Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 24 July 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 25...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu..

Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!




Mimi Paulo, niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Sosthene, tunawaandikia nyinyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho. Nyinyi mmefanywa watakatifu katika kuungana na Kristo Yesu, mkaitwa muwe watu wa Mungu, pamoja na watu wote popote wanaomwomba Bwana wetu Yesu Kristo aliye Bwana wao na wetu pia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...



Ninamshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu kwa sababu amewatunukia nyinyi neema yake kwa njia ya Kristo Yesu. Maana, kwa kuungana na Kristo mmetajirishwa katika kila kitu. Mmejaliwa elimu yote na uwezo wote wa kuhubiri. Maana ujumbe juu ya Kristo umethibitishwa ndani yenu, hata hampungukiwi kipaji chochote cha kiroho mkiwa mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye atawaimarisheni nyinyi mpaka mwisho mpate kuonekana bila hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita nyinyi muwe na umoja na Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua  njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...




Ndugu, nawasihini kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo: Pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe na fikira moja na nia moja. Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa jamaa ya Kloe, zaonesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu. Nataka kusema hivi: Kila mmoja anasema chake: Mmoja husema, “Mimi ni wa Paulo”, mwingine: “Mimi ni wa Apolo”, mwingine: “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine: “Mimi ni wa Kristo.” Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa tu Krispo na Gayo. Kwa hiyo hakuna awezaye kusema amebatizwa kwa jina langu. ( Samahani, nilibatiza pia jamaa ya Stefana; lakini zaidi ya hawa, sidhani kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote). Kristo hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Habari Njema; tena, niihubiri bila kutegemea maarifa ya hotuba za watu, kusudi nguvu ya kifo cha Kristo msalabani isibatilishwe.


 Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.

Mfalme Amazia wa Yuda

(2Fal 14:2-6)

1Amazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, akatawala kwa muda wa miaka ishirini na mitano katika Yerusalemu. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. 2Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa hakuyatenda kwa moyo mnyofu. 3Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani aliwaua watumishi waliomuua mfalme baba yake. 4Lakini hakuwaua watoto wao, kama ilivyoandikwa katika sheria zilizomo katika kitabu cha Mose, ambapo Mwenyezi-Mungu anasema: “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”

Vita dhidi ya Edomu

(2Fal 14:7)

5Mfalme Amazia aliwakusanya wanaume wa makabila ya Yuda na Benyamini, akawapanga katika vikosi mbalimbali kulingana na koo zao, akawaweka chini ya makamanda wa maelfu na wa mamia. Alipowakagua wale wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, alipata jumla ya watu 300,000. Wote walikuwa watu wateule, tayari kwa vita, hodari wa kutumia mikuki na ngao. 6Tena, alikodisha askari wengine mashujaa 1,000 kutoka Israeli, kwa gharama ya kilo 3,000 za fedha. 7Lakini mtu wa Mungu alimwendea, akamwambia, “Ee mfalme, usiende vitani pamoja na hawa askari wa Israeli, maana Mwenyezi-Mungu hayuko pamoja na watu wa Israeli. Hayuko pamoja na hawa Waefraimu wote. 8Bali, hivyo, hata ukiwa hodari vitani,25:8 maana katika Kiebrania si dhahiri. Mungu atakufanya ushindwe na maadui, kwa kuwa Mungu ana nguvu kumpa binadamu ushindi au kumfanya binadamu ashindwe.”
9Amazia akamwuliza huyo mtu wa Mungu, “Tutafanyaje na fedha yote ambayo nimekwisha wapa wanajeshi wa Israeli?” Naye akamjibu, “Mwenyezi-Mungu anaweza kukupa zaidi ya hiyo.” 10Hapo Amazia akawaachia wanajeshi waliotoka Efraimu warudi makwao. Basi wakarejea kwao wakiwa wamewakasirikia sana watu wa Yuda. 11Amazia alijipa moyo akaliongoza jeshi lake hadi Bonde la Chumvi. Hapo akapigana na kuwaua watu 10,000 wa Seiri. 12Waliteka watu 10,000, wakawapandisha juu ya jabali na kuwatupa chini miambani, wakapondeka vipandevipande. 13Wakati huohuo, wale wanajeshi Waisraeli ambao Amazia aliwaachia warudi kwao akiwakataza wasiandamane naye vitani, walikwenda na kuishambulia miji ya Yuda, toka Samaria hadi Beth-horoni, wakaua watu 3,000 na kuteka nyara nyingi.
14Amazia aliporejea baada ya kuwashinda Waedomu, alileta miungu ya Waedomu akaifanya kuwa miungu yake, akaisujudia na kuifukizia ubani. 15Haya yalimkasirisha sana Mwenyezi-Mungu, akatuma nabii kwa Amazia. Nabii huyo akamwuliza Amazia, “Kwa nini unategemea miungu ya watu wengine ambayo hata haikuweza kuwaokoa watu wake wenyewe kutoka mikononi mwako?”
16Lakini hata kabla hajamaliza kusema, Amazia alimkata kauli akamwambia, “Nyamaza! Tulikufanya lini mshauri wa mfalme? Wataka kuuawa?”
Nabii akanyamaza, lakini akasema, “Ninafahamu kuwa Mungu ameamua kukuangamiza kwa maana umetenda haya yote, kisha unapuuza shauri langu.”

Vita didhi ya Israeli

(2Fal 14:8-20)

17Basi, Amazia mfalme wa Yuda alifanya shauri, akatuma ujumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli, akamwambia, “Njoo tupambane.”25:17 tupambane: Kiebrania neno kwa neno: Uso. 18Lakini Yoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia akisema, “Siku moja, mchongoma wa Lebanoni uliuambia mwerezi wa hukohuko Lebanoni, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu!’ Lakini mnyama mmoja wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mchongoma huo. 19Sasa wewe Amazia unasema, ‘Nimewaua Waedomu;’ na moyo unakufanya ujivune. Basi, kaa nyumbani mwako; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?”
20Lakini Amazia hakujali kwa kuwa lilikuwa kusudi la Mungu ili awaweke mkononi mwa maadui zao kwa sababu alitegemea miungu ya Edomu. 21Kwa hiyo, Yehoashi, mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia, mfalme wa Yuda, huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda. 22Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi nyumbani kwake. 23Halafu Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi, akampeleka hadi Yerusalemu. Huko, aliubomoa ukuta wa mji huo, kuanzia Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200. 24Taz 2Nya 25:17 Alichukua dhahabu yote na fedha hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu chini ya ulinzi wa Obed-edomu; pia alichukua hazina ya ikulu na mateka kisha akarudi Samaria.
25Amazia mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha mfalme Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli. 26Matendo mengine yote ya Amazia kutoka mwanzo hadi mwisho yameandikwa katika Kitabu cha Habari za Wafalme wa Yuda na Israeli. 27Njama za kumuua Amazia zilifanywa Yerusalemu tangu alipomwacha Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo alikimbilia Lakishi. Lakini maadui walituma watu Lakishi wakamuua huko. 28Maiti yake ililetwa juu ya farasi, na kuzikwa kwenye makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi.




2Mambo ya Nyakati25;1-28

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: