Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 25 September 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 19....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: ‘Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.’ Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Yesu alipokwisha pandishwa na kuwekwa na Mungu upande wake wa kulia, akapokea kutoka kwake Baba yule Roho Mtakatifu ambaye alituahidi, ametumiminia huyo Roho. Hicho ndicho mnachoona sasa na kusikia.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, hadi niwafanye adui zako kiti cha miguu yako.’
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



Mungu ataiadhibu nchi ya Misri
1Kauli ya Mungu dhidi ya nchi ya Misri.
“Mwenyezi-Mungu amepanda juu ya wingu liendalo kasi
na kuja mpaka nchi ya Misri.
Sanamu za miungu ya Wamisri zitatetemeka mbele yake,
mioyo ya Wamisri itayeyuka kwa hofu.
2Mimi nitawachochea Wamisri wagongane:
Ndugu na ndugu yake,
jirani na jirani yake,
mji mmoja na mji mwingine,
mfalme mmoja na mfalme mwingine.
3Nitawaondolea Wamisri uhodari wao,
nitaivuruga mipango yao;
watatafuta maoni kwa sanamu na mizimu,
wachawi, mizuka na pepo.
4Nitawatia Wamisri mikononi mwa bwana katili,
mfalme mkali ambaye atawatawala.
Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nimenena.”
5Maji ya mto Nili yatakaushwa,
nao utakauka kabisa.
6Mifereji yake itatoa uvundo,
vijito vyake vitapunguka na kukauka.
Nyasi na mafunjo yake yataoza.
7Sehemu za kandokando ya Nili zitakuwa tupu.
Mimea yote iliyopandwa humo itakauka
na kupeperushiwa mbali na kutoweka.
8Wavuvi watalia na kuomboleza,
wote watumiao ndoana watalalama;
wote wanaotanda nyavu majini watakufa moyo.
9Wafuma nguo za kitani watakata tamaa,
wote kwa pamoja watakufa moyo.
10Wafuma nguo watafedheheshwa,
na vibarua watahuzunika.
11Viongozi wa mji wa Soani ni wapumbavu kabisa,
washauri wa Farao wanatoa shauri la kijinga!
Awezaje kila mmoja kumwambia Farao,
“Mimi ni mzawa wa mtaalamu stadi;
mzawa wa wafalme wa hapo kale!”
12Wako wapi, ewe Farao, wataalamu wako?
Waache basi wakuambie na kukujulisha
aliyopanga Mwenyezi-Mungu wa majeshi dhidi ya Misri!
13Lakini viongozi wa Soani ni wapumbavu,
wakuu wa Memfisi wamedanganyika.
Hao walio msingi wa makabila yao
wamelipotosha taifa la Misri.
14Mwenyezi-Mungu amewamwagia hali ya vurugu,
wakawapotosha Wamisri katika mipango yao yote,
wakawa kama mlevi anayeyumbayumba akitapika.
15Hakuna mtu yeyote nchini Misri,
kiongozi au raia, mashuhuri au duni,
awezaye kufanya lolote la maana.
Wamisri watamwabudu Mwenyezi-Mungu
16Siku ile watu wa Misri wataogopa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu watakapomwona Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameunyosha mkono wake dhidi yao. 17Yuda atakuwa tishio kubwa kwa Wamisri. Wote watakaoambiwa habari za Yuda wataingiwa na woga kwa sababu ya jambo aliloamua Mwenyezi-Mungu wa majeshi kuwatenda.
18Siku hiyo lugha ya Kiebrania itatumika katika miji mitano ya Misri, na watu wa miji hiyo wataapa kuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mji mmojawapo utaitwa “Mji wa Jua.”19:18 Mji wa Jua: Au Heliopoli, mji ulioko katika delta ya mto Nili; tafsiri nyingine: Mji wa Uharibifu.
19Siku hiyo, kutakuwa na madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu katikati ya nchi ya Misri, na nguzo iliyowekwa wakfu kwa Mungu kwenye mpaka wa Misri. 20Madhabahu hiyo itakuwa ishara na ushuhuda kwake Mwenyezi-Mungu wa majeshi katika nchi ya Misri. Watu wakimlilia Mwenyezi-Mungu humo kwa sababu ya kukandamizwa, yeye atawapelekea mkombozi atakayewatetea na kuwakomboa. 21Mwenyezi-Mungu atajijulisha kwa Wamisri na hapo ndipo Wamisri watakapomkiri na kumwabudu kwa kumtolea tambiko na sadaka za kuteketezwa. Hali kadhalika, watamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri ambazo watazitimiza. 22Mwenyezi-Mungu atawaadhibu Wamisri na kuwaponya. Nao watamrudia, naye atayasikiliza maombi yao na kuwaponya.
23Wakati huo, kutakuwa na barabara kuu kutoka nchi ya Misri hadi nchi ya Ashuru. Waashuru watawatembelea Wamisri, na Wamisri watawatembelea Waashuru; nao wote watamwabudu Mungu pamoja. 24Wakati huo, Israeli itahesabiwa pamoja na Misri na Ashuru; mataifa haya matatu yatakuwa baraka kwa dunia yote. 25Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawabariki na kusema, “Wabarikiwe Wamisri watu wangu, kadhalika na Waashuru ambao ni ishara ya kazi yangu na Waisraeli walio mali yangu.”

Isaya19;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: