu waliokuwa uhamishoni, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari huko Tel-abibu. Nikakaa nao kwa muda wa siku saba nikiwa nimepigwa bumbuazi.
Ezekieli anaitwa kuwa mlinzi
(Eze 33:1-9)
16Baada ya siku saba, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 17“Wewe mtu nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Kila utakaposikia neno kutoka kwangu utawaonya watu kwa niaba yangu. 18Nikimwambia mtu mwovu kwamba hakika atakufa, nawe humwonyi au kumwambia aache njia yake potovu ili kuyaokoa maisha yake, basi, mtu huyo mwovu atakufa kwa uovu wake; lakini damu yake nitakudai wewe. 19Lakini, ukimwonya mtu huyo mwovu naye hauachi uovu wake au njia yake potovu, mtu huyo atakufa kwa uovu wake, lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako. 20Tena, kama mtu mwadilifu anauacha uadilifu wake na kutenda uovu, nami nikamwekea kikwazo, mtu huyo atakufa. Kwa vile hukumwonya, atakufa kwa sababu ya dhambi yake, nayo matendo yake ya uadilifu hayatakumbukwa. Lakini damu yake nitakudai wewe. 21Lakini, ukimwonya mtu mwadilifu asitende dhambi, naye akaacha kutenda dhambi, hakika mtu huyo ataishi, kwa kuwa amepokea maonyo yako, nawe utakuwa umeyaokoa maisha yako.”
Ezekieli anakuwa bubu kwa muda
22Nguvu ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa juu yangu; naye akaniambia, “Inuka uende mpaka sehemu tambarare nami nitaongea nawe huko.” 23Basi, nikainuka na kwenda sehemu tambarare. Lo! Nikiwa huko nikauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umesimama huko kama utukufu ule niliokuwa nimeuona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.
24Lakini roho iliniingia na kunisimamisha wima. Kisha Mungu akaongea nami, akaniambia, “Nenda ukajifungie nyumbani mwako. 25Ewe mtu, utafungwa kwa kamba ili usiweze kutoka na kuwaendea watu. 26Nitaufanya ulimi wako uwe mzito nawe utakuwa bubu ili usiweze kuwakemea kwa sababu ni waasi. 27Lakini kila nitakapoongea nawe nitakifungua kinywa chako, nawe utawaambia kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi, atakayekusikiliza, na akusikilize; atakayekataa kukusikiliza na akatae; maana hao ni watu waasi.


Ezekieli3;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: