Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 16 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 2...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..



Hawa waliandikishwa kulingana na kazi zao kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kutoa huduma, kadiri ya utaratibu waliowekewa na Aroni babu yao, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 24:19

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Hawa ndio wazawa wengine wa Lawi: Mmoja wa wazawa wa Amramu alikuwa Shubaeli; wa Shubaeli alikuwa Yedeya. Mmoja wa wazawa wa Rehabia alikuwa Ishio kiongozi wa ukoo.

1 Mambo ya Nyakati 24:20-21

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Mmoja wa wazawa wa Ishio alikuwa Shelomithi na wa wazawa wa Shelomithi alikuwa Yahathi. Wana wa Hebroni walikuwa: Yeria wa kwanza, Amaria wa pili, Yahazieli wa tatu, Yakameamu wa nne.

1 Mambo ya Nyakati 24:22-23

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!



Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Kuzaliwa kwa Yesu

(Mat 1:18-25)
1Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote nchini kote wahesabiwe. 2Sensa hiyo ilikuwa mara ya kwanza, wakati Kurenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria. 3Basi, wote waliohusika walikwenda kuhesabiwa kila mtu katika mji wake.
4Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya, na kwa vile alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi, alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yudea, alikozaliwa mfalme Daudi. 5Alikwenda kuhesabiwa pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mjamzito. 6Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, 7akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.
Wachungaji na malaika
8Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. 9Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana. 10Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kubwa itakayowapata watu wote. 11Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. 12Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.”
13Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema:
14“Utukufu kwa Mungu juu mbinguni,
na amani duniani kwa watu anaowafadhili!”
15Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: “Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha.”
16Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini. 17Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake. 18Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji. 19Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake. 20Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.
Mtoto anapewa jina
21Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.
Yesu anawekwa mbele ya Bwana
22Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na sheria, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele za Bwana. 23Katika sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.” 24Pia walikwenda ili watoe sadaka: Hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika sheria ya Bwana.
25Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. 26Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. 27Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na sheria, 28Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu, akisema:
29“Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako,
umruhusu mtumishi wako aende kwa amani.
30Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu ulioleta,
31ambao umeutayarisha uonekane na watu wote:
32Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa,
na utukufu kwa watu wako Israeli.”
33Baba yake Yesu na mama yake walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. 34Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; 35na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako.”
36Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa. 37Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana. 38Saa hiyohiyo, alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na kueleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu.
Kurudi Nazareti
39Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, wilayani Galilaya. 40Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa naye.
Mtoto Yesu hekaluni
41Wazazi wake walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. 44Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. 45Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta.
46Siku ya tatu, walimkuta hekaluni kati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. 48Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutendea hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.” 49Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” 50Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia.
51Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. 52Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.

Luka2;1-52

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: