Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 27 July 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 28...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu....!!




Basi, mimi niliye mfungwa kwa kuwa namtumikia Bwana, nawasihi muishi maisha yanayostahili wito mlioitiwa. Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi; vumilianeni nyinyi kwa nyinyi kwa mapendo. Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja. Kuna Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja; kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote na yuko katika yote. Kila mmoja wetu amepewa neema kadiri ya kipimo alichojaliwa na Kristo. Kama yasemavyo Maandiko: “Alipopaa mbinguni juu kabisa, alichukua mateka; aliwapa watu zawadi.”



Tazama Jana imepita ee Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingineJehovah...
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha

na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti 

yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....




Basi, inaposemwa: “Alipaa juu,” ina maana gani? Maana yake ni kwamba, kwanza alishuka mpaka chini kabisa duniani. Basi, huyo aliyeshuka hapa duniani ndiye aliyepaa juu ya mbingu zote apate kuujaza ulimwengu. Ndiye aliyewapa watu zawadi: Wengine aliwajalia wawe mitume, wengine manabii, wengine wawe waeneza Injili, wengine wachungaji na waalimu. Alifanya hivyo apate kuwatayarisha watu wote wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma ya Kikristo ili kuujenga mwili wa Kristo, na hivyo sote tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe. Basi, hatutakuwa tena kama watoto, tukitupwa na kupeperushwa huko na huko kwa kila upepo wa mafundisho wanayozua watu wadanganyifu ili wawapotoshe wengine kwa hila. Kama tukiuzingatia ukweli kwa moyo wa mapendo tutakua katika kila jambo kulingana na Kristo ambaye ndiye kichwa; chini ya uongozi wake, viungo vyote vya mwili hushikamana pamoja, na mwili wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo vyake. Basi, kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo, mwili wote hukua na kujijenga katika upendo.




Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Tukawe barua njema  ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...





Basi, kwa jina la Bwana, nawaonyeni: Msiishi tena kama watu wasiomjua Mungu, ambao fikira zao zimekuwa upuuzi mtupu, na akili zao zimo gizani. Wako mbali na uhai wa Mungu kwa sababu ya upumbavu ulio ndani yao na ukaidi wao. Wamepotoka na hawana aibu, wamejitosa katika ufisadi; hufanya kwa pupa kila aina ya mambo ya aibu. Lakini nyinyi hamkujifunza hivyo juu ya Kristo. Ni dhahiri kwamba mlisikia barabara habari zake, na mkiwa wafuasi wake mkafundishwa ukweli ulivyo katika Yesu. Basi, acheni mwenendo wenu wa awali, yaani ule utu wenu wa kale uliokuwa unaangamizwa kwa tamaa zake danganyifu. Jirekebisheni upya rohoni na katika fikira zenu. Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu. Kwa hiyo, acheni uongo. Kila mmoja anapaswa kumwambia mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo. Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima. Msimpe Ibilisi nafasi. Aliyekuwa akiiba, asiibe tena, bali na aanze kufanya kazi njema kwa mikono yake, apate kuwa na kitu cha kumsaidia mtu aliye maskini. Maneno mabaya hata yasisikike kamwe miongoni mwenu; kila mara maneno yenu yawe ya kufaa na ambayo hujenga na kuwasaidia wengine, ili yawaneemeshe wasikilizaji wenu. Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, maana Roho huyo ni alama ya Mungu kwenu kwamba nyinyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku itakuja ambapo Mungu atawakomboeni. Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele na matusi. Acheni kila uovu! Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe nyinyi kwa njia ya Kristo.



Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabuwote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



Mfalme Ahazi wa Yuda

(2Fal 16:1-4)

1Ahazi alianza kutawala akiwa na umri wa miaka ishirini; alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Yeye, hakufuata mfano mzuri wa Daudi babu yake, bali alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, 2na kufuata mienendo ya wafalme wa Israeli. Isitoshe, alitengeneza hata sanamu za kusubu za Mabaali, 3akafukiza ubani kwenye Bonde la mwana wa Hinomu na kuwateketeza wanawe kama tambiko, akiiga desturi za kuchukiza za watu ambao walifukuzwa na Mwenyezi-Mungu wakati Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini. 4Alitoa tambiko na kufukiza ubani mahali pa kuabudia miungu mingine, vilimani na chini ya kila mti wenye majani mabichi.

Vita dhidi ya Shamu na Israeli

(2Fal 16:5)
5Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, alimwacha mfalme Ahazi ashindwe na mfalme wa Aramu ambaye pia alichukua mateka watu wake wengi, akarudi nao Damasko. Kadhalika, alimfanya ashindwe na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, ambaye alimshinda na kuua watu wengi sana. 6Aliua askari mashujaa wa Yuda 120,000 katika siku moja. Ilitokea hivyo kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. 7Zikri, askari mmoja shujaa wa Israeli, alimuua Maaseya, mwana wa mfalme, Azrikamu, kamanda wa Ikulu, na Elkana aliyekuwa mtu wa pili chini ya mfalme. 8Jeshi la Israeli lilichukua mateka ndugu zao watu laki mbili wakiwemo wanawake na watoto. Waliwachukua hadi Samaria pamoja na mali nyingi waliyoteka nyara.

Nabii Odedi

9Baadaye kidogo mtu mmoja, jina lake Odedi, nabii wa Mwenyezi-Mungu, alikuwa anakaa Samaria. Yeye alitoka kuwalaki wanajeshi wa Israeli pamoja na mateka wao wa Yuda walipokuwa karibu kuingia Samaria, akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, alikuwa amewakasirikia watu wa Yuda, ndiyo maana akawatia mikononi mwenu lakini mmewaua kwa hasira. Tendo hilo limefika mbinguni. 10Sasa mnanuia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Je, hamtambui ya kuwa nyinyi pia mmetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu? 11Sasa sikieni yale nisemayo: Warudisheni ndugu zenu na dada zenu mliowateka, maana ghadhabu kali ya Mwenyezi-Mungu iko juu yenu.”
12Nao wakuu fulani wa Efraimu, Azaria mwana wa Yohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, pia waliwashutumu hao waliotoka vitani. 13Wakawaambia, “Msiwalete humu mateka hao, kwa sababu mnanuia kutuletea hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu; tendo hili huku litakuwa nyongeza ya dhambi yetu na hatia yetu; kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa na kuna ghadhabu kali juu ya Israeli.” 14Hivyo, wanajeshi waliwaacha mateka wao na nyara zote mbele ya wakuu na mkutano wote. 15Wale wakuu waliotajwa majina yao waliwachukua mateka na kwa kutumia nyara wakawavika mateka ambao hawakuwa na nguo; waliwapatia ndara, chakula na vinywaji, na kuwapaka mafuta. Wale ambao walikuwa hawajiwezi, wakawabeba kwa punda, wakawachukua mateka wote hadi Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wao wakarudi Samaria.

Ahazi aomba msaada kutoka Ashuru

(2Fal 16:7-9)

16Wakati huo, mfalme Ahazi alituma wajumbe kwa mfalme28:16 mfalme: Kiebrania: Wafalme. wa Ashuru kuomba msaada, 17kwa sababu Waedomu walikuwa wamekuja tena, wakaivamia nchi ya Yuda, wakawashinda na kuchukua mateka wengi. 18Wakati huohuo pia, Wafilisti walikuwa wakiishambulia miji ya Shefela na Negebu ya Yuda. Waliiteka miji ya Beth-shemeshi, Ayaloni, Gederothi, Soko na vijiji vyake, Timna na vijiji vyake, Gimzo na vijiji vyake, wakafanya makao yao huko. 19Kwa sababu mfalme Ahazi wa Israeli28:19 Baadhi ya maandiko na tafsiri mbalimbali zina Yuda huku ni kusahihisha ingawa huenda mwandishi alimaanisha kuwa alifanya mabaya kama wafalme wa Israeli. alikuwa na ukatili kwa watu wake, na alikosa uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu aliwafanya watu wa Yuda wakose nguvu. 20Tiglath-pileseri, mfalme wa Ashuru alimshambulia badala ya kumtia nguvu. 21Ahazi alichukua dhahabu kutoka katika nyumba ya Mungu, kutoka ikulu na nyumba za wakuu, akampa mfalme wa Ashuru kama kodi; lakini hili pia halikumsaidia kitu.

Dhambi za Ahazia

22Wakati alipokuwa taabuni zaidi, mfalme huyu Ahazi alizidi kumwasi Mwenyezi-Mungu. 23Maana aliitolea tambiko miungu ya Damasko iliyokuwa imemshinda vitani akisema, “Maadamu miungu ya Shamu iliwasaidia wafalme wa Shamu, nikiitolea tambiko huenda ikanisaidia nami pia.” Lakini hiyo ilisababisha kuangamia kwake na taifa lote la Israeli. 24Zaidi ya hayo, alivikusanya vifaa vyote vya nyumba ya Mungu, akavikatakata vipandevipande, kisha akaifunga milango ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kujijengea madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu. 25Na katika kila mji wa Yuda, alitengeneza mahali pa kufukizia ubani miungu mingine. Kwa kutenda hivyo, alimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake.
26Matendo yake mengine na mienendo yake yote, kutoka mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda na Israeli. 27Mfalme Ahazi alifariki, akazikwa mjini Yerusalemu, lakini si katika makaburi ya wafalme wa Israeli. Naye Hezekia mwanawe, akatawala mahali pake.




2Mambo ya Nyakati28;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: