Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 7 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Marko 11...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Lakini, ni yupi kati ya manabii hao aliyepata kuhudhuria baraza la Mwenyezi-Mungu, hata akasikia na kuelewa neno lake? Au ni nani aliyejali neno lake, hata akapata kulitangaza?

Yeremia 23:18

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Tazama, dhoruba kutoka kwa Mwenyezi-Mungu! Ghadhabu imezuka; kimbunga cha tufani kitamlipukia mtu mwovu kichwani.

Yeremia 23:19

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Hasira ya Mwenyezi-Mungu haitarudi nyuma, mpaka atakapotekeleza na kukamilisha matakwa ya moyo wake. Siku zijazo mtayaelewa vema mambo hayo.

Yeremia 23:20

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe

(Mat 21:1-11; Luka 19:28-40; Yoh 12:12-19)
1Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake, 2akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwanapunda amefungwa, ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete. 3Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnafanya hivyo?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara.’”
4Basi, wakaenda, wakamkuta mwanapunda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua, 5baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwanapunda?” 6Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao. 7Wakampelekea Yesu huyo mwanapunda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwanapunda na Yesu akaketi juu yake. 8Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani. 9Taz Zab 118:25-26 Watu wote waliotangulia na wale waliofuata, wakapaza sauti zao wakisema, “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! 10Ubarikiwe ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Sifa kwa Mungu juu mbinguni!”
11Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
Yesu anaulaani mtini
(Mat 21:18-19)
12Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa. 13Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila tu majani matupu, kwa vile hayakuwa majira yake ya matunda. 14Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo.
Yesu anaingia hekaluni
(Mat 21:12-17; Luka 19:45-48; Yoh 2:13-22)
15Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha, na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 16Hakumruhusu mtu yeyote kupitia hekaluni akichukua kitu. 17Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi!”
18Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake. 19Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini.
Fundisho juu ya mtini ulionyauka
(Mat 21:20-22)
20Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi. 21Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!”
22Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu. 23Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo. 24Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa. 25Mnaposimama kusali, msameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe nyinyi makosa yenu.” [ 26Lakini msipowasamehe wengine, hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe nyinyi makosa yenu.]
Suala kuhusu mamlaka ya Yesu
(Mat 21:23-27; Luka 20:1-8)
27Basi, wakafika tena Yerusalemu. Yesu alipokuwa akitembea hekaluni, makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee walimwendea, 28wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?”
29Lakini Yesu akawaambia, “Nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, nami pia nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. 30Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka mbinguni ama kwa watu? Nijibuni.”
31Wakaanza kujadiliana, “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni’, atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’ 32Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu (Waliogopa umati wa watu maana wote waliamini kwamba Yohane alikuwa kweli nabii.) 33Basi, wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”

Marko11;1-33

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: