Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 1 March 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 72...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Siku ile chipukizi wa Yese atakuwa ishara kwa mataifa; mataifa yatamtafuta na makazi yake yatatukuka. Siku hiyo, Bwana ataunyosha mkono wake tena kuwarejesha watu wake waliosalia huko Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Shinari, Hamathi na sehemu za pwani.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Naye atatweka bendera kuwaashiria mataifa, kuwakusanya Waisraeli waliodharauliwa, kuwaleta pamoja watu wa Yuda waliotawanywa, na kuwarudisha toka pembe nne za dunia. Wivu wa Efraimu juu ya Yuda utakoma, hakutakuwa tena na uadui kati ya Yuda na Efraimu. Wote pamoja watawavamia Wafilisti walio magharibi, pamoja watawapora watu wakaao mashariki. Watawashinda Waedomu na Wamoabu, nao Waamoni watawatii.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Mwenyezi-Mungu atakausha ghuba ya bahari ya Shamu, kwa pumzi yake ichomayo atakausha mto Eufrate, nao utagawanyika katika vijito saba, watu wavuke humo miguu mikavu. Tena, kutakuwa na barabara kuu toka Ashuru kwa ajili ya watu wake waliobaki humo kama ilivyokuwa kwa Waisraeli wakati walipotoka nchini Misri.
Tazama wenye shida/tabu,watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh tunaomba  ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu  unajua haja za mioyo ya kila mmoja
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Jehovah ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.

Kumwombea mfalme
(Zaburi ya Solomoni)
1Ee Mungu, umjalie mfalme uamuzi wako,
umpe mwanamfalme uadilifu wako;
2atawale taifa lako kwa haki,
na maskini wako kwa uadilifu.
3Milima ilete fanaka kwa watu wako,
vilima vijae uadilifu.
4Mfalme awatetee wanyonge wa taifa,
awasaidie watoto wa fukara,
na kuwaangamiza watu wadhalimu.
5Mfalme aishi muda mrefu kama jua,
na kama mwezi, kwa vizazi vyote.
6Awe kama manyunyu yaburudishayo mashamba,
kama mvua iinyweshayo ardhi.
7Uadilifu ustawi maisha yake yote,
na amani kwa wingi mpaka mwezi ukome.
8Atawale kutoka bahari hata bahari,
kutoka mto Eufrate hata mipaka ya dunia.
9Maadui zake wakaao nyikani wanyenyekee mbele yake,
washindani wake walambe vumbi.
10Wafalme wa Tarshishi na visiwa wamlipe kodi,
wafalme wa Sheba na Seba wamletee zawadi.
11Wafalme wote wa dunia wamheshimu,
watu wa mataifa yote wamtumikie.
12Anamkomboa fukara anayemwomba,
na maskini asiye na wa kumsaidia.
13Anawahurumia watu dhaifu na fukara,
anayaokoa maisha yao wenye shida.
14Anawatoa katika udhalimu na ukatili,
maana maisha yao ni ya thamani kubwa kwake.
15Mfalme na aishi maisha marefu;
apokee zawadi ya dhahabu kutoka Sheba;
watu wamwombee kwa Mungu daima,
na kumtakia baraka mchana kutwa.
16Nchi na izae nafaka kwa wingi,
vilima vijae mavuno kama ya Lebanoni,
na watu mijini wastawi kama nyasi.
17Jina la mfalme litukuke daima;
fahari yake idumu pindi liangazapo jua.
Kwake mataifa yote yabarikiwe;
watu wote wamwite mbarikiwa!
18Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,
ambaye peke yake hufanya miujiza.
19Jina lake tukufu na litukuzwe milele;
utukufu wake ujae ulimwenguni kote!
Amina, Amina!
20Mwisho wa sala za Daudi, mwana wa Yese.



Zaburi72;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: