Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 13 November 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;Yobu 36...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Yahweh..!Jehovah..! Adonai..!Elohim..!El Olam..!El Qanna..!
El Elyon..!El shaddai..!Emanueli...!-Mungu pamoja nasi...
Unastahili sifa Mungu wetu,Unastahili kuabudiwa Jehovah,
Unastahili kuhimidiwa Yahweh,Unastahili Kutukuzwa Baba wa Mbinguni....!



Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Yule Mfilisti, naye akaanza kumwendea Daudi, na yule aliyemchukulia ngao yake akiwa mbele yake. Yule Mfilisti alipoangalia na kumwona vizuri Daudi, alimdharau, kwani Daudi alikuwa kijana tu, mwenye afya na wa kupendeza. Goliathi akamwuliza Daudi, “Sasa, hiyo fimbo ni ya nini? Unadhani mimi ni mbwa hata unijie kwa fimbo?” Mfilisti huyo akamlaani Daudi kwa miungu yake. Mfilisti akamwambia Daudi, “Njoo kwangu! Mwili wako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini!”

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazaretiyeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Lakini Daudi akamwambia Goliathi, “Wewe unanijia kwa upanga, mkuki na sime. Lakini mimi ninakujia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa askari wa Israeli, ambaye wewe umemtukana. Siku ya leo, Mwenyezi-Mungu atakutia mikononi mwangu. Nitakubwaga chini, nitakukata kichwa chako; na miili ya wanajeshi wa Wafilisti nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini. Ndipo dunia nzima itakapojua kuwa Mungu yuko katika Israeli. Watu wote waliokusanyika hapa leo, watajua kuwa Mwenyezi-Mungu hahitaji mikuki wala sime kuwaokoa watu. Hii ni vita ya Mwenyezi-Mungu, naye atawatia nyinyi nyote mikononi mwetu.” Goliathi akaanza tena kumwendea Daudi. Daudi akakimbia mbio kwenda kwenye mstari wa mapambano. Akatia mkono wake mfukoni mwake, akatoa jiwe moja, akalirusha kwa kombeo lake, akampiga nalo Goliathi kwenye paji la uso wake, jiwe likalipasua paji la Goliathi na kupenya ndani. Goliathi akaanguka chini kifudifudi. Ndivyo Daudi alivyomshinda Goliathi kwa kombeo lake na jiwe. Alimpiga yule Mfilisti na kumuua. Daudi hakuwa na upanga wowote mkononi mwake. Basi, akaenda mbio, akasimama juu ya Goliathi, akaufuta upanga wa Goliathi alani mwake, akamuua Goliathi kwa kumkata kichwa chake. Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao ameuawa, wakatimua mbio. Ndipo watu wa Israeli na watu wa Yuda, walipoanza kupiga kelele za ushindi, wakawafuatilia Wafilisti hadi Gathi, kwenye malango ya Ekroni, hata Wafilisti waliojeruhiwa vitani walienea njiani tangu Shaarimu hadi Gathi na Ekroni. Waisraeli walipotoka kuwafuatilia Wafilisti, waliteka nyara kambi yao. Daudi alikichukua kichwa cha yule Goliathi, Mfilisti, akakipeleka mjini Yerusalemu. Lakini silaha za Goliathi akaziweka katika hema lake.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Yahweh  tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni

Yahweh ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Shauli alipomwona Daudi akienda kumkabili yule Mfilisti Goliathi, alimwuliza Abneri, kamanda wa jeshi lake, “Abneri, huyu ni kijana wa nani?” Abneri alijibu, “Mfalme, kama uishivyo, mimi sijui.” Mfalme Shauli akamwambia, “Basi, uliza yeye ni kijana wa nani.” Mara tu Daudi aliporudi kambini baada ya kumuua Goliathi, Abneri alimchukua na kumpeleka kwa Shauli. Wakati huo Daudi alikuwa bado amechukua kichwa cha Goliathi mikononi mwake. Shauli akamwuliza Daudi, “Kijana, wewe ni mwana wa nani?” Daudi akajibu, “Mimi ni mwana wa mtumishi wako Yese, kutoka mji wa Bethlehemu.”

Tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani, Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea
Kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masikio ya kusikia
sauti yako,Ukawaokoe na kuwalinda,ukawaponye kimwili na kiroho
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Amani ikatawale katika maisha yao,Upendo ukadumu kati yao
 

Baba wa Mbinguni tunayaweke haya yote mikono mwako
tukiamini Mungu wetu utawatendea sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!



Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu
kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee
kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima
Nawapenda. 






1Kisha Elihu akaendelea kusema:
2“Nivumilie kidogo, nami nitakuonesha kitu;
maana bado ninacho cha kusema kwa niaba ya Mungu.
3Nitaleta hekima yangu kutoka mbali sana,
na kuonesha kwamba Muumba wangu ni mwadilifu.
4Kweli maneno yangu si ya uongo;
mwenye elimu kamili yuko hapa nawe.
5“Sikiliza Mungu ni mwenye nguvu
wala hamdharau mtu yeyote;
uwezo wa akili yake ni mkuu mno!
6Hawaachi waovu waendelee kuishi;
lakini huwapatia wanaodhulumiwa haki zao.
7Haachi kuwalinda watu waadilifu;
huwatawaza, wakatawala na kutukuka.
8Lakini kama watu wamefungwa minyororo,
wamenaswa katika kamba za mateso,
9Mungu huwaonesha matendo yao maovu,
na kwamba wao ni watu wenye kiburi.
10Huwafungua masikio wasikie mafunzo,
na kuwaamuru warudi na kuacha uovu.
11Wakimtii Mungu na kumtumikia,
hufanikiwa katika siku zao zote;
miaka yao yote huwa ya furaha.
12Lakini wasipomtii, huangamia kwa upanga,
na kufa kwa kukosa akili.
13“Wasiomcha Mungu hupenda kukasirika,
hawamlilii msaada anapowabana.
14Hufa wangali bado vijana,
maisha yao huisha kama ya walawiti.
15Lakini Mungu huwaokoa wanyonge kwa unyonge wao
hutumia shida zao kuwafumbua macho.
16Mungu alikuvuta akakutoa taabuni,
akakuweka mahali pa wasaa pasipo shida,
na mezani pako akakuandalia vinono.
17“Lakini sasa umehukumiwa kama mwovu,
hukumu ya haki imekukumba.
18Jihadhari ghadhabu isije ikakufanya ukadhihaki,
au ukubwa wa mali za kukukomboa ukakupotosha.
19Je, kilio chako kitafaa kukutoa taabuni,
au nguvu zako zote zitakusaidia?
20Usitamani usiku uje,
ambapo watu hufanywa watoweke walipo.
21Jihadhari! Usiuelekee uovu
maana umepatiwa mateso kukuepusha na uovu.
22Kumbuka ukuu wa uwezo wa Mungu;
nani awezaye kumfundisha kitu?
23Nani basi aliyeweza kumpangia njia yake,
au awezaye kumwambia: ‘Umekosea?’
24“Usisahau kuyasifu matendo yake;
ambayo watu wameyashangilia.
25Watu wote wameona aliyofanya Mungu;
binadamu huyaona kutoka mbali.
26Mungu ni mkuu mno hata hatuwezi kumjua;
muda wa maisha yake hauchunguziki.
27Yeye huyavuta kwake maji ya bahari,
na kutoka ukungu hufanya matone ya mvua.
28Huyafanya mawingu yanyeshe mvua,
na kuwatiririshia binadamu kwa wingi.
29Nani ajuaye jinsi mawingu yatandavyo,
au jinsi radi ingurumavyo angani kwake?
30Yeye huutandaza umeme wake kumzunguka,
na kuvifunika vilindi vya bahari.
31Kwa mvua huwalisha36:31 huwalisha: Au huwahukumu. watu
na kuwapatia chakula kwa wingi.
32Huukamata umeme kwa mikono yake,
kisha hulenga nao shabaha,
33Radi hutangaza ujio wake Mungu,
hata wanyama hujua kwamba anakuja.





Yobu36;1-33

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: