Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 19 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 11......
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,Isaka
na Yakobo,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane,Baba wa Upendo,Baba wa baraka,Baba wa huruma,Mungu mwenye kusamehe..
Matendo yako ni makuu mno,Mtendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha,Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...!!

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa uwepo wako,pumzi/uzima,afya na kuwa tayari 
kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu...
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni!!Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja, tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu. Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule uasi utokee na yule Mwovu aonekane, ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa. Yeye hujikuza yeye mwenyewe juu ya kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu; hata ataingia na kuketi ndani ya hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu.


Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,Kwakunena,Kwakutenda,Kwakujua/Kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Yahweh usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuokoe na yule
mwovu kazi zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...

Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi? Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao. Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe. Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mngao wa kuja kwake. Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo, na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe. Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo. Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, bali wanafurahia dhambi, watahukumiwa.

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Baba wa Mbinguni
tukawe salama rohoni Yahweh tunaomba ukatupe macho ya kuona na 
masikio ya kusikia sauti sauti yako na kuitii..
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu
Yahweh ukatupe hekima,busara,utu wema  na upendo ukadumu kati yetu
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi ndugu, nyinyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho, mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli. Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, simameni imara na kuzingatia yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua yetu. Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema, aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili muweze daima kutenda na kusema yaliyo mema.

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,
waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,walio katika
vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia na wengine
wote kulingana na mahitaji yao...
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawatendee kila mmoja na hitaji lake
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Baba wa Mbinguni ukawaokoe na kuwaweka huru
Jehovah ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukabariki mashamba/kazi zao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawape neema ya kujiombea
kufuata njia zako na kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,amani ikatawale kati yao
Ee Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki katika yote yampendezayo
Upendo wa Mungu ukawe nanyi daima...
Nawapenda.


Malkia Athalia wa Yuda

(2Nya 22:10-23:15)

1Mara Athalia, mamake mfalme Ahazia, alipoona kuwa mwanawe ameuawa, alitoka, akaangamiza jamii yote ya kifalme. 2Lakini Yehosheba binti ya mfalme Yoramu, dada yake Ahazia, alimchukua kwa siri Yoashi mwana wa Ahazia, kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Alimficha11:2 Kiebrania hakina “alimficha”. yeye pamoja na yaya wake katika chumba cha kulala. Hivyo walimficha ili Athalia asimwone na kumwua. 3Yoashi alikaa naye kwa muda wa miaka sita akiwa amefichwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi.
4Lakini katika mwaka wa saba Yehoyada alituma ujumbe na kuwakusanya makapteni wa Wakari na walinzi; akaamuru wamjie katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akafanya nao mapatano na kuwaapisha humo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akawaonesha Yoashi mwana wa mfalme Ahazia. 5Kisha akatoa amri: “Mtafanya hivi: Mtakapokuja kushika zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda ikulu; 6theluthi nyingine ikiwa kwenye lango la Suri na theluthi nyingine ikiwa kwenye lango nyuma ya walinzi. Hivyo ndivyo mtakavyolinda ikulu ili isivunjwe. 7Yale makundi mawili ambayo humaliza zamu yao siku ya Sabato yatashika zamu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kumlinda mfalme. 8Mtamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi na mtu yeyote atakayethubutu kuwakaribia lazima auawe. Lazima mkae na mfalme, awe anatoka au anakaa.”
9Makapteni walitii amri zote alizotoa kuhani Yehoyada. Kila ofisa akawachukua watu wake wote, wale waliokuwa wamemaliza zamu na wale waliokuwa wanaingia kushika zamu siku ya Sabato, basi wakamwendea kuhani Yehoyada. 10Kisha kuhani akawapa makapteni mikuki na ngao zilizokuwa mali ya mfalme Daudi, na ambazo zilikuwa zimewekwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, 11nao walinzi walisimama kuanzia upande wa kusini wa nyumba mpaka upande wa kaskazini wa nyumba na kuzunguka madhabahu na nyumba ili kumzunguka mfalme;11:11 kumzunguka mfalme: Makala ya Kiebrania si dhahiri. kila mtu akiwa ameshika mkuki wake mkononi. 12Halafu akamtoa nje mwana wa mfalme, akamvika taji kichwani, na kumpa ule ushuhuda; wakamtawaza na kumpaka mafuta; wakapiga makofi na kusema, “Aishi mfalme!”
13Naye Athalia aliposikia sauti za walinzi pamoja na za watu wengine, aliwaendea hao watu waliokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 14Alipochungulia akamwona mfalme mpya amesimama karibu na nguzo kwenye lango la hekalu, kama ilivyokuwa desturi, huku makapteni na wapiga tarumbeta wakiwa kando ya mfalme; na wakazi wote wakishangilia na kupiga tarumbeta; ndipo aliporarua nguo zake na kusema kwa sauti kubwa, “Uhaini! Uhaini!”
15Kisha kuhani Yehoyada akaamuru makapteni wa jeshi akisema; “Mtoeni nje katikati ya askari, na ueni mtu yeyote atakayemfuata.” Kwa sababu kuhani alisema, “Asiuawe katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” 16Basi, wakamkamata, wakampeleka na kumpitisha kwenye Lango la Farasi kuelekea ikulu, naye akauawa huko.

Mabadiliko ya Yehoyada

(2Nya 23:16-21)

17Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Mwenyezi-Mungu na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Mwenyezi-Mungu; kadhalika alifanya agano kati ya mfalme na watu. 18Halafu wakazi wote wakaenda kwenye nyumba ya Baali na kuibomoa, wakavunja madhabahu pamoja na sanamu zake, hata wakamuua Matani, kuhani wa Baali mbele ya madhabahu. Kuhani Yehoyada akaweka walinzi kulinda nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 19Aliwachukua makapteni, Wakari na wakazi wote; nao wakamsindikiza mfalme kutoka nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakapitia katika lango la walinzi mpaka ikulu. Naye akakikalia kiti cha enzi. 20Kwa hiyo, wakazi wote walijawa furaha; na mji wote ulikuwa mtulivu, baada ya Athalia kuuawa kwa upanga katika ikulu.
21 11:21 Kiebrania: 12:1. Yoashi alianza kutawala Yuda akiwa na umri wa miaka saba.2Wafalme11;1-21


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: