Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 20 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 4...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ukitaka kurudi ee Israeli, nirudie mimi. Ukiviondoa vitu vya kuchukiza mbele yangu, usipotangatanga huko na huko, ukiapa kwa ukweli, unyofu na uadilifu, kwa kusema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo’, ndipo mataifa yatakapopata baraka kwangu, na kutukuka kwa sababu yangu.”

Yeremia 4:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Mwenyezi-Mungu awaambia hivi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu: “Limeni mashamba yenu mapya; msipande mbegu zenu penye miiba. Enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, jitakaseni kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu, wekeni mioyo yenu wazi mbele yangu. La sivyo, ghadhabu yangu itachomoza kama moto, iwake hata pasiwe na mtu wa kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.

Yeremia 4:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


“Tangazeni huko Yuda, pazeni sauti huko Yerusalemu! Pigeni tarumbeta kila mahali nchini! Pazeni sauti na kusema: Kusanyikeni pamoja! Kimbilieni miji yenye ngome! Twekeni bendera ya vita kuelekea Siyoni, kimbilieni usalama wenu, msisitesite! Mwenyezi-Mungu analeta maafa na maangamizi makubwa kutoka kaskazini.

Yeremia 4:5-6

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.





 Kujaribiwa kwa Yesu

(Mat 4:1-11; Marko 1:12-13)
1Yesu alitoka mtoni Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani. 2Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa. 3Ndipo Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.” 4Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’”
5Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia, 6“Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza. 7Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu.” 8Yesu akamjibu, “Imeandikwa:
‘Utamwabudu Bwana Mungu wako,
na kumtumikia yeye peke yake.’”
9Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa hekalu, akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini 10Taz Zab 91:11 kwa maana imeandikwa:
‘Atawaamuru malaika wake wakulinde,’
11 Taz Zab 91:12 na tena,
‘Watakuchukua mikononi mwao,
usije ukajikwaa mguu kwenye jiwe.’”
12Lakini Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’” 13Ibilisi alipokwisha mjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda.
Yesu anaanza kazi yake Galilaya
(Mat 4:12-17; Marko 1:14-15)
14Hapo Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani. 15Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.
Yesu anakataliwa huko Nazareti
(Mat 13:53-58; Marko 6:1-6)
16Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti. 17Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:
18“Roho wa Bwana yu juu yangu,
kwani ameniweka wakfu
niwaletee maskini Habari Njema.
Amenituma niwatangazie mateka uhuru wao,
na vipofu watapata kuona tena;
amenituma niwakomboe wanaoonewa,
19na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.”
20Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho. 21Naye akaanza kuwaambia, “Andiko hili mlilosikia limetimia leo.” 22Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”
23Naye akawaambia, “Bila shaka mtaniambia msemo huu: ‘Mganga jiponye mwenyewe,’ na pia mtasema: ‘Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye pia hapa kijijini mwako.’” 24Akaendelea kusema, “Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi kijijini mwake. 25Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Elia. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote. 26Hata hivyo, Elia hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarefathi katika Sidoni. 27Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani mwenyeji wa Siria.” 28Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana. 29Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini. 30Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.
Mtu mwenye pepo mchafu
(Marko 1:21-28)
31Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu wilayani Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato. 32Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha. 33Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio: 34“Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!” 35Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo. 36Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!” 37Habari za Yesu zikaenea mahali pote katika eneo lile.
Yesu anawaponya watu wengi
(Mat 8:14-17; Marko 1:29-34)
38Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye. 39Yesu akaja akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Yule mama akainuka mara, akawatumikia.
40Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote. 41Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walijua kwamba yeye ndiye Kristo.
Yesu anahubiri huko Yudea
(Marko 1:35-39)
42Kesho yake asubuhi, Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta. Hao watu walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao. 43Lakini yeye akawaambia, “Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo.” 44Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.

Luka4;1-44

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: