Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 7 January 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 27....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu



Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa. Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile wanachokiita watu wengine “Elimu.” Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo yake wamepoteza imani. Nawatakieni nyote neema!
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Yeremia anavaa nira
1Mwanzoni mwa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu. 2Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Yeremia, jitengenezee kamba na nira ujivike shingoni. 3Kisha, peleka ujumbe27:3 peleka ujumbe: Kiebrania: Vipeleke. kwa mfalme wa Edomu, mfalme wa Moabu, mfalme wa Amoni, mfalme wa Tiro na mfalme wa Sidoni, kupitia kwa wajumbe waliokuja Yerusalemu kumwona Sedekia mfalme wa Yuda. 4Waamuru wajumbe hao wawaambie wakuu wao kwamba mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: 5Mimi ndimi niliyeiumba dunia, watu na wanyama waliomo kwa uwezo wangu na kwa mkono wangu wenye nguvu, nami humpa mtu yeyote kama nionavyo mimi kuwa sawa. 6Sasa nimemkabidhi mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babuloni, nchi hizi zote; kadhalika nimempa wanyama wa porini wamtumikie. 7Mataifa yote yatamtumikia yeye, mwanawe na mjukuu wake, mpaka wakati nchi yake itakapoanguka. Kisha mataifa mengi na wafalme wengi watamfanya kuwa mtumwa wao.
8“Lakini kama taifa lolote au utawala wowote hautajiweka chini ya mamlaka ya Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, basi, nitaliadhibu taifa hilo kwa vita, njaa na maradhi mpaka niliangamize kabisa kwa mkono wake. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. 9Basi, nyinyi msiwasikilize manabii wenu, wapiga ramli wenu, watabiri wenu, waaguzi wenu au wachawi wenu, wanaowaambia: ‘Msimtii mfalme wa Babuloni.’ 10Hao wanawatabirieni uongo na hii itasababisha mhamishwe mbali na nchi yenu. Nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia. 11Lakini watu wa taifa lolote litakalomtii mfalme wa Babuloni na kumtumikia, nitawaacha wakae nchini mwao, wailime ardhi yao na kuishi humo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
12Mimi Yeremia nilikuwa nimemwambia Sedekia mfalme wa Yuda, mambo hayohayo. Nilimwambia: “Mtii mfalme wa Babuloni. Mtumikie yeye na watu wake, nawe utaishi. 13Ya nini wewe na watu wako kufa kwa vita, njaa na maradhi? Maana, hivyo ndivyo alivyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu yatakayolipata taifa lolote litakaloacha kumtumikia mfalme wa Babuloni. 14Usisikilize maneno ya manabii wanaokuambia: ‘Usimtumikie mfalme wa Babuloni’, kwa sababu wanakutabiria uongo. 15Mwenyezi-Mungu anasema: ‘Mimi sikuwatuma manabii hao, bali wanatabiri uongo kwa jina langu. Kwa hiyo nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia, pamoja na hao manabii wanaowatabirieni uongo.’”
16Kisha, niliwaambia makuhani na watu wote: Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Msiwasikilize manabii wenu wanaowatabiria wakisema: ‘Tazama, vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu vitarudishwa hivi karibuni kutoka Babuloni’, kwa maana wanawadanganyeni. 17Msiwasikilize. Mtumikieni mfalme wa Babuloni, nanyi mtaishi. Ya nini mji huu ufanywe kuwa magofu? 18Ikiwa wao ni manabii, na kama wana neno la Mwenyezi-Mungu, basi, na wamsihi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ili vyombo vilivyobaki katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika nyumba ya mfalme wa Yuda, na katika mji wa Yerusalemu, visichukuliwe na kupelekwa Babuloni. 19Kwa maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi juu ya nguzo, sinia za shaba, vinara na vyombo vingine vilivyoachwa katika mji huu 20ambavyo Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, hakuvichukua wakati alipowachukua Yekonia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda na waheshimiwa wote wa Yuda na Yerusalemu kutoka Yerusalemu na kuwapeleka uhamishoni.
21“Sikilizeni mambo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, ninasema juu ya vile vyombo vilivyoachwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, katika nyumba ya mfalme wa Yuda na katika mji wa Yerusalemu. 22Vyombo hivyo vitachukuliwa Babuloni na vitabaki huko mpaka siku nitakapovishughulikia. Hapo ndipo nitakapovirudisha na kuviweka tena mahali hapa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”


Yeremia27;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: