Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 31 July 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 30...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu..

Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!



Tuseme nini basi? Je, tuendelee kubaki katika dhambi ili neema ya Mungu iongezeke? Hata kidogo! Kuhusu dhambi sisi tumekufa – tutaendeleaje kuishi tena katika dhambi? Maana, mnajua kwamba sisi tuliobatizwa tukaungana na Kristo Yesu, tulibatizwa na kuungana na kifo chake. Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa kitendo kitukufu cha Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...




Maana, kama sisi tumeungana naye katika kufa kama yeye, vivyo hivyo tutaungana naye kwa kufufuliwa kutoka kwa wafu kama yeye. Tunajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na Kristo, ili hali ya dhambi iharibiwe, tusiwe tena watumwa wa dhambi. Kwa maana, mtu aliyekufa, amenasuliwa kutoka dhambini. Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye. Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka kwa wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena. Hivyo, kwa kuwa alikufa – mara moja tu – dhambi haina nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu. Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa, na hivyo kuzitii tamaa zake. Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni nyinyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka kwa wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu. Maana, dhambi haitawatawala tena, kwani hamko chini ya sheria, bali chini ya neema.



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua  njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...





Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? Hata kidogo! Mnajua kwamba mkijitolea nyinyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo – au watumwa wa dhambi na matokeo yake ni kifo, au wa utii na matokeo yake ni kufanywa kuwa waadilifu. Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini – namshukuru Mungu – mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea. Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu (hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya udhaifu wenu wenyewe). Kama vile wakati fulani mlivyojitolea nyinyi wenyewe kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu. Mlipokuwa watumwa wa dhambi mlikuwa huru mbali na uadilifu. Sasa, mlipata faida gani siku zile kutokana na mambo yale ambayo mnayaonea aibu sasa? Maana, matokeo ya mambo haya ni kifo! Lakini sasa mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uhai wa milele. Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi anayotoa Mungu ni uhai wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu.


Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.


Maandalio ya Pasaka

1Mfalme Hezekia aliwatumia ujumbe watu wote wa Israeli na Yuda, na pia akawaandikia barua wenyeji wa Efraimu na Manase, akiwaalika wote waje katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu Yerusalemu, ili kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka kwa heshima yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. 2Mfalme, viongozi na watu wote wa mji wa Yerusalemu waliafikiana kuiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka mnamo mwezi wa pili 3badala ya mwezi wa kwanza kama ilivyokuwa kawaida, kwa sababu idadi ya makuhani waliokuwa wamekwisha kujiweka wakfu ilikuwa ndogo, nao watu walikuwa bado hawajakusanyika Yerusalemu. 4Aidha, mpango huu ulimridhisha mfalme pamoja na watu wote waliokuwa wamekusanyika. 5Kwa hiyo waliamua kutoa tangazo kote nchini Israeli, kutoka Beer-sheba hadi Dani, kwamba watu waje Yerusalemu kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Ulikuwa umepita muda mrefu kabla watu hawajaiadhimisha Pasaka kulingana na sheria zake. 6Matarishi, kwa amri yake mfalme na maofisa wake, walipeleka barua kote nchini Israeli na Yuda. Barua hizo zilikuwa na ujumbe ufuatao:
“Enyi watu wa Israeli mlionusurika baada ya mashambulizi ya wafalme wa Ashuru. Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, ili naye apate kuwarudieni. 7Msiwe kama babu zenu na ndugu zenu ambao hawakuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, ambaye kama mnavyoona aliwaadhibu vikali. 8Msiwe wakaidi kama babu zenu, ila mtiini Mwenyezi-Mungu. Njoni katika hekalu lake ambalo amelitakasa milele, mumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili asiwakasirikie. 9Mkimrudia Mwenyezi-Mungu, wale ambao waliwateka ndugu zenu na watoto wenu, watawahurumia na kuwaacha warudi katika nchi hii. Kwa maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mwenye rehema na huruma, naye atawapokea ikiwa mtamrudia.”
10Basi, matarishi hao wakaenda toka mji mmoja hadi mwingine kote nchini Efraimu na Manase, wakafika hata Zebuluni. Lakini watu waliwacheka na kuwadhihaki. 11Hata hivyo, watu wachache miongoni mwa makabila ya Asheri, Manase na Zebuluni, walijinyenyekesha wakaja Yerusalemu. 12Nguvu ya Mungu ilikuwa ikifanya kazi katika Yuda, akawapa moyo kutii amri za mfalme na maofisa wake kadiri ya maagizo ya Mwenyezi-Mungu.

Kuiadhimisha Pasaka

13Watu wengi sana walijumuika mjini Yerusalemu mnamo mwezi wa pili, kuiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. 14Walianza kazi, wakaziondoa madhabahu zote zilizokuwa Yerusalemu, na nyingine zote zilizotumiwa kufukizia ubani, wakazibeba na kuzitupa katika Bonde la Kidroni. 15Siku ya kumi na nne ya mwezi huo walichinja mwanakondoo wa Pasaka. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketeza katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 16Walichukua nafasi zao hekaluni kulingana na maagizo yaliyokuwamo katika sheria za Mose, mtu wa Mungu. Walawi waliwapa makuhani damu ya tambiko, nao wakainyunyiza madhabahuni. 17Kwa vile wengi wa wale waliokusanyika hapo hawakuwa wamejitakasa, iliwabidi Walawi kuwachinjia wanakondoo wa Pasaka na kuwaweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. 18Aidha miongoni mwa kusanyiko hilo la watu, wengi wa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zebuluni, walikuwa wakiiadhimisha Pasaka kinyume cha maagizo. Hii ni kwa kuwa mfalme Hezekia aliwaombea akisema, “Mwenyezi-Mungu uliye mwema, msamehe yeyote yule 19atakayekuomba kwa moyo wake wote wewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hata ingawa si msafi kulingana na sheria za utakaso.” 20Mwenyezi-Mungu alikubali ombi la Hezekia, akawasamehe watu hao. 21Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika mjini Yerusalemu waliiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu kwa muda wa siku saba, wakiwa na furaha kubwa. Walawi na makuhani walimsifu Mwenyezi-Mungu kila siku, walimwimbia kwa nguvu zao zote. 22Mfalme Hezekia aliwasifu na kuwatia moyo makuhani kwa kuwa waliendesha ibada kwa ujuzi mwingi.

Adhimisho la pili

Baada ya kumaliza siku saba wakati ambao watu walikula, wakatoa sadaka za amani na kumtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, 23watu waliamua kwa kauli moja kuziendeleza sherehe kwa muda wa siku saba zaidi. Basi, wakaendelea kusherehekea kwa furaha kuu kwa muda wa siku saba zaidi. 24Mfalme Hezekia wa Yuda aliwapa watu waliokusanyika jumla ya mafahali 1,000 na kondoo 7,000. Hali kadhalika, wakuu wakawapa mafahali 1,000 na kondoo 10,000. Idadi kubwa ya makuhani walijitakasa. 25Kila mtu aliyehudhuria alifurahi sana. Watu wote wa Yuda, makuhani na Walawi, wakazi wa Yerusalemu waliohudhuria, wageni waliotoka nje ya Yerusalemu na wale walioishi Yuda, wote walifurahi sana. 26Kukawa na furaha kuu mno Yerusalemu, maana tangu enzi ya mfalme Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, jambo kama hilo lilikuwa halijatokea Yerusalemu. 27Kisha, makuhani na Walawi wakawaombea watu baraka zake Mwenyezi-Mungu, naye katika makao yake matakatifu huko mbinguni akayasikia maombi yao na kuyakubali.


2Mambo ya Nyakati30;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: