Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 20 July 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 23...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe ee Mungu wetu....!!




Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni. Hii ndiyo njia ya kujua kama mtu anaongozwa na Roho wa Mungu: Kila anayekiri kwamba Kristo alikuja, akawa binadamu, mtu huyo anaye Roho wa Mungu. Lakini mtu yeyote asiyemkiri Kristo hivyo, hana huyo Roho atokaye kwa Mungu. Mtu huyo ana roho ambaye ni wa mpinzani wa Kristo; nanyi mlikwisha sikia kwamba anakuja, na sasa tayari amekwisha wasili ulimwenguni! Lakini nyinyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu. Wao husema mambo ya ulimwengu, nao ulimwengu huwasikiliza kwani wao ni wa ulimwengu. Lakini sisi ni wake Mungu. Mtu anayemjua Mungu hutusikiliza, mtu asiye wa Mungu hatusikilizi. Basi, kwa njia hiyo tunaweza kutambua tofauti kati ya Roho wa ukweli na roho wa uongo.


Tazama Jana imepita ee Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingineJehovah...
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha

na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazaretiyeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....





Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu. Mtu asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo. Na Mungu alionesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uhai kwa njia yake. Hivi ndivyo upendo ulivyo: Si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu. Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana. Hakuna mtu aliyekwisha mwona Mungu kamwe; lakini kama tukipendana, Mungu anaishi katika muungano nasi, na upendo wake unakamilika ndani yetu.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....




Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Tukawe barua njema  ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...





Tunajua kwamba tunaishi katika umoja na Mungu, naye Mungu anaishi katika umoja nasi, kwani yeye ametupa Roho wake. Sisi tumeona na kuwaambia wengine kwamba Baba alimtuma Mwanae awe Mwokozi wa ulimwengu. Kila mtu anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anaishi katika muungano na mtu huyo, naye anaishi katika muungano na Mungu. Basi, sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi. Mungu ni upendo, na kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye. Upendo umekamilika ndani yetu kusudi tuweze kuwa na ujasiri siku ile ya hukumu; kwani maisha yetu hapa duniani ni kama yale ya Kristo. Palipo na upendo hapana woga; naam, upendo kamili hufukuza woga wote. Basi, mtu mwenye woga hajakamilika bado katika upendo, kwani woga huhusikana na adhabu. Sisi tuna upendo kwa sababu Mungu alitupenda kwanza. Mtu akisema kwamba anampenda Mungu, hali anamchukia ndugu yake, huyo ni mwongo. Maana mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hamwoni. Basi, hii ndiyo amri aliyotupa Kristo: Anayempenda Mungu anapaswa pia kumpenda ndugu yake.




Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabuwote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



Athalia apinduliwa

(2Fal 11:4-16)

1Baadaye, mnamo mwaka wa saba, kuhani Yehoyada alijipa moyo akafanya mapatano na makapteni: Azaria mwana wa Yehoramu, Ishmaeli mwana wa Yehohanani, Azaria mwana wa Obedi, Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri. 2Wakazunguka katika miji yote ya Yuda wakiwakusanya Walawi na viongozi wa makabila ya Israeli, wakaenda mpaka Yerusalemu.
3Mkutano wote ukafanya agano na mfalme katika nyumba ya Mungu. Yehoyada akawaambia, “Mwangalie huyu mwana wa mfalme! Mwacheni atawale kulingana na ahadi aliyoitoa Mwenyezi-Mungu kuhusu uzao wa Daudi. 4Hivi ndivyo mtakavyofanya: Theluthi moja yenu nyinyi makuhani na Walawi mtakaoshika zamu siku ya Sabato, mtayalinda malango, 5theluthi nyingine italinda ikulu na theluthi iliyobakia mtalinda Lango la Msingi. Watu wote watakuwa katika nyua za nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 6Asikubaliwe mtu mwingine yeyote kuingia nyumba ya Mwenyezi-Mungu isipokuwa makuhani tu pekee na wale Walawi watakaokuwa wanahudumu. Hao wanaweza kuingia kwa sababu wao ni watakatifu, lakini wale watu wengine wote, watatii amri ya Mwenyezi-Mungu. 7Walawi watamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi; na mtu yeyote atakayejaribu kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, atauawa. Mkae na mfalme popote aendapo.”
8Walawi na watu wa Yuda walitii amri zote alizotoa kuhani Yehoyada. Kila ofisa akawachukua watu wake wote, wale waliokuwa wamemaliza zamu na wale waliokuwa wanaingia kushika zamu siku ya Sabato; kwa sababu Yehoyada hakuwaruhusu waondoke. 9Kisha kuhani Yehoyada akawapa makapteni mikuki na ngao kubwa na ndogo zilizokuwa mali ya mfalme Daudi, na ambazo zilikuwa zimewekwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
10Kisha, akawapanga watu wote kuanzia upande wa kusini mpaka upande wa kaskazini wa nyumba na kuzunguka madhabahu na nyumba, kila mmoja silaha yake mkononi, ili kumlinda mfalme. 11Halafu wakamtoa nje mwana wa mfalme, wakamvika taji kichwani, na kumpa ule ushuhuda; wakamtawaza nao Yehoyada na wanawe wakampaka mafuta awe mfalme, kisha watu wakashangilia wakisema, “Aishi mfalme!”
12Naye Malkia Athalia aliposikia sauti za watu wakikimbia na kumshangilia mfalme aliwaendea hao watu waliokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 13Alipochungulia akamwona mfalme mpya amesimama karibu na nguzo kwenye lango, huku makapteni na wapiga tarumbeta wakiwa kando ya mfalme na wakazi wote wakishangilia na kupiga tarumbeta; nao waimbaji wakiwa na ala zao za muziki wakiongoza watu katika sherehe; ndipo aliporarua nguo zake na kusema kwa sauti kubwa “Uhaini! Uhaini!”
14Kisha kuhani Yehoyada aliwatoa nje makapteni wa jeshi akisema mtoeni nje katikati ya askari; yeyote atakayemfuata na auawe kwa upanga. Kwa sababu alisema “Msimuulie katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”
15Basi, wakamkamata, na akaingia katika njia ya Lango la Farasi la ikulu, wakamuulia huko.

Matengenezo ya Yehoyada

(2Fal 11:17-20)

16Yehoyada akafanya agano kati yake mwenyewe, watu wote, na mfalme kwamba watakuwa watu wa Mwenyezi-Mungu. 17Halafu watu wote wakaenda kwenye nyumba ya Baali, wakaibomoa na kuzivunja madhabahu pamoja na sanamu zake. Kisha wakamuua Matani, kuhani wa Baali, mbele ya madhabahu. 18Kuhani Yehoyada akaweka walinzi kulinda nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hao walinzi walisimamiwa na makuhani na Walawi ambao Daudi aliwaweka katika huduma ya kutunza nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kutoa sadaka za kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, wakishangilia na kuimba kwa kufuata amri ya Daudi. 19Aliweka mabawabu malangoni mwa nyumba ya Mwenyezi-Mungu ili asije akaingia mtu yeyote aliye najisi kwa namna moja au nyingine.
20Aliwachukua makapteni wa jeshi, waheshimiwa, watawala wa watu, na wakazi wote; nao wakamsindikiza mfalme kutoka nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakapitia katika lango la juu mpaka ikulu. Kisha wakamkalisha mfalme kwenye kiti cha enzi. 21Kwa hiyo wakazi wote walishangilia; na mji wote ulikuwa mtulivu baada ya Athalia kuuawa kwa upanga.




2Mambo ya Nyakati23;1-21

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: