Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 1 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Marko 7...

 



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..



“Ole wao wachungaji wanaowaangamiza na kuwatawanya kondoo wa malisho yangu!” Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli nasema hivi kuhusu wachungaji wanaowachunga watu wangu: Nyinyi mmewatawanya kondoo wangu na kuwafukuza, wala hamkuwatunza. Basi, nami pia nitawaadhibu kwa ajili ya matendo yenu maovu.

Yeremia 23:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Kisha, nitawakusanya kondoo wangu waliobaki kutoka nchi zote nilikowatawanya, na kuwarudisha malishoni mwao. Nao watazaa na kuongezeka. Nitawapa wachungaji watakaowatunza vema, nao hawatakuwa na woga tena wala kufadhaika, na hakuna hata mmoja wao atakayepotea, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

Yeremia 23:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



“Tazama, siku zaja nitakapomchipushia Daudi chipukizi adili. Huyo atatawala kama mfalme, na atatenda kwa busara, haki na uadilifu katika nchi. Katika siku za utawala wake, Yuda ataokolewa na Israeli ataishi kwa usalama. Naye ataitwa, ‘Mwenyezi-Mungu ni uadilifu wetu.’

Yeremia 23:5-6

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Mapokeo ya mababu

(Mat 15:1-9)
1Baadhi ya Mafarisayo na waalimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu. 2Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa. 3Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: Hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo. 4Tena, hawali kitu chochote kutoka sokoni, mpaka wamekiosha kwanza.7:4 mpaka wamekiosha kwanza: Au Mpaka wametawadha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizozipokea toka zamani kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba.
5Basi, Mafarisayo na waalimu wa sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati mapokeo tuliyoyapokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?” 6Yesu akawajibu, “Wanafiki nyinyi! Nabii Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu alipoandika:
‘Mungu asema: Watu hawa, huniheshimu kwa maneno tu,
lakini mioyoni mwao, wako mbali nami.
7Kuniabudu kwao hakufai,
maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’
8Nyinyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu.”
9Yesu akaendelea kusema, “Nyinyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu! 10Maana Mose aliamuru: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima afe’. 11Lakini nyinyi mwafundisha, ‘Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani zawadi kwa Mungu), 12basi, halazimiki tena kumsaidia baba yake au mama yake’. 13Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo.”
Mambo yanayomtia mtu unajisi
(Mat 15:10-20)
14Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, mkaelewe. 15Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu kutoka nje kinachoweza kumtia mtu unajisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu unajisi.” 16Mwenye masikio na asikie!
17Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano. 18Naye akawaambia, “Je, hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu kutoka nje, hakiwezi kumtia unajisi, 19kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alihalalisha vyakula vyote.)
20Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia unajisi. 21Maana kutoka ndani, moyoni mwa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, 22uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu. 23Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu unajisi.”
Imani ya mama mmoja
(Mat 15:21-28)
24Yesu aliondoka hapo, akaenda wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha. 25Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake. 26Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu. 27Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” 28Lakini huyo mama akasema, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.” 29Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!” 30Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.
Yesu anamponya bubu kiziwi
31Kisha Yesu aliondoka wilaya ya Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli. 32Basi, wakamletea bubu kiziwi, wakamwomba amwekee mikono. 33Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi. 34Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, “Efatha,” maana yake “Funguka.” 35Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa. 36Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo. 37Watu walishangaa sana, wakasema, “Amefanya yote vyema: Amewajalia viziwi kusikia, na mabubu kusema!”


Marko7;1-37

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: