Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 9 September 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 7....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!

Ee Mwenyezi-Mungu, nakutukuza maana umeniokoa, wala hukuwaacha maadui zangu wanisimange. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nilikulilia msaada, nawe ukaniponya. Ee Mwenyezi-Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu; umenipa tena uhai, umenitoa miongoni mwa waendao kuzimu.
Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa, enyi waaminifu wake; kumbukeni utakatifu wake na kumshukuru. Hasira yake hudumu kitambo kidogo, wema wake hudumu milele. Kilio chaweza kuwapo hata usiku, lakini asubuhi huja furaha.
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Mimi nilipofanikiwa, nilisema: “Kamwe sitashindwa!” Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu, umeniimarisha kama mlima mkubwa. Lakini ukajificha mbali nami, nami nikafadhaika.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

Ujumbe kwa mfalme Ahazi
1 7:1 Taz 2Fal 16:5; 2Nya 28:5-6 
Wakati mfalme Ahazi mwana wa Yothamu na mjukuu wa Uzia, alipokuwa anatawala Yuda, Resini, mfalme wa Aramu, na Peka mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, waliushambulia mji wa Yerusalemu, lakini hawakuweza kuuteka. 2Mfalme wa Yuda alipopata habari kwamba Waashuru wanashirikiana na Waisraeli, yeye pamoja na watu wote wa Yuda waliogopa na kutetemeka kama miti inayotikiswa na upepo.
3Mwenyezi-Mungu akamwambia Isaya, “Mchukue mwanao, Shearyashubu,7:3 Shearyashubu: Maana yake watakaobaki watarudi. uende kukutana na mfalme Ahazi. Utamkuta barabarani mahali wanapofanyia kazi watengenezaji nguo, mwisho wa mfereji uletao maji kutoka bwawa la juu. 4Mwambie awe macho, atulie na asiogope wala asife moyo, kwa sababu ya hasira kali ya mfalme Resini wa Ashuru, na ya mwana wa Remalia. Hao wawili ni kama tu moshi wa kuni zinazozimika. 5Waashuru, kadhalika na Peka pamoja na jeshi la Efraimu wamefanya mpango mbaya dhidi yako. Wamesema, 6‘Twende kuivamia nchi ya Yuda, tuwatie watu hofu, tuitwae nchi na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme wao.’
7“Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Jambo hilo halitafaulu kamwe.
8,9Kwani mji mkuu wa Aramu ni Damasko,
na huyo Resini ni mkuu wa Damasko tu.
Mji mkuu wa Efraimu ni Samaria,
na mwana wa Remalia ni mkuu wa Samaria tu.
Mnamo miaka sitini na mitano utawala wa Efraimu utavunjwa;
Efraimu halitakuwa taifa tena.
Kama hutaamini hutaimarika.”

Ishara ya Emanueli
10Tena Mwenyezi-Mungu akamwambia Ahazi, 11“Mwombe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, akupe ishara; iwe ni kutoka chini kuzimu au juu mbinguni.” 12Ahazi akajibu, “Sitaomba ishara! Sitaki kumjaribu Mwenyezi-Mungu.” 13Basi, Isaya akamjibu, “Sikiliza basi, enyi watu wa ukoo wa Daudi! Je, haitoshi kuwachosha watu hata sasa mnataka kumchosha Mungu wangu pia? 147:14 Taz Mat 1:23 Haya basi, Bwana mwenyewe atawapa ishara: Msichana atachukua mimba, atajifungua mtoto wa kiume na kumwita jina lake Emanueli.7:14 Emanueli: Maana yake Mungu yu pamoja nasi. 15Atakula siagi na asali mpaka atakapojua kukataa mabaya na kuchagua mema. 16Maana, kabla mtoto huyo hajajua kukataa maovu na kuchagua mema, nchi za wafalme hao wawili unaowaogopa zitakuwa mahame. 17Mwenyezi-Mungu atakuletea wewe pamoja na watu wako na jamii yote ya kifalme siku za taabu kuliko zile zote zilizowahi kutokea tangu wakati watu wa Efraimu walipojitenga na Yuda; yaani, atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”
18Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atawapigia mruzi watu wa Misri waje kama nzi toka vijito vya mto Nili; na watu wa Ashuru waje kama nyuki kutoka nchi yao. 19Watakuja makundi kwa makundi na kuyajaza mabonde yaliyopasukapasuka, mapango miambani, miiba, vichaka vyote na malisho yote.
20Wakati huo, Bwana atakopa wembe kutoka ngambo ya mto Eufrate, yaani mfalme wa Ashuru. Atawanyoa vichwa vyenu, miili yenu na kukatilia mbali pia ndevu zenu.
21Wakati huo, mtu atafuga ng'ombe mmoja mchanga na kondoo wawili; 22nao watatoa maziwa kwa wingi hata aweze kula siagi. Watu watakaosalia katika nchi watakula siagi na asali.
23Wakati huo, kila mahali palipokuwa na mashamba ya mizabibu kwa maelfu ya thamani ya fedha 1,000 kwa kipimo cha hekalu yatakuwa mbigili na miiba mitupu. 24Watu watakwenda huko kuwinda kwa pinde na mishale, maana nchi yote itakuwa imejaa mbigili na miiba. 25Nayo milima yote iliyokuwa ikilimwa itakuwa imejaa mbigili na miiba, hata hakuna mtu atakayejaribu kwenda huko, badala yake itakuwa malisho ya ng'ombe na kondoo.

Isaya7;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: