Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 6 January 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 26....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki/mwezi/mwaka
Mwingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie.
Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao.
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uhai ambao ni uhai wa kweli.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Yeremia mahakamani
1Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, katika nchi ya Yuda, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yeremia hivi: 2“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Simama katika ukumbi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, uwatangazie watu wa miji yote ya Yuda wanaofika kuabudu katika nyumba ya Mungu, mambo yote niliyokuamuru uwaambie, bila kuacha hata neno moja. 3Labda watasikiliza na kuacha njia zao mbaya. Wakifanya hivyo, huenda nikabadili nia yangu kuhusu maafa niliyonuia kuwaletea kwa sababu ya matendo yao maovu.
4“Utawaambia hivi: Mwenyezi-Mungu asema hivi: Msiponisikiliza na kufuata sheria zangu nilizowawekea, 5na msipoyajali wanayosema watumishi wangu manabii ambao nimekuwa nikiwatuma kwenu kila mara, ingawa hamkuwajali, 6basi, nitaiharibu nyumba hii kama nilivyoharibu ile ya Shilo, na nitaufanya mji huu kuwa laana kwa mataifa yote ya dunia.”
7Makuhani, manabii na watu wote walimsikia Yeremia akisema maneno haya katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 8Basi Yeremia alipomaliza kutangaza mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimwamuru ayatangaze kwa watu wote, makuhani, manabii na watu wote walimkamata na kusema, “Utakufa! 9Kwa nini umetabiri kwa jina la Mwenyezi-Mungu na kusema, nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa, bila wakazi?” Watu wote wakamzingira Yeremia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
10Basi, wakuu wa Yuda waliposikia mambo hayo, walipanda kutoka katika nyumba ya mfalme, wakaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaketi penye Lango Jipya. 11Hapo makuhani na manabii wakawaambia wakuu na watu wote: “Mtu huyu anastahili hukumu ya kifo kwa maana amehubiri dhidi ya mji huu, kama nyinyi wenyewe mlivyosikia kwa masikio yenu.”
12Ndipo Yeremia akawaambia wakuu na watu wote: “Mwenyezi-Mungu alinituma niwatabirie mambo yote mliyosikia nikiyasema dhidi ya hekalu hili na mji huu. 13Sasa basi, rekebisheni mienendo yenu na matendo yenu na kutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mkifanya hivyo, Mwenyezi-Mungu atabadili nia yake na kuacha kuwaletea maafa aliyotamka dhidi yenu. 14Lakini mimi, tazama nimo mikononi mwenu. Nitendeeni kama mnavyoona vema na haki. 15Ila jueni kwa hakika kwamba mkiniua, mtakuwa mmejiletea laana nyinyi wenyewe kwa kumwaga damu isiyo na hatia, na kuuletea laana mji huu na wakazi wake. Maana, ni kweli kwamba Mwenyezi-Mungu alinituma niwaambieni mambo hayo muyasikie.”
16Hapo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani na manabii: “Mtu huyu hastahili hukumu ya kifo, kwa kuwa amesema nasi kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.” 17Basi, baadhi ya wazee wa nchi wakasimama na kuwaambia watu waliokuwa wamekusanyika: 18“Wakati Hezekia alipokuwa mfalme wa Yuda, Mika wa Moreshethi, aliwatangazia watu wote kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi alisema hivi:
‘Mji wa Siyoni utalimwa kama shamba
mji wa Yerusalemu utakuwa magofu,
nao mlima wa hekalu utakuwa msitu.’
19Je, Hezekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa Yuda walimuua Mika? La! Badala yake Hezekia alimwogopa Mwenyezi-Mungu na kuomba fadhili zake. Naye Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake ya kuwaletea balaa. Lakini sisi tuko mbioni kujiletea wenyewe maafa.”
20(Kulikuwa na mtu mwingine pia aliyetabiri kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo alikuwa anaitwa Uria mwana wa Shemaya, kutoka mji wa Kiriath-yearimu. Yeye alitabiri dhidi ya mji huu na dhidi ya nchi hii kama alivyofanya Yeremia. 21Naye mfalme Yehoyakimu pamoja na mashujaa wake na wakuu wote waliposikia mambo aliyosema Uria, mfalme alitaka kumuua. Lakini Uria alipopata habari, alishikwa na hofu, akatoroka na kwenda Misri. 22Mfalme Yehoyakimu alimpeleka Elnathani mwana wa Akbori, pamoja na watu kadhaa huko Misri. 23Wao walimrudisha Uria kutoka Misri, wakampeleka kwa mfalme Yehoyakimu. Mfalme akamuua kwa upanga na maiti yake ikazikwa kwenye makaburi ya watu wa kawaida.)
24Lakini Yeremia alikuwa akilindwa na Ahikamu mwana wa Shefani, ili asitiwe mikononi mwa watu na kuuawa.

Yeremia26;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: