Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 22 October 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 6...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Tazama! Adui anakuja kama mawingu. Magari yake ya vita ni kama kimbunga, na farasi wake waenda kasi kuliko tai. Ole wetu! Tumeangamia! Yerusalemu, yasafishe maovu moyoni mwako, ili upate kuokolewa. Mpaka lini utaendelea kuwaza maovu?

Yeremia 4:13-14

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Sauti kutoka Dani inatoa taarifa; inatangaza maafa kutoka vilima vya Efraimu. Inayaonya mataifa, inaitangazia Yerusalemu: “Wavamizi waja kutoka nchi ya mbali, wanaitisha miji ya Yuda,

Yeremia 4:15-16

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



wanauzingira Yerusalemu kama walinda mashamba, kwa sababu watu wake wameniasi mimi Mwenyezi-Mungu. Yuda, mwenendo wako na matendo yako yamekuletea hayo. Hayo ndiyo maafa yaliyokupata, tena ni machungu; yamepenya mpaka ndani moyoni mwako.”

Yeremia 4:17-18

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Suala juu ya siku ya Sabato

(Mat 12:1-8; Marko 2:23-28)
1Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. 2Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” 3Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? 4Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” 5Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.”
Mtu mwenye mkono uliopooza
(Mat 12:9-14; Marko 3:1-6)
6Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza. 7Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. 8Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati. 9Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?” 10Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. 11Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.
Yesu anateua mitume kumi na wawili
(Mat 10:1-4; Marko 3:13-19)
12Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. 13Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume: 14Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, 15Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), 16Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.
Yesu anafundisha na kuwaponya watu
(Mat 4:23-25)
17Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. 18Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. 19Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.
Heri na ole
(Mat 5:1-12)
20Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema:
“Heri nyinyi mlio maskini,
maana ufalme wa Mungu ni wenu.
21Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa,
maana baadaye mtashiba.
Heri nyinyi mnaolia sasa,
maana baadaye mtacheka kwa furaha.
22“Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. 23Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo.
24Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri,
maana mmekwisha pata faraja yenu.
25Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa,
maana baadaye mtasikia njaa.
Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa,
maana baadaye mtaomboleza na kulia.
26Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu,
maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.
Kuwapenda maadui
(Mat 5:38-48; 7:12a)
27“Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. 28Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 29Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. 30Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. 31Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo.
32“Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. 33Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. 34Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. 35Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. 36Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.
Juu ya kuwahukumu wengine
(Mat 7:1-5)
37“Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. 38Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.”
39Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. 40Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. 41Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? 42Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako.
Mtu hujulikana kwa matunda yake
(Mat 7:16-20; 12:33-35)
43“Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. 44Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. 45Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake.
Wajenzi wa namna mbili
(Mat 7:24-27)
46“Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema? 47Nitawapeni mfano unaofaa kuonesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: 48Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. 49Lakini yeyote anayesikia maneno yangu asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!”

Luka6;1-49

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: