Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 2 January 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 30...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante

 kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Jehovah  Jireh..!Jehovah Nissi..!Jehovah Raah..!
Jehovah Rapha..!Jehovah Shammah..!Jehovah Shamlom..!
Emanuel-Mungu pamohja nasi..!!
Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni..!

Hapo wakaanza kumhoji: “Haya, sasa tuambie! Kwa nini balaa hili linatupata? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? U kabila gani?” Yona akawajibu, “Mimi ni Mwebrania; namcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, muumba wa bahari na nchi kavu.” Kisha Yona akawaeleza kwamba alikuwa anamkwepa Mwenyezi-Mungu. Kusikia hayo, mabaharia hao wakazidi kujawa na hofu, wakamwambia, “Umefanya nini wewe!” Wakati huo wote, bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Basi, wakamwuliza Yona, “Tukufanye nini ili bahari itulie?”

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona.....

Yona akawajibu, “Nichukueni mkanitupe baharini, nayo bahari itatulia, maana naona wazi kwamba dhoruba hii imewapata kwa sababu yangu mimi.” Mabaharia hao wakajaribu bado kupiga makasia wapate kuifikisha meli yao pwani, lakini hawakufanikiwa kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia. Basi, wakamlilia Mwenyezi-Mungu wakisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, twakusihi usituangamize kwa kuutoa uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umefanya upendavyo.”

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu tunaomba ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Basi, wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, na papo hapo bahari ikatulia. Mabaharia hao wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu, wakamtolea sadaka na kuweka nadhiri. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaamuru samaki mkubwa ammeze Yona, naye akawa tumboni mwa samaki huyo kwa muda wa siku tatu, usiku na mchana.
Tazama wenye shida/tabu,watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh tunaomba  ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu  unajua haja za mioyo ya kila mmoja
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Jehovah ukaonekane katika maisha yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.

Sala ya shukrani
(Zaburi ya Daudi)
1Ee Mwenyezi-Mungu, nakutukuza maana umeniokoa,
wala hukuwaacha maadui zangu wanisimange.
2Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu,
nilikulilia msaada, nawe ukaniponya.
3Ee Mwenyezi-Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu;
umenipa tena uhai,
umenitoa miongoni mwa waendao kuzimu.
4Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa, enyi waaminifu wake;
kumbukeni utakatifu wake na kumshukuru.
5Hasira yake hudumu kitambo kidogo,
wema wake hudumu milele.
Kilio chaweza kuwapo hata usiku,
lakini asubuhi huja furaha.
6Mimi nilipofanikiwa, nilisema:
“Kamwe sitashindwa!”
7Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu,
umeniimarisha kama mlima mkubwa.
Lakini ukajificha mbali nami,
nami nikafadhaika.
8Nilikulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu;
naam niliomba dua kwako ee Mwenyezi-Mungu:
9“Je, utapata faida gani nikifa
na kushuka hadi kwa wafu?
Je, mavumbi ya wafu yanaweza kukusifu?
Je, yanaweza kusimulia uaminifu wako?
10Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie;
ee Mwenyezi-Mungu, unisaidie!”
11Wewe umegeuza maombolezo langu kuwa ngoma ya furaha;
umeniondolea huzuni yangu, ukanizungushia furaha.
12Mimi nitakusifu wala sitakaa kimya.
Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nitakushukuru milele.


Zaburi30;1-12

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: