Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 13 July 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 18...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu....!!





Wanangu, sikilizeni mwongozo wa baba yenu, tegeni sikio mpate kuwa na akili. Maana ninawapa maagizo mema, msiyakatae mafundisho yangu. Mimi pia nilikuwa mtoto mwenye baba, nilikuwa mpole, kipenzi cha mama yangu. Baba yangu alinifundisha hiki: “Zingatia kwa moyo maneno yangu, shika amri zangu nawe utaishi. Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usisahau wala kupuuza maneno yangu. Usimwache Hekima, naye atakutunza; umpende, naye atakulinda. Jambo la msingi ni kujipatia hekima; toa vyote ulivyonavyo ujipatie akili. Mthamini sana Hekima, naye atakutukuza; ukimshikilia atakupa heshima. Atakuvika kilemba kizuri kichwani pako, atakupa taji maridadi.”

Tazama Jana imepita ee Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingineJehovah...
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha

na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Mwanangu, sikia na kuyapokea maneno yangu, ili upate kuwa na miaka mingi ya kuishi. Nimekufundisha njia ya hekima, nimekuongoza katika njia nyofu. Ukitembea hatua zako hazitazuiwa, wala ukikimbia hutajikwaa. Zingatia mafundisho ya Hekima na usimwache aponyoke, mshike kwa makini maana yeye ni uhai wako. Usijiingize katika njia ya waovu, wala usifuate mwenendo wa watu wabaya. Iepe njia hiyo wala usiikaribie; jiepushe nayo, uende zako.


Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Tukawe barua njema  ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi






Waovu kamwe hawalali wasipotenda uovu; hawapati usingizi wasipomkwaza mtu. Maana uovu ndicho chakula chao, ukatili ndiyo divai yao. Njia ya watu wema ni kama nuru ya alfajiri, ambayo hungaa zaidi na zaidi hata mchana kamili. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene, hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, sikiliza kwa makini maneno yangu, itegee sikio misemo yangu. Usiyaache yatoweke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako. Maana hayo ni uhai kwa mtu anayeyapata, ni dawa kwa mwili wake wote. Linda moyo wako kwa uangalifu wote, maana humo zatoka chemchemi za uhai. Tenga mbali nawe lugha potovu; wala midomo yako isitamke maneno madanganyifu. Uyaelekeze macho yako mbele kwa ujasiri, mtazamo wako uwe mbele moja kwa moja. Fikiria njia utakayochukua, na hatua zako zote zitakuwa kamili. Usigeukie kulia wala kushoto; epusha mguu wako mbali na uovu.



Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabuwote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



Nabii Mikaya amwonya Ahabu

(1Fal 22:1-28)

1Wakati mfalme Yehoshafati wa Yuda alipokuwa amekwisha kuwa mtu tajiri na mwenye heshima, alifanya mpango wa ndoa baina ya jamaa yake, na jamaa ya mfalme Ahabu wa Israeli. 2Baada ya miaka kadhaa Yehoshafati alikwenda Samaria kumtembelea mfalme Ahabu. Ahabu akamchinjia Yehoshafati kondoo na ng'ombe wengi, kwa heshima yake pamoja na watu waliokuwa pamoja naye, kisha akamshawishi aandamane naye kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi. 3Ahabu mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati mfalme wa Yuda, “Je, utaandamana nami kwenda kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi?” Naye akajibu, “Naam, mimi niko nawe, pia watu wangu ni watu wako. Tutakuwa pamoja nawe vitani.” 4Kisha Yehoshafati akaendelea kumwambia mfalme wa Israeli, “Lakini kwanza mwulize Mwenyezi-Mungu shauri.”
5Basi, Ahabu akaitisha kikao cha manabii wapatao 400, akawauliza, “Je, twende tukaushambulie mji wa Ramoth-gileadi, au nisiende?” Wao wakamjibu, “Nenda! Mungu atakupatia ushindi!” 6Lakini, Yehoshafati akauliza, “Je, hapa hakuna nabii mwingine wa Mwenyezi-Mungu ambaye twaweza kumwuliza shauri?” 7Naye mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Yupo bado mmoja, Mikaya mwana wa Imla. Yeye twaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu. Lakini namchukia kwa sababu yeye kamwe hatabiri jambo jema juu yangu, ila mabaya tu.” Yehoshafati akamwambia, “Si vizuri mfalme kusema hivyo.” 8Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli akamwita ofisa mmoja na kumwamuru, “Haraka, nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.” 9Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati, mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme. Wakati huo manabii wote walikuwa wakitoa unabii wao mbele yao. 10Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma, akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Washamu hata kuwaangamiza.’” 11Hata wale manabii wengine wakatabiri vivyo hivyo wakasema, “Nenda ukaushambulie Ramoth-gileadi, Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”
12Wakati huo, yule mjumbe aliyetumwa kwa Mikaya alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.” 13Lakini Mikaya akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, kile atakachoniambia Mungu wangu, ndicho nitakachosema.”
14Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme akamwuliza, “Je, twende18:14 Kiebrania: Twende. Lakini Taz 1Fal 22:6 kupigana vitani huko Ramoth-gileadi au nisiende?” Mikaya akajibu, “Nenda ushinde; Mwenyezi-Mungu atawatia mikononi mwako.” 15Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba kila unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?” 16Naye Mikaya akasema, “Niliwaona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; waache warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’”
17Hapo mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia, kamwe hatatabiri jema juu yangu, ila mabaya tu?” 18Kisha Mikaya akasema: “Haya, sikia neno la Mwenyezi-Mungu: Nilimwona Mwenyezi-Mungu ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lake lote la mbinguni limesimama upande wake wa kulia na wa kushoto. 19Ndipo Mwenyezi-Mungu akauliza, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu mfalme wa Israeli aende akaangamie huko Ramoth-gileadi?’ Kila mmoja akajibu alivyofikiri. 20Kisha, pepo mmoja akajitokeza mbele ya Mwenyezi-Mungu, akasema, ‘Mimi nitamshawishi.’ Mwenyezi-Mungu akamwuliza, ‘Kwa mbinu gani?’ 21Naye akajibu, ‘Nitakwenda na kuwafanya manabii wake wote waseme uongo.’ Mwenyezi-Mungu akamwambia, ‘Wewe utamshawishi na utafaulu; haya nenda ukafanye hivyo.’ 22Basi ndivyo ilivyo: Mwenyezi-Mungu amewafanya hawa manabii wako waseme uongo. Lakini Bwana amenena mabaya juu yako!”
23Hapo nabii Sedekia mwana wa Kenaana akamkaribia Mikaya, akampiga kofi shavuni na kumwuliza, “Kwa njia gani Roho wa Mwenyezi-Mungu ameniacha na akaja kunena nawe?” 24Mikaya akamjibu, “Siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani kujificha ndipo utakapojua.”
25Naye mfalme wa Israeli akatoa amri, “Mkamateni Mikaya mrudisheni kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoashi, mwana wa mfalme. 26Waambie wamfunge gerezani na kumlisha mkate kidogo na maji, mpaka nitakaporudi salama.” 27Ndipo Mikaya aliposema, “Ukirudi salama, basi, utajua Mwenyezi-Mungu hakunena nami.” Kisha akaendelea kusema, “Sikieni, enyi watu wote!”

Kifo cha Ahabu

(1Fal 22:29-35)

28Basi, mfalme wa Israeli akaenda pamoja na Yehoshafati mfalme wa Yuda kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi. 29Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Mimi nitavaa mavazi yasiyo ya kifalme kuingia vitani, lakini wewe utavaa mavazi yako ya kifalme.” Hivyo mfalme wa Israeli akaenda vitani bila kuvaa mavazi ya kifalme.
30Mfalme wa Aramu alikuwa amewaamuru makapteni wake waliosimamia magari yake ya kukokotwa akisema, “Msipigane na mtu yeyote yule mkubwa au mdogo, ila tu na mfalme wa Israeli.” 31Baadaye makapteni hao walipomwona Yehoshafati, walisema, “Huyu mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo, walimwelekea kumshambulia; lakini Yehoshafati akapiga kelele, na Mwenyezi-Mungu akamwokoa. Mungu akawaondoa wale waliokuwa karibu kumshambulia. 32Makapteni walipotambua kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, waliacha kumshambulia, wakarudi. 33Lakini askari mmoja wa Aramu akauvuta upinde wake kwa kubahatisha, mshale ukamchoma mfalme wa Israeli katika nafasi ya kuungana kwa vazi lake la chuma. Hapo Ahabu akamwambia dereva wa gari lake, “Nimejeruhiwa! Geuza gari uniondoe vitani.” 34Nayo mapigano siku hiyo, yakazidi kuwa makali huku mfalme wa Israeli amejiegemeza mwenyewe garini akiwaelekea Washamu mpaka jioni. Halafu mnamo machweo ya jua, alifariki.




2Mambo ya Nyakati18;1-34

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: