Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 17 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 9......Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma
,Mungu mwenye kuponya,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Muweza wa yote Alfa na Omega...!!

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa uwepo wako,pumzi/uzima,afya na kuwa tayari 
kwa majukumu yetu
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...!!


Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu. Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani. Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.” Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini. Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Tazama jana imepita  ee Mungu wetu leo ni siku mpya Baba wa Mbinguni
na kesho ni siku nyingine Jehovah....
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote
waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi
zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni. Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia; ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Kwa hiyo nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako.” Tena Maandiko yasema: “Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake.” Na tena: “Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni.” Tena Isaya asema: “Atatokea chipukizi katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia.” Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Jehovah ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Yahweh tukawe salama rohoni Baba wa Mbinguni ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu neema yako na Nuru
yako ikaangaze katika maisha yetu,hekima,busara vikawe nasi  upendo
ukadumu kati yetu....
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama 
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba nyinyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana nyinyi kwa nyinyi. Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa tambiko inayokubaliwa na Mungu, tambiko iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu. Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo, kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo. Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Watu wote ambao hawakuambiwa habari zake wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.”

Baba wa Mbinguni tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya
yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,walio kataliwa,
walio kata tamaa,wenye hofu na mashaka,walioumizwa rohoni,
waliokwama kibiashara,waliokwama kielimu...
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Jehovah tunaomba ukawaponye na kuwaokoa,Mungu wetu ukawaweke huru na haki ikatendeke ,Baba wa Mbinguni ukabariki mashamba,biashara na kazi  zao
Yahweh tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Jehovah tunaomba ukawape neema ya kujiombea na kufuata njiza zako
nazo zikawaweke huru
Neema na nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Ee Mungu wetu tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/
kunisoma Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye,Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo
wa Mungu Baba vikawe nanyi daima....
Nawapenda. 
  

Yehu atawazwa kuwa mfalme wa Israeli

1Wakati huohuo nabii Elisha alimwita mmoja wa wanafunzi wa manabii, akamwambia, “Jitayarishe kwenda Ramothi katika Gileadi. Chukua chupa hii ya mafuta 2na utakapofika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati na mjukuu wa Nimshi. Mchukue kando chumbani mbali na wenzake, 3kisha chukua chupa hii ya mafuta, ummiminie kichwani na kumwambia, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimekupaka mafuta kuwa mfalme wa Israeli.’ Kisha fungua mlango na kuondoka upesi utakavyoweza.”
4Basi, Nabii huyo kijana akaenda Ramothi Gileadi. 5Alipofika aliwakuta makamanda wa jeshi mkutanoni. Akasema “Nina ujumbe wako, kamanda.”
Yehu akamwuliza, “Ni nani kati yetu unayemwambia?” Akamjibu, “Wewe, kamanda.” 6Ndipo wote wawili wakaingia chumba cha ndani na huko nabii akamtia Yehu mafuta kichwani na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema, ‘Nakupaka mafuta uwe mfalme juu ya watu wangu Israeli. 7Nawe utaipiga jamaa ya bwana wako Ahabu ili nimlipize kisasi Yezebeli damu ya watumishi wangu manabii na ya watumishi wangu wote. 8Utafanya hivyo kwa sababu jamaa yote ya Ahabu itaangamia; pia nitamkatilia mbali kila mwanamume wa jamaa ya Ahabu awe mtumwa au mtu huru. 9Jamaa yake itakuwa kama jamaa ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ya Baasha mwana wa Ahiya. 10Yezebeli hatazikwa na mtu, maiti yake italiwa na mbwa katika nchi ya Yezreeli.’” Baada ya kusema hayo, nabii akaondoka chumbani na kukimbia.
11Yehu aliporudi kwa wenzake, mmoja wao alimwuliza, “Kuna shida yoyote? Mwendawazimu huyu alitaka nini kwako?” Yehu akawajibu, “Mnajua alichotaka.” 12Nao wakamwambia, “Hiyo si kweli! Tuambie alilosema!” Akawaambia, “Aliniambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema, ‘Nimekutawaza kuwa mfalme wa Israeli.’”
13Mara moja makamanda wenzake wakavua mavazi yao, wakayarundika pamoja kwenye ngazi ili asimame juu yake, wakapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Yehu ni mfalme!”

Mfalme Yoramu wa Israeli auawa

14Yehu mwana wa Yehoshafati, ambaye pia alikuwa mjukuu wa Nimshi, alikula njama dhidi ya Yoramu. Yoramu na watu wote wa Israeli walikuwa Ramoth-gileadi kulinda zamu dhidi ya mfalme Hazaeli wa Aramu. 15Lakini mfalme Yoramu alikuwa amerudi Yezreeli ili apone majeraha aliyopata wakati wa kupigana vitani na mfalme Hazaeli wa Aramu. Yehu aliwaambia maofisa wenzake; “Ikiwa mtakubaliana nami, mtu yeyote asitoke Ramothi kwenda Yezreeli kupeleka habari hizi.” 16Ndipo akapanda gari lake na kuelekea Yezreeli. Yoramu alikuwa bado hajapona, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa amemtembelea.
17Mlinzi aliyekuwa kwa zamu juu ya mnara wa Yezreeli akasema, “Naona watu wakija na gari!” Yoramu akajibu, “Chagua mpandafarasi mmoja, umtume ili akutane nao, awaulize ‘Kuna amani?’” 18Basi, mjumbe huyo alipokwenda alikutana na Yehu na kumwambia, “Mfalme anauliza: Kuna amani?” Yehu akajibu, “Kwa nini unauliza kuhusu amani? Wewe geuka ufuatane nami!” Mlinzi juu ya mnara akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini harudi.” 19Ndipo mjumbe wa pili akatumwa, ambaye pia alimwuliza Yehu swali hilohilo. Yehu akamwambia vivyo hivyo, “Kwa nini unauliza kuhusu amani? Wewe geuka ufuatane nami!” 20Kwa mara nyingine tena mlinzi akasema “Mjumbe amewafikia lakini harudi.” Halafu akaongeza, “Uendeshaji wa gari ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi; kwa sababu yeye huendesha kwa kasi.”
21Basi, Yoramu mfalme wa Israeli akaamuru akisema, “Tayarisha gari.” Nao walitayarisha gari lake. Kisha Yoramu mfalme wa Israeli na Ahazia mfalme wa Yuda waliondoka kila mmoja akipanda gari lake, wakaenda kukutana na Yehu. Walimkuta katika uwanja wa Nabothi Myezreeli. 22Ikawa Yoramu, alipomwona Yehu, alimwuliza, “Je, kuna amani, Yehu?” Yehu akamjibu, “Amani gani, wakati makahaba na wachawi wa Yezebeli ni wengi?” 23Yoramu aligeuza gari lake na kuondoka, huku akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini Ahazia!” 24Yehu akatwaa upinde wake na kutupa mshale ambao ulipenya mabega ya Yoramu na kuchoma moyo wake, naye akafa papo hapo garini mwake. 25Yehu akamwambia msaidizi wake Bidkari, “Chukua hiyo maiti yake uitupe katika shamba hilo la Nabothi Myezreeli. Kwa maana, kumbuka wewe na mimi tulipokuwa tumepanda farasi wetu nyuma ya baba yake Ahabu, jinsi Mwenyezi-Mungu alivyonena maneno haya dhidi yake. 26Mwenyezi-Mungu alisema, ‘Kwa ile damu ya Nabothi na kwa damu ya wanawe niliyoona jana naapa kwamba nitakulipiza kisasi katika shamba hilo.’ Kwa hiyo, chukua maiti ya Yoramu uitupe katika shamba la Nabothi kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.”

Mfalme Ahazia wa Yuda auawa

27Ahazia mfalme wa Yuda alipoona yaliyotukia alikimbia akielekea Nyumba ya Bustani, huku akifuatwa na Yehu. Yehu akawaamuru watu wake, “Muueni naye pia!” Nao wakampiga mshale akiwa garini kwenye njia ya kupanda Guri karibu na mji wa Ibleamu. Halafu alikimbilia Megido na kufia huko. 28Maofisa wake wakaichukua maiti yake ndani ya gari lake na kuipeleka Yerusalemu; na huko akazikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi.
29Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda katika mwaka wa kumi na moja wa enzi ya Yoramu mwana wa Ahabu.

Malkia Yezebeli auawa

30Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli alikuwa amekwisha pata habari za mambo yaliyotokea. Alijipaka rangi machoni na kupanga nywele zake, ndipo akaenda dirishani na kuangalia chini. 31Yehu alipokuwa akiingia langoni Yezebeli alisema, “Unakuja kwa amani, ewe Zimri! Wewe unayewaua mabwana zako?” 32Yehu akaangalia juu na kusema “Ni nani aliye upande wangu?” Maofisa wawili au watatu wakatokeza vichwa vyao kumwangalia kutoka dirishani, 33naye Yehu akawaambia, “Mtupe chini!” Wakamtupa chini na damu yake ikatapakaa juu ya ukuta na kwenye farasi. Yehu akapitisha farasi na gari lake juu ya maiti yake 34na kuingia katika jumba la kifalme, na huko akala na kunywa. Halafu akaamuru: “Mzikeni mwanamke huyo aliyelaaniwa; kwa kuwa ni binti mfalme.” 35Ndipo walipokwenda kumzika; lakini hawakuona chochote isipokuwa fuvu la kichwa, mifupa ya mikono na miguu. 36Kisha walirudi na kumpasha Yehu habari hizi, naye akasema, “Hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyotabiri kupitia kwa mtumishi wake Elia Mtishbi akisema, ‘Mbwa wataula mwili wa Yezebeli katika nchi ya Yezreeli. 37Maiti yake Yezebeli itakuwa kama mavi shambani katika nchi ya Yezreeli, hivyo kwamba hakuna atakayeweza kumtambua.’”
2Wafalme9;1-37


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: