Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 28 February 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 71...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Yahweh..!Jehovah..! Adonai..!Elohim..!El Olam..!El Qanna..!
El Elyon..!El shaddai..!Emanueli...!-Mungu pamoja nasi...
Unastahili sifa Mungu wetu,Unastahili kuabudiwa Jehovah,
Unastahili kuhimidiwa Yahweh,Unastahili Kutukuzwa Baba wa Mbinguni....!


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Kutatokea chipukizi katika kisiki cha Yese, tawi litachipua mizizini mwake. Roho ya Mwenyezi-Mungu itakaa kwake, roho ya hekima na maarifa, roho ya shauri jema na nguvu, roho ya ujuzi na ya kumcha Mwenyezi-Mungu. Atafurahia kumcha Mwenyezi-Mungu. Hatahukumu kadiri ya mambo ya njenje, wala kuamua kufuatana na yale anayosikia.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Atawapatia haki watu maskini, atawaamulia sawasawa wanyonge nchini. Kwa neno lake ataiadhibu dunia, kwa tamko lake atawaua waovu. Haki itakuwa kama mkanda wa kujifunga, uaminifu utakaa naye kama mkanda kiunoni.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,

watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka...
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahweh ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu...
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahwe tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho 
akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Mbwamwitu ataishi pamoja na mwanakondoo, chui watapumzika pamoja na mwanambuzi. Ndama na wanasimba watakula pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ngombe na dubu watakula pamoja, ndama wao watapumzika pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe. Mtoto mchanga atacheza kwenye shimo la nyoka mtoto ataweza kutia mkono shimoni mwa nyoka wa sumu. Katika mlima mtakatifu wa Mungu hakutakuwa na madhara wala uharibifu. Maana kumjua Mwenyezi-Mungu kutaenea pote nchini, kama vile maji yajaavyo baharini.
Tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani, Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea
Kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masikio ya kusikia
sauti yako,Ukawaokoe na kuwalinda,ukawaponye kimwili na kiroho
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Amani ikatawale katika maisha yao,Upendo ukadumu kati yao...

Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako tukiamini Mungu wetu utawatendea sawasawa na mapenzi yako 
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
 Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee
kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu wa Mungu Baba ukae nanyi daima
Nawapenda.


Mungu tumaini la wazee
1Kwako ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama;
kamwe usiniache niaibike!
2Kwa uadilifu wako uniokoe na kunisalimisha;
unitegee sikio lako na kuniokoa!
3Uwe mwamba wangu wa kukimbilia usalama,
ngome imara ya kuniokoa,
kwani wewe ni mwamba na ngome yangu.
4Niokoe, ee Mungu wangu, mikononi mwa waovu,
kutoka makuchani mwa wabaya na wakatili.
5Maana wewe Bwana u tumaini langu;
tegemeo langu ee Mwenyezi-Mungu, tangu ujana wangu;
6nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu,
ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu.
Mimi nitakusifu wewe daima.
7Kwa wengi nimekuwa kioja,
lakini wewe u kimbilio langu imara.
8Kinywa changu kimejaa sifa zako,
na utukufu wako mchana kutwa.
9Wakati wa uzee usinitupe;
niishiwapo na nguvu usiniache.
10Maana maadui zangu wanasema vibaya juu yangu;
wanaovizia uhai wangu wanafanya mipango,
11na kusema: “Mungu amemwacha;
mfuateni na kumkamata,
kwani hakuna wa kumwokoa!”
12Usikae mbali nami, ee Mungu;
uje haraka kunisaidia, ee Mungu wangu.
13Wapinzani wangu wote waaibishwe na kuangamizwa;
wenye kutaka kuniumiza wapate aibu na fedheha.
14Lakini mimi nitakuwa na matumaini daima;
tena nitakusifu zaidi na zaidi.
15Kinywa changu kitatamka matendo yako ya haki,
nitatangaza mchana kutwa matendo yako ya wokovu
ijapokuwa hayo yanapita akili zangu.
16Nitataja matendo yako makuu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu;
nitatangaza kuwa ndiwe mwadilifu peke yako.
17Ee Mungu, wewe umenifunza tangu ujana wangu;
tena na tena, natangaza matendo yako ya ajabu.
18Usiniache, ee Mungu, niwapo mzee mwenye mvi,
hata nivitangazie vizazi vijavyo nguvu yako.
19Nguvu na uadilifu wako, ee Mungu,
vyafika mpaka mbingu za juu.
Wewe umefanya mambo makuu mno.
Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?
20Umenifanya nione taabu nyingi ngumu,
lakini utanirudishia tena uhai,
wewe utaniinua tena kutoka huko chini.
21Utaniongezea heshima yangu,
na kunifariji tena.
22Nitakusifu pia kwa kinubi,
kwa sababu ya uaminifu wako, ee Mungu wangu;
nitakuimbia sifa kwa zeze, ewe Mtakatifu wa Israeli.
23Nitapaza sauti kwa furaha,
ninapokuimbia wewe sifa zako,
na roho yangu itakusifu maana umeniokoa.
24Nitatamka uadilifu wako mchana kutwa,
maana waliotaka kuniumiza wameaibishwa na kufedheheshwa.



Zaburi71;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: