Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 4 March 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 73...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah ni siku/wiki/mwezi  mwingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!

Basi, mimi niliye mfungwa kwa kuwa namtumikia Bwana, nawasihi muishi maisha yanayostahili wito mlioitiwa. Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi; vumilianeni nyinyi kwa nyinyi kwa mapendo. Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu.
Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...

Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja. Kuna Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja; kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote na yuko katika yote.
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Kila mmoja wetu amepewa neema kadiri ya kipimo alichojaliwa na Kristo. Kama yasemavyo Maandiko: “Alipopaa mbinguni juu kabisa, alichukua mateka; aliwapa watu zawadi.”
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


KITABU CHA TATU
(Zaburi 73–89)
Haki itatawala
(Zaburi ya Asafu)
1Hakika, Mungu ni mwema kwa watu wanyofu;
ni mwema kwa walio safi moyoni.
2Karibu sana ningejikwaa,
kidogo tu ningeteleza;
3maana niliwaonea wivu wenye kiburi,
nilipoona wakosefu wakifanikiwa.
4Maana hao hawapatwi na mateso;
miili yao ina afya na wana nguvu.
5Taabu za binadamu haziwapati hao;
hawapati mateso kama watu wengine.
6Kiburi kimekuwa mkufu wao shingoni,
uhasama ni kama nguo yao.
7Macho yao hufura kwa uovu;
mioyo yao hububujika mipango mibaya.
8Huwadhihaki wengine na kusema mabaya;
hujivuna na kupanga kufanya uhasama.
9Kwa vinywa vyao hutukana mbingu;
kwa ndimi zao hujitapa duniani.
10Hata watu wa Mungu wanawafuata,
hawaoni kwao chochote kibaya73:10 hawaoni … kibaya: Tafsiri yamkini ya Kiebrania kigumu. Wengine: Na kunywa maneno yao kama maji.
na kusadiki kila wanachosema.
11Wanasema: “Mungu hawezi kujua!
Mungu Mkuu hataweza kugundua!”
12Hivi ndivyo watu waovu walivyo;
wana kila kitu na wanapata mali zaidi.
13Je, nimetunza bure usafi moyoni,
na kujilinda nisitende dhambi?
14Mchana kutwa nimepata mapigo,
kila asubuhi nimepata mateso.
15Kama ningalisema hayo kama wao,
ningalikuwa mhaini miongoni mwa watu wako.
16Basi, nilijaribu kufikiria jambo hili,
lakini lilikuwa gumu mno kwangu,
17mpaka nilipoingia patakatifu pako.
Ndipo nikatambua yatakayowapata waovu.
18Kweli wewe wawaweka mahali penye utelezi;
wawafanya waanguke na kuangamia.
19Wanaangamizwa ghafla,
na kufutiliwa mbali kwa vitisho.
20Ee Bwana, uinukapo, wao hutoweka mara,
kama ndoto wakati mtu anapoamka asubuhi.
21Nilipoona uchungu moyoni
na kuchomwa rohoni,
22nilikuwa mpumbavu na mjinga,
nilikuwa kama mnyama mbele yako.
23Hata hivyo niko daima nawe, ee Mungu!
Wanishika mkono na kunitegemeza.
24Wewe waniongoza kwa mashauri yako;
mwishowe utanipokea kwenye utukufu.
25Mbinguni, nani awezaye kunisaidia ila wewe?
Na duniani hamna ninachotamani ila wewe!
26Hata nikikosa nguvu mwilini na rohoni,
wewe, ee Mungu, u mwamba wangu;
riziki yangu kuu ni wewe milele.
27Anayejitenga nawe, hakika ataangamia.
Anayekukana, utamwangamiza.
28Lakini, kwangu ni vema kuwa karibu na Mungu,
wewe Bwana Mwenyezi-Mungu ndiwe usalama wangu.
Nitatangaza mambo yote uliyotenda!


Zaburi73;1-28

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: