Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 22 January 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 38....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na sheria, Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu, akisema:
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


“Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, umruhusu mtumishi wako aende kwa amani. Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu ulioleta, ambao umeutayarisha uonekane na watu wote: Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Baba yake Yesu na mama yake walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako.”
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Yeremia ndani ya kisima
1Shefatia mwana wa Matani, Gedalia mwana wa Pashuri, mwana wa Malkia, walisikia maneno ambayo Yeremia aliwatangazia watu wote akisema, 2“Mwenyezi-Mungu asema hivi: Yeyote atakayebaki katika mji huu atakufa kwa vita, njaa na maradhi; lakini yule atakayeondoka na kujisalimisha kwa Wakaldayo, ataishi. Atakuwa ametekwa nyara na kuishi. 3Mwenyezi-Mungu asema kuwa hakika mji huu utatiwa mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babuloni na kutekwa.”
4Wakuu wakamwambia mfalme, “Yafaa mtu huyu auawe kwa maana anawavunja moyo askari ambao wameachwa katika mji huu na watu wote kwa jumla, kwa kusema maneno kama hayo. Yeye hawatakii watu hawa mema bali mabaya.”
5Mfalme Sedekia akasema, “Haya! Mtu huyu yumo mikononi mwenu; mimi siwezi kuwapinga.” 6Basi, wakamchukua Yeremia wakamtumbukiza katika kisima cha Malkia mwana wa mfalme ambacho kilikuwa katika ukumbi wa walinzi. Walimshusha Yeremia ndani kwa kamba. Ndani ya kisima hicho hakukuwa na maji bali tope, naye Yeremia akazama katika tope. 7Lakini Ebedmeleki, towashi Mwethiopia aliyekuwa akifanya kazi katika ikulu, alipata habari kwamba walikuwa wamemtumbukiza Yeremia kisimani. Wakati huo mfalme alikuwa anabarizi penye lango la Benyamini. 8Basi, Ebedmeleki akamwendea mfalme, akamwambia, 9“Bwana wangu mfalme, watu hawa wamefanya kitu kibaya. Wamemtumbukiza yule nabii Yeremia kisimani ambamo kwa kweli atakufa kwa njaa, kwa maana hamna chakula tena mjini.” 10Hapo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mwethiopia: “Chukua watu watatu kutoka hapa uende ukamtoe nabii Yeremia kisimani, kabla hajafa.” 11Basi, Ebedmeleki akawachukua watu hao na kwenda pamoja nao ikulu kwa mfalme, wakaingia katika ghala ya ikulu; Ebedmeleki akatwaa nguo zilizotumika na matambara makuukuu, akamteremshia Yeremia kisimani kwa kamba. 12Kisha Ebedmeleki, Mwethiopia, akamwambia Yeremia, “Weka hayo matambara kwapani mwako, kisha pitisha kamba hizo chini ya matambara hayo.” Yeremia akafanya hivyo. 13Kisha wakamvuta Yeremia kwa kamba, wakamtoa kisimani. Baada ya hayo, Yeremia akaendelea kukaa katika ukumbi wa walinzi.
Sedekia anaomba shauri kwa Yeremia
14Wakati fulani mfalme Sedekia alitaka kumwona nabii Yeremia. Basi, akaagiza Yeremia aletwe kwenye mlango wa tatu wa hekalu la Mwenyezi-Mungu. Huko, mfalme alimwambia Yeremia, “Nataka kukuuliza jambo fulani; usinifiche kitu chochote.” 15Yeremia akamjibu Sedekia, “Je, nikikuambia ukweli hutaniua? Na kama nikikushauri, hutanisikiliza.” 16Hapo, mfalme Sedekia alimwapia Yeremia kwa siri akisema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyetupa uhai, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa hawa wanaotaka kukuua.”
17Hapo Yeremia akamwambia Sedekia: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama ukijitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, utayaokoa maisha yako na mji hautateketezwa kwa moto; nawe pamoja na jamaa yako mtaendelea kuishi. 18Lakini usipojitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, basi, mji huu utatekwa na Wakaldayo nao watauteketeza kwa moto, nawe hutaweza kujiepusha mikononi mwao.” 19Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Nawaogopa Wayahudi waliokimbilia kwa Wakaldayo. Huenda nikakabidhiwa kwao, wakanitesa.”
20Yeremia akamjibu, “Hutakabidhiwa kwao. Wewe sasa tii anachosema Mwenyezi-Mungu, kama ninavyokuambia, na mambo yote yatakuendea vema, na maisha yako yatasalimika. 21Lakini kama ukikataa kujitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwao, haya ndiyo maono ambayo Mwenyezi-Mungu amenionesha. 22Katika maono hayo, niliona wanawake waliobaki katika ikulu ya mfalme wa Yuda wakipelekwa kwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, nao walikuwa wakisema hivi:
‘Marafiki zako uliowaamini wamekudanganya,
nao wamekushinda;
kwa kuwa miguu yako imezama matopeni,
wamekugeuka na kukuacha.’
23Wake zako wote na watoto wako watapelekwa kwa Wakaldayo, nawe mwenyewe hutanusurika. Utachukuliwa mateka na mfalme wa Babuloni na mji huu utateketezwa kwa moto.”
24Sedekia akamwambia Yeremia: “Mtu yeyote asijue habari hizi, nawe hutauawa. 25Kama viongozi wakisikia kuwa nimeongea nawe, kisha wakaja na kukuambia, ‘Hebu tuambie, ulizungumza nini na mfalme. Usitufiche chochote nasi hatutakuua’; 26wewe utawaambia hivi: ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme kwa unyenyekevu asinirudishe gerezani nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafia huko.’” 27Kisha, viongozi walimjia Yeremia wakamwuliza mambo hayo, naye akawajibu kama mfalme alivyomwelekeza. Ndipo walipoacha kuzungumza naye kwa sababu hakuna mtu aliyekuwa amesikia mazungumzo yake na mfalme. 28Yeremia alibaki katika ukumbi wa walinzi mpaka siku mji wa Yerusalemu ulipotekwa.



Yeremia38;1-28

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: