Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 13 January 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 31....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu. Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto.
Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.”
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

Waisraeli wanarudi makwao
1Mwenyezi-Mungu asema: “Wakati utakuja ambapo nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli nao watakuwa watu wangu.
2Mimi Mwenyezi-Mungu nasema:
Watu walionusurika kuuawa
niliwaneemesha jangwani.
Wakati Israeli alipotafuta kupumzika,
3mimi Mwenyezi-Mungu nilimtokea kwa mbali.
Nami nimekupenda kwa mapendo ya daima,
kwa hiyo nimeendelea kuwa mwaminifu kwako.
4Nitakujenga upya nawe utajengeka,
ewe Israeli uliye mzuri!
Utazichukua tena ngoma zako
ucheze kwa furaha na shangwe.
5Utapanda tena mizabibu
juu ya milima ya Samaria;
wakulima watapanda mbegu
na kuyafurahia mazao yake!
6Maana siku yaja ambapo mlinzi atapiga mbiu
katika vilima vya Efraimu:
‘Amkeni, twende juu mpaka Siyoni
kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’”
7Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Imbeni kwa furaha kwa ajili ya Yakobo,
pigeni vigelegele kwa ajili ya taifa kuu,
tangazeni, shangilieni na kusema:
‘Mwenyezi-Mungu na awaokoe watu wake,
amewaletea ukombozi waliobaki wa Israeli!’
8Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini,
nitawakusanya kutoka miisho ya dunia.
Wote watakuwapo hapo;
hata vipofu na vilema,
wanawake waja wazito na wanaojifungua;
umati mkubwa sana utarudi hapa.
9Watarudi wakiwa wanatoa machozi,
nitawarudisha nikiwafariji;
nitawapitisha kando ya vijito vya maji,
katika njia iliyonyoka ambamo hawatajikwaa;
maana mimi nimekuwa baba wa Israeli,
Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.
10Enyi mataifa, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu,
litangazeni katika nchi za mbali,
semeni: ‘Aliyemtawanya Israeli, atamkusanya,
atamtunza kama mchungaji atunzavyo kondoo wake.’
11Maana mimi Mwenyezi-Mungu nimemkomboa Yakobo,
nimemwokoa kutoka kwa wenye nguvu kuliko yeye.
12Watakuja na kuimba kwa sauti juu ya mlima Siyoni,
wataona fahari juu ya wema wangu mimi Mwenyezi-Mungu,
kwa nafaka, divai na mafuta niwapavyo,
kwa kondoo na ng'ombe kadhalika;
maisha yao yatakuwa kama bustani iliyotiliwa maji,
wala hawatadhoofika tena.
13Ndipo wasichana wao watafurahi na kucheza,
vijana na wazee watashangilia kwa furaha.
Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,
nitawafariji na kuwapa furaha badala ya huzuni.
14Nitawashibisha makuhani kwa vinono,
nitawaridhisha watu wangu kwa wema wangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Huruma ya Mungu kwa Israeli
15Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Sauti imesikika mjini Rama,
maombolezo na kilio cha uchungu.
Raheli anawalilia watoto wake,
wala hataki kufarijiwa kwa ajili yao,
maana wote hawako tena.
16Sasa, acha kulia,
futa machozi yako,
kwani utapata tuzo kwa kazi yako,
mimi Mwenyezi-Mungu nimesema;
watoto wenu watarudi kutoka nchi ya maadui zenu.
17Yapo matumaini kwa siku zenu zijazo,
mimi Mwenyezi-Mungu nimesema;
kwani watoto wenu watarejea nchini mwao.
18“Nimesikia Efraimu akilalamika:
‘Umenichapa ukanifunza nidhamu,
kwani nilikuwa kama ndama asiyezoea nira.
Unigeuze nami nitakugeukia,
kwani wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.
19Maana baada ya kukuasi, nilitubu,
na baada ya kufunzwa, nilijilaumu,
nikaona haya na kuaibika,
maana lawama za ujana wangu ziliniandama.’
20“Efraimu ni mwanangu mpendwa;
yeye ni mtoto wangu nimpendaye sana.
Ndio maana kila ninapomtisha,
bado naendelea kumkumbuka.
Moyo wangu wamwelekea kwa wema;
hakika nitamhurumia.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21“Weka alama katika njia zako,
simika vigingi vya kukuongoza,
ikumbuke vema ile njia kuu,
barabara uliyopita ukienda.
Ewe Israeli rudi,
rudi nyumbani katika miji yako.
22Utasitasita mpaka lini
ewe binti usiye mwaminifu?
Maana, mimi nimefanya kitu kipya duniani:
Mwanamke amtafuta mwanamume.”31:22 mwanamke … mwanamume: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
Fanaka siku zijazo
23Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nitakapowafanikisha tena watu wa Israeli, wao watatangaza tena katika nchi ya Yuda na katika miji yake wakisema:
‘Mwenyezi-Mungu akubariki ewe makao adili,
akubariki ee mlima mtakatifu!’
24“Ndipo watu wa Yuda na miji yake yote, wakulima na wachungaji wanaopitapita na makundi yao, watakaa huko pamoja. 25Waliochoka nitawachangamsha, na walegevu nitawapa nguvu. 26Ndio maana mtu ataweza kusema: ‘Niliamka nikatambua kwamba usingizi wangu ulinifaa sana.’”
27Mwenyezi-Mungu asema: “Tazama, siku zaja ambapo nitaijaza nchi ya Israeli na nchi ya Yuda watu na wanyama kama mkulima asiavyo mbegu. 28Na kadiri nilivyokuwa mwangalifu kuwangoa, kuwabomoa, kuwaangusha, kuwaharibu na kuwatesa, ndivyo nitakavyokuwa mwangalifu kuwapanda na kuwajenga. 29Siku hizo watu hawatasema tena:
‘Wazee walikula zabibu chungu,
na meno ya watoto yakatiwa ganzi.’
30La! Kila mmoja atakufa kwa sababu ya dhambi zake mwenyewe; ni yule tu atakayekula zabibu mbivu ndiye meno yake yatatiwa ganzi.”
31Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na watu wa Yuda. 32Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na wazee wao nilipowatoa kwa mkono wangu kutoka Misri; agano hilo walilivunja, ingawa mimi nilikuwa Bwana wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. 33Baada ya siku hizo, nitafanya agano lifuatalo na Waisraeli: Nitaiweka sheria yangu ndani yao, na kuiandika katika mioyo yao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. 34Wala haitawabidi kufundishana na kusema: ‘Mjue Mwenyezi-Mungu’, kwa sababu wote, wadogo kwa wakubwa, watanijua mimi Mungu. Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.” 35Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi, aliyepanga jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku, na aifanyaye bahari iwe na mawimbi: 36Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi hulifanya jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku; pia mimi huitikisa bahari, nayo hutoa mawimbi. Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Basi, nami nasema: Kadiri ninavyotegemeza mipango hiyo yote yangu kadiri hiyohiyo Israeli watakavyobaki kuwa watu wangu. 37Kama mbingu zaweza kupimwa, na misingi ya dunia kuchunguzwa, basi, nitawatupilia mbali wazawa wa Israeli, kwa sababu ya mambo yote waliyotenda. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
38Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo mji huu wa Yerusalemu utajengwa upya kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu, kutoka mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni. 39Nayo kamba ya kupimia itanyoshwa moja kwa moja hadi mlima Garebu, kisha itazungushwa hadi Goa. 40Bonde lote walimozikwa wafu na kutupiwa majivu, mashamba yote, mpaka kijito cha Kidroni, mpaka pembe ya lango la Farasi kuelekea mashariki, litakuwa eneo takatifu kwa Mwenyezi-Mungu. Hakuna kitakachoharibiwa humo wala kubomolewa tena milele.”

Yeremia31;1-40

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: