Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 5 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Marko 9...

 



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!



Maana, nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya laana, nchi inaomboleza, na malisho ya nyanda zake yamekauka. Mienendo ya watu ni miovu, nguvu zao zinatumika isivyo halali.

Yeremia 23:10

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Mwenyezi-Mungu asema: “Manabii na makuhani, wote hawamchi Mungu, uovu wao nimeuona hata nyumbani mwangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

Yeremia 23:11

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Kwa hiyo njia zao zitakuwa vichochoro vya utelezi gizani ambamo watasukumwa na kuanguka; maana, nitawaletea maafa, ufikapo mwaka wa kuwaadhibu, Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

Yeremia 23:12

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


1Yesu akaendelea kuwaambia, “Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa enzi.”
Yesu anageuka sura
(Mat 17:1-13; Luka 9:28-36)
2Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, 3mavazi yake yakangaa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe. 4Elia na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu. 5Petro akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri sisi kuwapo hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” 6Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema. 7Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni.” 8Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao.
9Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu. 10Basi, wakashika agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana wao kwa wao maana ya kufufuka kutoka kwa wafu. 11Wakamwuliza Yesu, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?” 12Naye akawajibu, “Naam, Elia anakuja kwanza kutayarisha yote. Hata hivyo, kwa nini basi imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Mwana wa Mtu atapatwa na mateso mengi na kudharauliwa? 13Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyotaka kama ilivyoandikwa juu yake.”
Yesu anamponya mtoto mwenye pepo
(Mat 17:14-21; Luka 9:37-43a)
14Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliona umati mkubwa wa watu hapo. Na baadhi ya waalimu wa sheria walikuwa wanajadiliana nao. 15Mara tu ule umati wa watu ulipomwona, wote walishangaa sana, wakamkimbilia wamsalimu. 16Yesu akawauliza, “Mnajadiliana nini nao?” 17Hapo mtu mmoja katika ule umati wa watu akamjibu, “Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo aliyemfanya kuwa bubu. 18Kila mara anapomvamia, humwangusha chini na kumfanya atokwe na povu kinywani, akisaga meno na kuwa mkavu mwili wote. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo lakini hawakuweza.”
19Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu.” 20Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto, 21“Amepatwa na mambo hayo tangu lini?” Naye akamjibu, “Tangu utoto wake. 22Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!” 23Yesu akamwambia, “Ati ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani.” 24Hapo, huyo baba akalia kwa sauti, “Naamini! Lakini imani yangu haitoshi, nisaidie.”
25Yesu alipouona umati wa watu unaongezeka upesi mbele yake, alimkemea yule pepo mchafu “Pepo unayemfanya huyu mtoto kuwa bubu na kiziwi, nakuamuru, mtoke mtoto huyu wala usimwingie tena!” 26Hapo huyo pepo alipaza sauti, akamwangusha huyo mtoto chini, kisha akamtoka. Mtoto alionekana kama maiti, hata wengine walisema, “Amekufa!” 27Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.
28Basi, Yesu alipoingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?” 29Naye akawaambia, “Pepo wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala.”
Yesu anasema tena juu ya kifo chake
(Mat 17:22-23; Luka 9:43b-45)
30Yesu na wanafunzi wake waliondoka hapo, wakaendelea na safari kupitia wilaya ya Galilaya. Yesu hakupenda watu wajue alipokuwa, 31kwa sababu alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Aliwaambia, “Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu ambao watamuua; lakini siku ya tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32Wanafunzi hawakufahamu jambo hilo. Wakaogopa kumwuliza.
Ni nani aliye mkubwa?
(Mat 18:1-5; Luka 9:46-48)
33Basi, walifika Kafarnaumu. Na alipokuwa nyumbani, aliwauliza, “Mlikuwa mnajadiliana nini njiani?” 34Lakini wao wakanyamaza, maana njiani walikuwa wamebishana ni nani aliyekuwa mkubwa kati yao.
35Yesu akaketi chini, akawaita wale kumi na wawili, akawaambia, “Mtu akitaka kuwa wa kwanza lazima awe wa mwisho na mtumishi wa wote.” 36Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kati yao, akamkumbatia, halafu akawaambia, 37“Anayempokea mtoto kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, hanipokei mimi tu, bali anampokea yule aliyenituma.”
Asiyetupinga yuko upande wetu
(Luka 9:49-50)
38Yohane akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako, nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.” 39Lakini Yesu akasema, “Msimkataze, maana hakuna mtu anayefanya mwujiza kwa jina langu, na papo hapo akaweza kusema mabaya juu yangu. 40Maana, asiyepingana nasi, yuko upande wetu. 41Mtu yeyote atakayewapeni kikombe cha maji ya kunywa, kwa sababu nyinyi ni watu wake Kristo, hakika hatakosa kupata tuzo lake.
Vikwazo
(Mat 18:6-9; Luka 17:1-2)
42“Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali kwa mtu huyo kufungiwa shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutupwa baharini. 43Mkono wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uhai bila mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda katika moto wa Jehanamu. [ 44Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.] 45Na mguu wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uhai bila mguu mmoja, kuliko kuwa na miguu yote miwili na kutupwa katika moto wa Jehanamu. [ 46Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.] 47Na jicho lako likikukosesha, lingoe! Afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja tu, kuliko kuwa na macho yako yote mawili na kutupwa katika moto wa Jehanamu. 48Humo wadudu wake hawafi, na huo moto hauzimiki.
49“Maana kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto. 50Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini? Muwe na chumvi ndani yenu na kudumisha amani kati yenu.”

Marko9;1-49

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: