Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 4 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 22...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha 
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa makujumu yetu
Utukuzwe ee Baba wa Mbinguni,Usifiwe Jehovah,Uhimidiwe ee Yahweh,
Uabudiwe ee Mungu wetu,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni
ya ajabu,Matendo yako yanatisha,hakuna kama wewe ee Mungu wetu,
wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,wewe ni alfa na Omega...
Neema yako yatutosha Mungu wetu...!!Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu. Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanauamini ujumbe huu. Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu. Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni. Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo.Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovaha nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Yahweh usitutie katika majaribu Mungu wetu tunaomba utuokoe na yule
mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Jehovah tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
kama inavyokupendeza wewe...Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa. Nyinyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu. Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, “Mtu yeyote asiyependa kufanya kazi, asile chakula.” Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine. Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe. Lakini nyinyi ndugu, msichoke kutenda mema. Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye, kusudi aone aibu. Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu.Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu
tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni
tukawe salama rohoni Jehovah tunaomba ukatupe macho ya kuona
na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,Jehovah ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni...
Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,amani ikatawale na upendo
ukadumu kati yetu...
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...Bwana mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote. Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika. Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.Mungu wetu tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba
kwa bidii/imani Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako
wenye nguvu,Mungu wetu tunaomba ukawatendee kila mmoja
na mahitaji yake,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kimwili
na kiroho pia,Jehovah ukaonekane katika maisha yao Mungu wetu
ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe..
Jehovah tunaomba ukawape macho ya kuona Mungu wetu ukawape
Neema ya kujiombea,kufuata njia zako nazo ziwaweke huru
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yao
Nuru ikaangaze ukawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele....
Amina...!!

Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwanami/kunisoma
Baba wa Mbinguni akawaguse kwa mkono wake wenye nguvu
akawabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye...
Amani ya Kristo Yesu ikawe nanyi Daima....
Nawapenda. 

Nabii Mikaya amwonya Ahabu

(2Nya 18:2-27)
1Kwa muda wa miaka mitatu hivi, kulikuwa na amani kati ya Israeli na Aramu. 2Lakini mnamo mwaka wa tatu, Yehoshafati, mfalme wa Yuda, alifika kumtembelea Ahabu, mfalme wa Israeli. 3Ahabu akawaambia watumishi wake, “Je, hamjui kwamba Ramoth-gileadi ni mali yetu? Mbona basi tunajikalia tu bila kuunyakua kutoka kwa mfalme wa Aramu?” 4Kisha akamwambia Yehoshafati, “Je, utaandamana nami kupigana huko Ramoth-gileadi?” Naye Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Naam; mimi na wewe ni kitu kimoja, na pia watu wangu ni watu wako, farasi wangu ni farasi wako.” 5Kisha Yehoshafati aliendelea kumwambia mfalme wa Israeli: “Lakini, kwanza mwulize Mwenyezi-Mungu ushauri.”
6Basi, Ahabu akaitisha kikao cha manabii wapatao 400, akawauliza, “Je, niende nikaushambulie mji wa Ramoth-gileadi au nisiende?” Wao wakamjibu: “Nenda! Mwenyezi-Mungu atakupatia ushindi.” 7Lakini, Yehoshafati akasema, “Je, hapa hakuna nabii mwingine wa Mwenyezi-Mungu ambaye twaweza kumwuliza shauri?” 8Naye mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Yupo, bado mmoja, Mikaya mwana wa Imla. Yeye twaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu. Lakini namchukia sana kwa sababu yeye, kamwe hatabiri jambo jema juu yangu, ila mabaya tu.” Yehoshafati akamwambia, “Si vizuri mfalme kusema hivyo.” 9Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwita mtumishi mmoja, akamwamuru, “Haraka! Nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.” 10Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme; wakati huo manabii wote wakawa wanatabiri mbele yao. 11Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Waaramu na kuwaangamiza.’” 12Hata wale manabii wengine wote wakatabiri vivyo hivyo, wakasema, “Nenda uushambulie Ramoth-gileadi, utashinda! Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”
13Wakati huo, yule mtumishi aliyetumwa kwenda kwa Mikaya, alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja, wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali, nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.” 14Lakini Mikaya akamjibu, “Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, mimi nitasema tu yale atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.”
15Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme alimwuliza, “Je, twende kupigana vita huko Ramoth-gileadi ama tusiende?” Naye alimjibu, “Nenda na ufanikiwe, naye Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.” 16Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?” 17Ndipo, Mikaya akasema, “Niliona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; basi warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’”
18Hapo, mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kamwe hatatabiri jema juu yangu ila mabaya tu?” 19Kisha Mikaya akasema, “Haya sikia neno la Mwenyezi-Mungu: Nilimwona Mwenyezi-Mungu ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni limesimama kando yake, upande wake wa kulia na wa kushoto; 20ndipo Mwenyezi-Mungu akauliza, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu aende akaangamie huko Ramoth-gileadi?’ Kila mmoja akajibu alivyofikiri. 21Kisha pepo mmoja akajitokeza mbele ya Mwenyezi-Mungu, akasema, ‘Mimi nitamshawishi.’ 22Mwenyezi-Mungu akamwuliza, ‘Kwa mbinu gani?’ Naye akajibu, ‘Nitakwenda na kuwafanya manabii wake wote waseme uongo.’ Mwenyezi-Mungu akamwambia, ‘Wewe utamshawishi na utafaulu; haya, nenda ukafanye hivyo.’ 23Basi, ndivyo ilivyo: Mwenyezi-Mungu amewafanya hawa manabii wako wote waseme uongo. Mwenyezi-Mungu amenena mabaya juu yako!”
24Hapo, Sedekia, mwana wa Kenaana, akamkaribia Mikaya, akampiga kofi shavuni na kumwuliza, “Tangu lini Roho ya Mwenyezi-Mungu ikaniacha mimi, ikaja kunena nawe?” 25Mikaya akamjibu, “Siku utakapoingia katika chumba cha ndani kujificha, ndipo utakapojua.” 26Naye mfalme wa Israeli akatoa amri, “Mkamateni Mikaya; mrudisheni kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme. 27Waambie wamtie gerezani na kumlisha mkate kidogo na maji, mpaka nitakaporudi salama.” 28Ndipo Mikaya aliposema, “Ukirudi salama basi, utajua kwamba Mwenyezi-Mungu hakunena nami.” Kisha akaendelea kusema, “Sikilizeni enyi watu wote!”

Kifo cha Ahabu

(2Nya 18:28-34)

29Basi, mfalme wa Israeli akaenda pamoja na mfalme Yehoshafati wa Yuda, kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi. 30Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Mimi nitavaa mavazi yasiyo ya kifalme na kuingia vitani lakini wewe utavaa mavazi yako ya kifalme.” Hivyo mfalme wa Israeli akaenda vitani bila kuvaa mavazi ya kifalme.
31Mfalme wa Aramu alikuwa amewaamuru makapteni wake thelathini na wawili waliosimamia magari yake ya kukokotwa, akisema: “Msipigane na mtu yeyote yule, mkubwa au mdogo, ila tu na mfalme wa Israeli.” 32Baadaye, makapteni hao walipomwona Yehoshafati, walisema: “Kweli, huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo, walimwelekea, wakamshambulia; lakini Yehoshafati akapiga kelele. 33Makapteni walipotambua kwamba hakuwa mfalme wa Israeli waliacha kumshambulia, wakarudi. 34Lakini, askari mmoja wa Aramu, akauvuta upinde wake kwa kubahatisha, mshale ukamchoma mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma kifuani. Ahabu akamwambia dereva wa gari lake, “Geuza gari uniondoe vitani. Nimejeruhiwa!” 35Na mapigano siku hiyo yakazidi kuwa makali, huku mfalme ameegemeshwa garini, anawaelekea watu wa Aramu. Ilipofika jioni, akafariki. Damu ikawa inamtoka jerahani mwake na kutiririka hadi chini ya gari. 36Mnamo machweo ya jua, amri ikatolewa: “Kila mtu arudi mjini kwake; kila mtu arudi nchini kwake!”
37Mfalme Ahabu alipofariki maiti yake ilipelekwa Samaria, ikazikwa huko. 38Gari lake la kukokotwa waliliosha katika bwawa la Samaria, mbwa wakairamba damu yake, nao makahaba wakaoga humo, sawa kabisa na neno alilosema Mwenyezi-Mungu.
39Matendo mengine ya mfalme Ahabu, jinsi alivyojenga na kupamba nyumba yake kwa pembe, na miji yote aliyojenga, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. 40Ahabu alipofariki, mwanawe Ahazia alitawala mahali pake.

Yehoshafati, mfalme wa Yuda

(2Nya 20:31–21:1)
41Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Ahabu wa Israeli, Yehoshafati mwana wa Asa, alianza kutawala Yuda. 42Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala. Alitawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na mitano. Mama yake alikuwa Azuba binti Shilhi. 43Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya baba yake Asa. 44Lakini hakupaharibu mahali pa kutambikia vilimani. Watu waliendelea kutambikia na kufukiza ubani mahali hapo. 45Yehoshafati pia, alifanya mapatano ya amani na mfalme wa Israeli.
46Matendo mengine ya Yehoshafati, ushujaa wake na vita alivyopigana, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Wafiraji wote wa kidini waliosalia tangu nyakati za baba yake Asa, Yehoshafati aliwaondoa nchini.
47Katika nchi ya Edomu, hapakuwa na mfalme. Nchi hiyo ilitawaliwa na naibu.
48Mfalme Yehoshafati aliunda meli za kwenda Ofiri kuleta dhahabu lakini hazikufika kwa sababu zilivunjikavunjika huko Esion-geberi. 49Basi, Ahazia mwana wa Ahabu, akamwambia Yehoshafati, “Waache watumishi wangu wasafiri pamoja na watumishi wako katika meli.” Lakini Yehoshafati hakukubali jambo hilo.
50Hatimaye, Yehoshafati alifariki, na kuzikwa pamoja na babu zake katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi baba yake; naye Yehoramu, mwanawe, akatawala mahali pake.

Ahazia, mfalme wa Israeli

51Mnamo mwaka wa kumi na saba wa utawala wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Ahazia, mwana wa Ahabu, alianza kutawala Israeli. Alitawala kwa muda wa miaka miwili, kutoka Samaria. 52Ahazia alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; aliuiga mwenendo wa baba yake na mwenendo wa Yezebeli, mama yake, na wa Yeroboamu, mwana wa Nebati ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi. 53Alimtumikia na kumwabudu Baali, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kila jambo kama alivyofanya baba yake.
1Wafalme22;1-53


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: