Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 10 July 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 15...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu,Neema yako yatutosha
Baba wa Mbinguni...!!



Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia wakati Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, pamoja na jeshi lake lote na falme zote za dunia zilizokuwa chini yake, kadhalika na watu wote walipokuwa wakiushambulia mji wa Yerusalemu na miji mingine yote ya kandokando yake: “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli asema hivi: Nenda ukaongee na Sedekia, mfalme wa Yuda. Mwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nimeutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteketeza kwa moto. Nawe hutatoroka mikononi mwake, bali kwa hakika utatekwa na kupelekwa kwake; utaonana na mfalme wa Babuloni macho kwa macho, na kuongea naye ana kwa ana; kisha, utakwenda Babuloni. Lakini, ewe Sedekia, mfalme wa Yuda, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu yako: Wewe hutauawa kwa upanga vitani. Utakufa kwa amani. Na, kama vile watu walivyochoma ubani walipowazika wazee wako waliokuwa wafalme, ndivyo watakavyokuchomea ubani na kuomboleza wakisema, ‘Maskini! Mfalme wetu amefariki!’ Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Kisha, nabii Yeremia akamweleza Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno hayo yote huko Yerusalemu, wakati jeshi la mfalme wa Babuloni lilipokuwa linaushambulia mji wa Yerusalemu na pia miji ya Lakishi na Azeka, ambayo ilikuwa miji pekee iliyosalia yenye ngome.



Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...



Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu baada ya mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote wa Yerusalemu kuwaachia huru watumwa wao wa Kiebrania wa kiume na wa kike, ili mtu yeyote asimfanye Myahudi mwenzake mtumwa. Viongozi wote na watu wote waliofanya agano hilo walikubaliana wote wawaachie huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na mtu yeyote asiwafanye tena kuwa watumwa. Walikubaliana, wakawaacha huru. Lakini baadaye walibadili nia zao, wakawashika tena watumwa hao wa kiume na wa kike ambao walikuwa wamewaacha huru, wakawafanya watumwa.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua  njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Hapo neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia: “Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nilifanya agano na wazee wenu nilipowatoa nchini Misri ambako walikuwa watumwa, nikawaambia: ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu atamwacha huru ndugu yake Myahudi aliyeuzwa akawa mtumwa kwa muda wa miaka sita. Mnapaswa kuwaacha huru, wasiwatumikie tena.’ Lakini wazee wenu hawakunisikiliza wala kunitegea sikio. Hivi karibuni nyinyi mlitubu, mkafanya mambo yaliyo sawa mbele yangu, mkawaacha huru Waisraeli wenzenu na kufanya agano mbele yangu katika nyumba yangu. Lakini baadaye mligeuka, mkalitia unajisi jina langu, wakati mlipowachukua tena watumwa walewale wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaachia kama walivyotaka, mkawalazimisha kuwa watumwa tena. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nyinyi hamkunitii kuhusu kuwapatia uhuru ndugu zenu Waisraeli. Basi, nami pia nitawapatieni uhuru; uhuru wa kuuawa kwa upanga vitani, kuuawa kwa maradhi na kwa njaa. Nitawafanya muwe kioja kwa falme zote duniani. Watu waliovunja agano langu na kukataa kufuata masharti ya agano walilofanya mbele yangu, nitawafanya kama yule ndama waliyemkata sehemu mbili na kupita katikati yake. Watu hao ndio hao maofisa wa Yuda, maofisa wa mji wa Yerusalemu, matowashi, makuhani, pamoja na wananchi wote waliopita katikati ya sehemu mbili za yule ndama. Watatiwa mikononi mwa maadui zao, na mikononi mwa watu wanaotaka kuwaua. Maiti zao zitaliwa na ndege wa angani na wanyama wa porini. Naye Sedekia, mfalme wa Yuda, pamoja na viongozi wake, nitawatia mikononi mwa maadui zao, na mikononi mwa watu wanaotaka kuwaua; yaani mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babuloni ambalo limeondoka na kuacha kuwashambulia. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema: Nitawaamuru nao wataurudia mji huu. Wataushambulia, watauteka na kuuteketeza kwa moto. Nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa bila wakazi.”

 Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.


Asa afanya matengenezo

1Roho ya Mungu ilimjia Azaria mwana wa Odedi, 2naye akatoka kwenda kumlaki mfalme Asa, akamwambia, “Nisikilize, ee mfalme Asa na watu wote wa Yuda na Benyamini! Mwenyezi-Mungu yu pamoja nanyi, ikiwa mtakuwa pamoja naye. Mkimtafuta, mtampata, lakini mkimwacha naye atawaacha. 3Kwa muda mrefu sasa, Waisraeli wameishi bila Mungu wa kweli, wala makuhani wa kuwafundisha, na bila sheria. 4Lakini walipopatwa na shida, walimgeukia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, wakamtafuta, wakampata. 5Zamani hizo, hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka kwa usalama kwa sababu hapakuwa na amani; ghasia nyingi mno ziliwasumbua wananchi wa kila nchi. 6Kulijaa mafarakano mengi, taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ulipigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu aliwafadhaisha kwa taabu za kila aina. 7Lakini nyinyi jipeni moyo, wala msilegee kwa maana mtapata tuzo kwa kazi mfanyayo.”
8Asa alipoyasikia maneno haya, yaani unabii wa Azaria mwana wa Odedi, alipata moyo. Akaziondoa sanamu zote za kuchukiza katika nchi yote ya Yuda na Benyamini, na kutoka katika miji yote aliyoiteka katika nchi ya milima ya Efraimu. Pia, akaitengeneza upya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa katika ukumbi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
9Asa aliwaita watu wote wa Yuda na Benyamini, na wengine wote waliokuwa wakikaa nchini mwake kutoka Efraimu, Manase na Simeoni. Hawa walikuja kwake walipoona kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye. 10Wote walikusanyika Yerusalemu katika mwezi wa tatu wa mwaka wa kumi na tano wa utawala wake Asa. 11Siku hiyo, walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za ng'ombe 700 na kondoo 7,000, kutoka katika zile nyara walizoteka. 12Hapo wakafanya agano, ya kuwa watamtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, kwa moyo wote na kwa roho yao yote; 13na kwamba yeyote asiyemtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, awe kijana au mzee, mwanamume au mwanamke, sharti auawe. 14Walimwapia Mwenyezi-Mungu kwa sauti kuu, wakapaza sauti zaidi, wakapiga tarumbeta na baragumu. 15Watu wote wa Yuda walikuwa na furaha tele kwa kuwa walikuwa wameapa kwa moyo wote. Walikuwa wamemtafuta kwa dhati, wakampata. Naye Mwenyezi-Mungu akawapa amani pande zote.
16Mfalme Asa alimwondoa hata Maaka, mama yake, katika cheo chake cha mama malkia, kwa sababu alitengeneza sanamu ya kuchukiza ya Ashera, mungu wa kike. Asa alikatilia mbali sanamu hiyo, akaipondaponda na kuiteketeza katika bonde la kijito Kidroni. 17Lakini hata hivyo mahali pa kutambikia miungu mingine katika Israeli hapakuharibiwa; lakini yeye alikuwa na moyo mwaminifu maisha yake yote. 18Alivirudisha katika nyumba ya Mungu vifaa vyote vilivyowekwa wakfu na baba yake pamoja na vile alivyoviweka wakfu yeye mwenyewe: Fedha na dhahabu na vyombo vinginevyo. 19Hapakuwa na vita tena nchini mpaka mwaka wa thelathini na tano wa utawala wake Asa.





2Mambo ya Nyakati15;1-19

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: