Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 6 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Marko 10...Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..“Miongoni mwa manabii wa Samaria, nimeona jambo la kuchukiza sana: Walitabiri kwa jina la Baali wakawapotosha watu wangu Waisraeli. Lakini miongoni mwa manabii wa Yerusalemu, nimeona kinyaa cha kutisha zaidi: Wanafanya uzinzi na kusema uongo; wanawaunga mkono wanaotenda maovu hata pasiwe na mtu anayeachana na uovu. Kwangu wote wamekuwa kama watu wa Sodoma; wakazi wake wamekuwa wabaya kama watu wa Gomora.

Yeremia 23:13-14

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


“Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi juu ya manabii wa Yerusalemu: Nitawalisha uchungu, na kuwapa maji yenye sumu wanywe. Maana, kutoka kwa manabii wa Yerusalemu kutomcha Mungu kumeenea kila mahali nchini.”

Yeremia 23:15

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza weweJehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Msisikilize maneno ya manabii wanaowatabiria; wanawapeni matumaini ya uongo. Wanayowaambia ni maono yao wenyewe, wala hayakutoka kwangu mimi Mwenyezi-Mungu. Wao hawakomi kuwaambia wale wanaodharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu: ‘Mambo yatawaendea vema.’ Na kumwambia kila mtu afuataye kwa ukaidi fikira zake; ‘Hakuna baya lolote litakalokupata!’”

Yeremia 23:16-17

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

 Kuhusu talaka

(Mat 19:1-12; Luka 16:18)
1Yesu alitoka hapo akaenda mkoani Yudea, hata ngambo ya mto Yordani. Umati wa watu ukamwendea tena, naye akawafundisha tena kama ilivyokuwa desturi yake.
2Basi, Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, “Je, ni halali mume kumpa mkewe talaka?” 3Yesu akawajibu, “Mose aliwapa maagizo gani?” 4Nao wakasema, “Mose aliagiza mume
 kumpatia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”
5Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. 6Lakini tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke. 7Hivyo mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, 8nao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. 9Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe.”
10Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo. 11Naye akawaambia, “Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe. 12Na mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini.”
Yesu anawabariki watoto wadogo
(Mat 19:13-15; Luka 18:15-17)
13Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea. 14Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa. 15Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia humo.” 16Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki.
Mtu aliyekuwa tajiri
(Mat 19:16-36; Luka 18:18-30)
17Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanyeje niupate uhai wa milele?” 18Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. 19Unazijua amri: ‘Usizini, Usiue, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.’” 20Naye akamjibu, “Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.”
21Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja: Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha uje unifuate.” 22Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi.
23Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu!” 24Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, “Watoto wangu, ni vigumu sana kuingia katika ufalme wa Mungu! 25Ni rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” 26Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, “Ni nani basi, atakayeweza kuokoka?” 27Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana.”
28Petro akamwambia, “Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata!” 29Yesu akasema, “Kweli nawaambieni, kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au mama, au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, 30atapokea mara mia zaidi wakati huu wa sasa: Nyumba, ndugu, dada, mama, watoto na mashamba pamoja na mateso; na katika wakati ujao atapokea uhai wa milele. 31Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.”
Yesu anasema mara ya tatu kuhusu kifo na ufufuo wake
(Mat 20:17-19; Luka 18:31-34)
32Basi, walikuwa njiani kwenda juu Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata: 33“Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa. 34Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua. Lakini baada ya siku tatu atafufuka.”
Ombi la Yakobo na Yohane
(Mat 20:20-28)
35Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.” 36Yesu akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” 37Wakamjibu, “Uturuhusu kuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.” 38Yesu akawaambia, “Hamjui mnaomba nini! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?” 39Wakamjibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa. 40Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa.”
41Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane. 42Hivyo, Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. 43Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkubwa kati yenu, sharti awe mtumishi wenu. 44Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote. 45Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”
Yesu anamponya kipofu Bartimayo
(Mat 20:29-34; Luka 18:35-43)
46Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu, mwana wa Timayo aitwaye Bartimayo, alikuwa ameketi kando ya barabara, anaomba maskini. 47Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaza sauti, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!” 48Watu wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaza sauti, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
49Yesu alisimama, akasema, “Mwiteni.” Basi, wakamwita huyo kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Simama, anakuita.” 50Naye akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu.
51Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Huyo kipofu akamwambia, “Mwalimu, naomba nipate kuona.”
52Yesu akamwambia, “Nenda, imani yako imekuponya.” Mara huyo kipofu akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani.

Marko10;1-52

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: