Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 26 February 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 6...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Kuhusu kuwa mwadilifu kwa kuitii sheria, Mose aliandika hivi: “Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya sheria ataishi.” Lakini kuhusu kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: “Usiseme moyoni mwako: ‘Nani atapanda mpaka mbinguni?’ (yaani, kumleta Kristo chini); wala usiseme: ‘Nani atashuka mpaka kuzimu?’ (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu).”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Maandiko Matakatifu yasema hivi: “Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako” nao ndio ile imani tunayoihubiri.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Maana mtu huamini kwa moyo akafanywa mwadilifu; na hukiri kwa kinywa akaokolewa.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Lawama kwa wanaoabudu sanamu
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu, igeukie milima ya Israeli, utangaze ujumbe huu wangu dhidi ya wakazi wake 3na kusema: Sikilizeni neno la Bwana Mwenyezi-Mungu enyi wakazi wa milima ya Israeli: Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambieni nyinyi wakazi wa milimani na vilimani, wa magengeni na mabondeni kwamba mimi mwenyewe nitaleta upanga na kuharibu sehemu zenu zote zilizoinuka za ibada. 4Madhabahu zenu zitaharibiwa na mahali penu pa kufukizia ubani patavunjwavunjwa. Wale watakaouawa nitawatupa mbele ya sanamu zenu za miungu. 5Maiti za Waisraeli nitazilaza mbele ya sanamu zao za miungu, na mifupa yenu nitaitawanya kandokando ya madhabahu zenu. 6Kokote mnakoishi, miji yenu itakuwa ukiwa na sehemu za mwinuko za ibada zenu zitabomolewa, madhabahu zenu ziwe uharibifu na maangamizi, sanamu zenu za miungu zivunjwe na kuharibiwa. Mahali penu pa kufukizia ubani patabomolewa na chochote mlichofanya kitatokomezwa. 7Wale watakaouawa wataanguka kati yenu, nanyi mtatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu.
8“Hata hivyo, nitawaacha wengine wabaki hai; baadhi yenu watanusurika kuuawa nao watatawanyika katika nchi mbalimbali. 9Ndipo watakaponikumbuka mimi miongoni mwa hao watu wa mataifa ambamo watatawanyika. Watakumbuka jinsi nilivyowapiga kwa sababu mioyo yao isiyo na uaminifu ilinigeuka na kwa vile waliacha kunitazamia mimi wakazitazamia sanamu za miungu. Kwa hiyo watajichukia wao wenyewe kwa sababu ya maovu na machukizo yao yote waliyoyatenda. 10Hapo ndipo watakapojifunza kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu; sikuwatisha bure ya kwamba nitawaletea maovu hayo yote.”
11Bwana Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Piga makofi, piga kishindo kwa mguu na kusema: Ole wenu Waisraeli kwa sababu ya machukizo yenu yote, kwani mtakufa kwa upanga, njaa na kwa maradhi mabaya. 12Aliye mbali sana atakufa kwa maradhi mabaya. Aliye karibu atauawa kwa upanga. Atakayekuwa amebaki na kunusurika hayo mawili atakufa kwa njaa. Ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu dhidi yao. 13Maiti zao zitatapakaa kati ya sanamu zao za miungu na madhabahu zao, juu ya kila mlima, chini ya kila mti mbichi, chini ya kila mwaloni wenye majani na kila mahali walipotolea tambiko zao za harufu nzuri ya kuzipendeza sanamu zao za miungu. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. 14Nitaunyosha mkono wangu dhidi yao, na kuiharibu nchi yao. Tangu huko jangwani kusini mpaka mjini Ribla kaskazini, nitaifanya nchi yao kuwa mahame kabisa wasipate mahali pa kuishi. Hapo ndipo wote watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”



Ezekieli6;1-14

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: