Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 18 July 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 21...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Yahweh..!Jehovah..! Adonai..!Elohim..!El Olam..!El Qanna..!
El Elyon..!El shaddai..!Emanueli...!-Mungu pamoja nasi...
Unastahili sifa Mungu wetu,Unastahili kuabudiwa Jehovah,
Unastahili kuhimidiwa Yahweh,Unastahili Kutukuzwa Baba wa Mbinguni....!



Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Yesu akaendelea kusema, “Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake? Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo. Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote. Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: ‘Bwana wangu amekawia kurudi,’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi, bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua. Atamwadhibu vibaya na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.



Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....






“Wakati huo, ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi. Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara. Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta. Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao. Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wasichana wote walisinzia, wakalala. Usiku wa manane kukawa na kelele: ‘Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.’ Hapo wale wasichana wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao. Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: ‘Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.’ Lakini wale wenye busara wakawaambia, ‘Hayatatutosha sisi na nyinyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!’ Basi, wale wasichana wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wasichana waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la harusi, kisha mlango ukafungwa. Baadaye wale wasichana wengine wakaja, wakaita: ‘Bwana, Bwana, tufungulie!’ Lakini yeye akawajibu, ‘Nawaambieni kweli, siwajui nyinyi.’” Kisha Yesu akasema, “Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Yahweh  tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni

Yahweh ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...





“Wakati huo itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ngambo: Aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake. Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: Mmoja fedha talanta tano, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri. Mara yule aliyekabidhiwa fedha talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano. Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili. Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaenda, akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake. “Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake. Mtumishi aliyekabidhiwa fedha talanta tano akaja amechukua talanta tano faida, akamwambia, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.’ Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’ “Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.’ Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’ “Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya. Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.’ “Bwana wake akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya. Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake! Basi, mnyanganyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi. Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’




Tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea
Kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masikio ya kusikia
sauti yako,Ukawaokoe na kuwalinda,ukawaponye kimwili na kiroho
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Amani ikatawale katika maisha yao,Upendo ukadumu kati yao
 
Baba wa Mbinguni tunayaweke haya yote mikono mwako
tukiamini Mungu wetu utawatendea sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu
kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee
kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima
Nawapenda. 
  



Mwisho wa utawala wa Yehoshafati

(1Fal 22:41-50)

1Hatimaye Yehoshafati alifariki na kuzikwa pamoja na babu zake katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi; naye Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake.

Mfalme Yehoramu wa Yuda

(2Nya 8:17-24)

2Yehoramu alikuwa na ndugu kadhaa wana wa Yehoshafati: Azaria, Yehieli, Zekaria, Azaria, Mikaeli na Shefatia. 3Baba yao aliwapa zawadi kubwakubwa za fedha, dhahabu na vitu vingine vya thamani, na pia miji ya Yuda yenye ngome. Lakini kwa sababu Yehoramu ndiye aliyekuwa mzaliwa wake wa kwanza, Yehoshafati akampa ufalme atawale badala yake. 4Yehoramu alipokikalia kiti cha enzi na utawala wake ulipokuwa umekwisha imarika, yeye aliwaua ndugu zake wote kwa upanga, na pia baadhi ya wakuu wa Israeli.
5Yehoramu alianza kutawala akiwa na umri wa miaka thelathini na miwili. Alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka minane. 6Alizifuata njia mbaya za mfalme Ahabu na za wafalme wengine wa Israeli kama jamaa ya Ahabu ilivyofanya kwa sababu mkewe alikuwa binti ya Ahabu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, 7lakini Mwenyezi-Mungu hakutaka kuangamiza ukoo wa Daudi kwa ajili ya agano alilokuwa amefanya na Daudi na pia kwa sababu alikuwa ameahidi wazawa wake wataendelea kutawala milele.
8Wakati wa enzi ya Yehoramu, watu wa Edomu waliasi utawala wa Yuda, wakamtawaza mfalme wao wenyewe. 9Kwa hiyo, Yehoramu pamoja na makamanda wake na magari yake yote aliondoka akawashambulia Waedomu waliokuwa wamemzunguka yeye pamoja na makamanda wake na magari. 10Hivyo Edomu imeuasi utawala wa Yuda mpaka sasa. Wakati huohuo pia, wakazi wa Libna nao wakauasi utawala wake kwa sababu Yehoramu alikuwa amemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake. 11Isitoshe, alitengeneza mahali pa kuabudia miungu mingine katika milima ya Yuda na kusababisha wakazi wa Yerusalemu kukosa uaminifu na watu wa Yuda kupotoka.
12Nabii Elia alimpelekea mfalme Yehoramu barua ifuatayo:
“Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Daudi babu yako, anakulaani kwa sababu hukufuata mwenendo wa Yehoshafati baba yako, au wa Asa mfalme wa Yuda. 13Badala yake umeifuata mienendo ya wafalme wa Israeli na kuwaongoza watu wa Yuda na Yerusalemu katika kukosa uaminifu kama vile Ahabu, na wafalme wa jamaa yake waliomfuata walivyowaongoza watu wa Israeli kukosa uaminifu. Pia umewaua ndugu zako, ndugu za baba mmoja waliokuwa watu wema zaidi kuliko wewe. 14Kwa sababu hiyo, Mwenyezi-Mungu atawaadhibu vikali watu wako, wanao, wake zako na kuiharibu mali yako yote. 15Wewe mwenyewe utaugua maradhi mabaya ya tumbo, ambayo yataongezeka siku hata siku, mpaka matumbo yako yatoke nje.”
16Kulikuwa na Wafilisti na Waarabu wengine waliokuwa wakikaa karibu na Waethiopia. Hawa, Mwenyezi-Mungu aliwapandisha hasira ili wapigane na Yehoramu. 17Basi, wakaishambulia nchi ya Yuda, wakaiteka mali yote iliyokuwamo katika jumba la mfalme na kuwachukua mateka wanawe wote na wake zake, isipokuwa Ahazia, mwanawe mdogo.
18Baada ya haya yote, Mwenyezi-Mungu akamletea mfalme ugonjwa wa tumbo usioponyeka. 19Aliendelea kuugua, na ugonjwa wake ukawa unaongezeka siku hata siku, hata kufikia mwisho wa mwaka wa pili, akafariki dunia katika maumivu makali. Watu hawakuwasha moto kuomboleza kifo chake kama walivyowafanyia babu zake.
20Yehoramu alianza kutawala akiwa na umri wa miaka thelathini na miwili; akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka minane. Wakati alipofariki, hakuna mtu yeyote aliyemsikitikia. Alizikwa katika mji wa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme.



2Mambo ya Nyakati21;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: