Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 10 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme4......Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana Tumshukuru katika yote

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Baba wa yatima,
Mume wa wajane,Muweza wa yote,Alfa na Omega..!

Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa,Unasthahili kuabudiwa,
Unastahili kuhidiwa,Unatosha Baba wa mbinguni,
Neema yako yatutosha  Jehovah...!!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa uwepo wako,pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa 
majukumu yetu
Sifa na utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu....!!

Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu. Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe. Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo. Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake. Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja. Nyinyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote
waliotukosea
Jehovah usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mpinga
Kristo zishindwe katika jina lililo kuu jina la Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa
Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Nyinyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli; hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani, mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno lingine, kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa: “Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe.” Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema, “Naogopa na kutetemeka.”

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe 
kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu watoto,wazazi wetu,
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Yahweh tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Jehovah ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu 
Yesu Kristo....
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama rohoni Jehovah tunaomba ukatupe macho
ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Yahweh tunaomba ukatupe kutambua mema na mabaya
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Jehovah neema yako ya Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu Mungu wetu tukanene
yaliyo yako Yahweh ukatupe hekima,busara  na upendo ukadumu
kati yetu....
Mungu wetu ukatufanye barua njema Yahweh nasi tukasomeke 
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....Lakini nyinyi mmefika katika mlima wa Siyoni, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika kwa maelfu. Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa wakamilifu. Mmefika kwa Yesu ambaye ni mpatanishi katika agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema kuliko ile ya Abeli. Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza huyo anayesema nanyi. Kama wale waliokataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni? Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: “Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu.” Neno hili: “Tena” linatuonesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa. Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu; maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.

Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia
magumu/majaribu mbalimbali,walio katika vifungo vya yule mwovu
walio magerezani pasipo na hatia,walio umizwa rohoni,walio kataliwa
walio kata tamaa,wenye hofu na mashaka,waliokwama kibiashara,kielimu,waliopoteza matumaini,wafiwa ukawe mfariji wao,
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia,Jehovah tunaomba
ukabariki mashamba yao Mungu wetu ukawape ubunifu na maarifa
katika kazi/biashara zao Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaokoe na
kuwaweka huru Mungu wetu ukawape neema ya kufuata njia zako
Jehovah wakasimamie Neno lako Mungu wetu ukawape macho ya rohoni
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe,Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kujiombea na kutubu..
Mungu wetu tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Baba wa Mbinguni ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu  kwakuwanami/kunisoma
Mungu  wetu mwenye nguvu akawaguse kwa mkono wake wenye nguvu
Amani ikatawale katika maisha yetu upendo ukadumu kati yetu..
Nawapenda.
Elisha anamsaidia mjane maskini

1Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wanafunzi wa manabii akamwendea Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu amefariki, na kama ujuavyo, alikuwa mcha Mungu, lakini aliyemwia fedha amekuja kuwatwaa wanangu wawili wawe watumwa wake.” 2Elisha akamwuliza, “Sasa nikusaidieje? Niambie kile ulicho nacho nyumbani.” Mama huyo mjane akamjibu, “Mimi mtumishi wako sina kitu chochote ila chupa ndogo ya mafuta.” 3Elisha akamwambia, “Nenda kwa jirani zako uazime vyombo vitupu vingi kadiri utakavyopata. 4Kisha uende, wewe pamoja na wanao, mjifungie ndani ya nyumba, na muanze kujaza mafuta. Kila chombo mnachojaza, kiwekeni kando.” 5Akaenda na kujifungia ndani ya nyumba na wanawe na kuanza kumimina mafuta ndani ya vyombo. 6Vilipojaa vyote, akamwambia mwanawe mmojawapo, “Niletee chombo kingine.” Mwanae akamjibu, “Vyote vimejaa!” Hapo mafuta yakakoma kutiririka. 7Akarudi kwa mtu wa Mungu na kumweleza habari hizo. Naye mtu wa Mungu akamwambia, “Nenda ukauze hayo mafuta na kulipa madeni yako, ndipo wewe na wanao mtaishi kwa kutumia hayo yatakayobaki.”

Elisha na mama tajiri Mshunami

8Siku moja Elisha alikwenda Shunemu, ambako alikaa mama mmoja tajiri. Mama huyu akamwalika Elisha kwa chakula, na toka siku hiyo ikawa kawaida Elisha kula chakula kwake kila alipopitia huko. 9Mama huyo akamwambia mumewe, “Sina shaka kwamba mtu huyu anayefika kwetu kila mara ni mtakatifu wa Mungu. 10Mbona basi tusimjengee chumba na huko tumwekee kitanda, meza, kiti na taa, ili akitumie kila anapotutembelea?”
11Siku moja Elisha akaja huko na kuingia chumbani mwake ili apumzike. 12Akamwuliza mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyu mama Mshunami.” Alipomwita alikuja na kusimama mbele yake. 13Naye Elisha akamwambia Gehazi, “Mwambie, tumeona jinsi alivyotushughulikia; sasa anataka tumtendee jambo gani? Je, angependa aombewe lolote kwa mfalme au kwa jemadari wa jeshi?” Mama Mshunami akamjibu, “Mimi ninaishi miongoni mwa watu wangu.” 14Elisha akasema, “Tumfanyie nini basi?” Gehazi akamjibu, “Hakika hana mtoto, na mumewe amekuwa mzee.” 15Elisha akamwambia, “Mwite.” Naye akamwita. Akaja na kusimama mlangoni. 16Elisha akamwambia “Majira kama haya mwakani, utakapotimia mwaka ujao, wakati kama huu, utakuwa na mtoto mikononi mwako.” Mama akamjibu, “La, Bwana wangu! Wewe ni mtu wa Mungu; usinidanganye mimi mtumishi wako!” 17Lakini huyo mwanamke akapata mimba na kuzaa mtoto wakati kama huo mwaka uliofuata, kama Elisha alivyokuwa amemwambia.
18Mtoto huyo alipokua, alitoka siku moja pamoja na baba yake akafuatana na wavunaji, 19naye akamwambia baba yake, “Ole, kichwa changu! Naumwa na kichwa!” Baba yake akamwambia mtumishi wake mmoja, “Mpeleke kwa mama yake.” 20Alipofikishwa kwa mama yake, alikaa juu ya magoti ya mama yake mpaka adhuhuri, halafu akafa. 21Mama yake akampeleka na kumlaza kitandani mwa mtu wa Mungu, akaufunga mlango na kuondoka. 22Akamwita mumewe na kumwambia, “Nipe mtumishi mmoja na punda mmoja, ili nimwendee mara moja yule mtu wa Mungu, kisha nitarudi.” 23Mumewe akamwuliza, “Mbona unataka kumwona leo? Leo si siku ya mwezi mwandamo wala Sabato?” Akamjibu, “Usijali.” 24Akatandika punda na kumwambia mtumishi, “Sasa kaza mwendo, wala usipunguze mpaka nitakapokuambia.” 25Basi, akaondoka, akaenda mpaka mlima Karmeli alipokuwa mtu wa Mungu.
Mtu wa Mungu alipomwona akija, akamwambia Gehazi mtumishi wake, “Tazama, namwona Mshunami akija; 26kimbia mara moja ukakutane naye na kumwambia, ‘Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo?’” Naye Mshunami akamjibu “Hatujambo.” 27Alipofika mlimani kwa mtu wa Mungu akamshika miguu, naye Gehazi akakaribia ili amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, “Mwache, kwani ana uchungu mkali, naye Mwenyezi-Mungu hakunijulisha jambo hilo.” 28Huyo mama akamwambia, “Bwana wangu, je, si nilikuomba mtoto? Kwani sikukusihi usije ukanipa matumaini ambayo yangenipa huzuni baadaye?”
29Elisha akamwambia Gehazi, “Chukua fimbo yangu, uondoke mara moja. Usisimame njiani kumwamkia mtu yeyote, na mtu yeyote akikuamkia njiani, usipoteze wakati kurudisha salamu. Nenda moja kwa moja mpaka nyumbani na kuweka fimbo yangu juu ya mtoto.”
30Mwanamke akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe uishivyo, sitakuacha.” Basi Elisha akaondoka na kufuatana naye. 31Gehazi akatangulia mbele, na alipofika akaweka fimbo ya Elisha juu ya uso wa mtoto, lakini hakukuonekana dalili yoyote ya uhai. Akarudi na kukutana na Elisha, akamwambia, “Kijana hakufufuka.”
32Elisha alipofika, akaingia peke yake chumbani na kuona maiti ya kijana kitandani. 33Basi, akafunga mlango na kumwomba Mwenyezi-Mungu. 34Ndipo akajilaza juu ya mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, na macho yake juu ya macho ya mtoto na mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Na alipokuwa amekaa hivyo, mwili wa mtoto ukaanza kupata joto. 35Elisha akasimama na kutembeatembea chumbani, kisha akarudi na kujilaza tena juu ya mtoto. Mtoto akapiga chafya mara saba, halafu akafungua macho. 36Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite yule Mshunami.” Alipoitwa Elisha akamwambia, “Mchukue mwanao.” 37Akainama miguuni pa Elisha kwa shukrani na kumchukua mwanawe.

Miujiza mingine miwili ya Elisha

38Elisha akarudi Gilgali wakati nchini kulikuwa na njaa. Siku moja, alipokuwa akifundisha wanafunzi wa manabii alimwambia mtumishi wake, “Weka chungu kikubwa motoni, uwapikie manabii.” 39Mmoja wao akaenda shambani na kuchuma mboga. Huko akaona mtango-mwitu, akachuma matango mengi kadiri alivyoweza kuchukua. Akaja nayo, akayakatakata na kuyatia chunguni bila kuyajua. 40Chakula kikapakuliwa. Lakini walipokionja wakamlilia Elisha wakisema, “Ee mtu wa Mungu, chakula hiki kitatuua!” Nao hawakuweza kukila. 41Elisha akaagiza aletewe unga. Akaletewa unga, naye akautia ndani ya chungu na kusema, “Sasa wape chakula wale.” Wakakila, na hapo hakikuwadhuru.
42Mtu Mmoja akatoka Baal-shalisha, akamletea Elisha mikate ishirini iliyotengenezwa kwa shayiri ya malimbuko ya mavuno ya mwaka huo na masuke mabichi ya ngano guniani. Elisha akamwagiza Gehazi awape watu wale. 43Mtumishi wake akasema, “Sitawapa kwa sababu hakitawatosha watu 100”. Elisha akasema, “Wape wale, kwa sababu Mwenyezi-Mungu amesema kwamba watakula washibe na kingine kitabaki.” 44Mtumishi wake akawaandalia chakula, wakala wote wakashiba, na kingine kikabaki, kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.
2Wafalme4;1-44


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: