Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 5 July 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 12...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Jehovah  Jireh..!Jehovah Nissi..!Jehovah Raah..!
Jehovah Rapha..!Jehovah Shammah..!Jehovah Shamlom..!
Emanuel-Mungu pamohja nasi..!!
Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni..!



Daudi alikimbia kutoka Nayothi katika Rama, akaenda mpaka kwa Yonathani, akamwambia, “Nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemtendea baba yako dhambi gani hata ajaribu kuyaangamiza maisha yangu?” Yonathani akamjibu, “Hilo na liwe mbali nawe. Hutakufa. Baba yangu hafanyi jambo lolote, liwe kubwa au dogo, bila ya kunieleza. Hata jambo hili hawezi kunificha. Sivyo ilivyo hata kidogo.” Daudi akaapa pia, “Hakika baba yako anajua vizuri unavyonipenda; na anafikiri kukuficha juu ya jambo hili ili usihuzunike atakapolitenda. Lakini, kwa vyovyote vile, naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, nawe ulivyo hai, kwamba kati yangu na mauti ipo hatua moja tu!” Yonathani akamwambia, “Lolote utakalosema nitakutendea.”



Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...



Daudi akamwambia, “Kesho ni sherehe za mwezi mwandamo, nami natazamiwa kuwapo mezani kula pamoja na mfalme. Lakini niache, nikajifiche huko shambani hadi siku ya tatu jioni. Baba yako akinikosa mezani kwa chakula, akauliza habari zangu, basi mwambie, ‘Daudi amenisihi nimpe ruhusa ili aende mjini kwake Bethlehemu, kuhudhuria tambiko ya kila mwaka pamoja na jamaa yake’. Ikiwa ataona hilo ni sawa, basi, ujue kuwa mambo yangu, mimi mtumishi wako, yako sawa. La sivyo, kusudi lake juu yangu ni baya. Hivyo nifanyie kwa hisani yako kwani umefanya agano takatifu nami, mimi mtumishi wako, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Lakini, kama nimefanya kosa basi, na uniue wewe mwenyewe; kwa nini unipeleke kwa baba yako ili aniue?” Yonathani akamjibu, “Wazo hilo na liwe mbali nawe. Hakika, kama ningejua kuwa baba yangu amekusudia mabaya juu yako nisingekuficha.” Daudi akauliza, “Nitajuaje ikiwa baba yako atakujibu kwa ukali?”



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe kama inavyokupendeza wewe....




Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi



Yonathani akamjibu, “Njoo twende shambani!” Basi, wakaenda. Yonathani akamwambia Daudi, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, na awe shahidi yetu. Kesho au kesho kutwa, wakati kama huu nitamwuliza baba yangu. Ikiwa msimamo wake juu yako ni mzuri nitakueleza. Mwenyezi-Mungu na aniue ikiwa Shauli anakusudia kukudhuru, nami nisikutahadharishe ili uende mahali mbali ambapo utakuwa salama. Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu. Ikiwa nitaendelea kuwa hai basi, nioneshe ule upendo thabiti wa Mwenyezi-Mungu, ili nisife, tena usiache kuitendea jamaa yangu kwa uaminifu milele. Na Mwenyezi-Mungu atakapowakatilia mbali adui zako kutoka duniani, naomba na jina langu lisikatiliwe mbali kutoka jamaa yako. Mwenyezi-Mungu awalipize kisasi adui zako.”



Tazama wenye shida/tabu,watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh tunaomba  ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu  unajua haja za mioyo ya kila mmoja
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Jehovah ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.




Wamisri waivamia Yuda

(1Fal 14:25-28)

1Ikawa utawala wa Rehoboamu ulipokwisha imarika na kuwa na nguvu, yeye pamoja na watu wake wote waliacha kutii sheria ya Mwenyezi-Mungu. 2Katika mwaka wa tano wa utawala wake, kwa sababu hawakumtii Mwenyezi-Mungu, Shishaki, mfalme wa Misri aliushambulia Yerusalemu, 3akiwa na magari 1,200, wapandafarasi 60,000, na askari wengi mno wasiohesabika, waliotoka Misri pamoja naye: Walibia, Wasukii na Waethiopia. 4Aliiteka miji yenye ngome katika Yuda, akafika hadi Yerusalemu. 5Kisha Nabii Shemaya alimwendea mfalme Rehoboamu na wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu ambapo walikimbilia ili kumwepuka Shishaki, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Nyinyi mmeniacha mimi, kwa hiyo basi, nami nimewaacha nyinyi na kuwatia mikononi mwa Shishaki.’”
6Ndipo wakuu wa Israeli na mfalme wakajinyenyekesha, wakasema, “Mwenyezi-Mungu ametenda sawa.”
7Mwenyezi-Mungu alipoona ya kuwa wamejinyenyekesha, alizungumza tena na nabii Shemaya, akamwambia, “Wamejinyenyekesha, sitawaangamiza, bali nitawaokoa baada ya muda mfupi. Sitaushushia mji wa Yerusalemu ghadhabu yangu kuuharibu kwa mkono wa Shishaki, 8lakini watamtumikia ili wapate kujua tofauti iliyopo kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa duniani.”
9Basi, mfalme Shishaki wa Misri aliushambulia Yerusalemu, akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu, pamoja na ngao za dhahabu alizozitengeneza mfalme Solomoni. 10Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu. 11Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi waliiingia wakazibeba ngao hizo na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi. 12Alipojinyenyekesha, Mwenyezi-Mungu aliacha kumghadhibikia na hakumwangamiza kabisa. Zaidi ya hayo, hali ya nchi ya Yuda ilikuwa nzuri.

Muhtasari wa utawala wa Rehoboamu

13Hivyo mfalme Rehoboamu alijiimarisha zaidi katika Yerusalemu, akaitawala Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu aliitwa Naama, kutoka Amoni. 14Rehoboamu alitenda maovu, kwa maana hakunuia kumtafuta Mwenyezi-Mungu kwa moyo. 15Matendo yote ya mfalme Rehoboamu ya mwanzo mpaka ya mwisho na rekodi ya ukoo yameandikwa katika kitabu cha Kumbukumbu za nabii Shemaya, na Kumbukumbu za Ido Mwonaji. Wakati huu wote, kulikuwa na vita vya mfululizo kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. 16Hatimaye Rehoboamu alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi, na Abiya mwanawe, akatawala mahali pake.




2Mambo ya Nyakati12;1-16

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: