Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 20 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 12......
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa uwepo wako,pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa makujukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu
Sifa na Utukufu  tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni..!!


Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu, nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu. Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao. Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani. Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
 na kujiachilia mikononi mwako ee Mungu wetu
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea
Mungu wetu utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe na
 yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike na damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana. Wanapenda kuwa waalimu wa sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza. Twajua kwamba sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo. Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia, watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale; sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wezi wa watu, waongo na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho sahihi. Mafundisho hayo hupatikana katika injili ya Mungu mtukufu na mwenye heri ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu 
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Jehovah tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama rohoni Baba wa Mbinguni tunaomba
ukatupe macho ya kuona na  masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Yahweh tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu Jehovah popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Baba wa Mbinguni
nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie, ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya. Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu. Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote, lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aoneshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uhai wa milele. Kwake yeye aliye Mfalme wa milele, asiyekufa, asiyeonekana na aliye Mungu pekee – kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina. Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri, na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao. Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

Mungu wetu tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani
Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah tunaomba ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie kulia kwao Mungu wetu
tunaomba ukawafute machozi yao
Yahweh ukaonekane katika mapito/majaribu yao
Mungu wetu tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Jehovah tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawape neema ya ujiombea,kufuata
njia zako na kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Nuru yako ikaangze katika maisha yao,amani ikatawale upendo
ukadumu kati yao...
Ee Baba tunaomba ukasikie kuomba kwetu Mungu wetu ukapokee sala/maombi yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Mungu mwenye nguvu na baraka akawabariki na kuwatendea
sawasawa na mapenzi yake
Amani,furaha na upendo vikadumu kati yetu...
Nawapenda.


Mfalme Yoashi wa Yuda

(2Nya 24:1-16)

1Katika mwaka wa saba wa enzi ya mfalme Yehu wa Israeli Yoashi alianza kutawala Yuda huko Yerusalemu, naye akatawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia, kutoka Beer-sheba. 2Wakati wa maisha yake yote alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu kuhani Yehoyada alikuwa akimfundisha. 3Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia miungu hapakuharibiwa, na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani huko.
4Yoashi akaita makuhani na kuwaamuru, akisema, “Fedha yote inayoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ikiwa imetokana na uuzaji wa vitu vitakatifu, fedha ya kila mtu kadiri alivyoandikiwa, na fedha ambayo mtu huvutwa kuitoa kwa hiari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, 5makuhani wazipokee kutoka kwa kila mtu; nao warekebishe nyumba popote panapohitajika marekebisho.”
6Lakini hata baada ya miaka ishirini na mitatu ya mfalme Yoashi makuhani walikuwa bado hawajafanya marekebisho yoyote ya nyumba. 7Kwa hiyo mfalme Yoashi alimwita kuhani Yehoyada na makuhani wengine na kuwauliza, “Mbona hamrekebishi nyumba? Basi, msichukue fedha kutoka kwa watu mnaowatumikia, bali mtazileta, ili nyumba irekebishwe.” 8Makuhani wakakubali wasipokee fedha tena kutoka kwa watu na pia wakaahidi kutofanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
9Yehoyada akachukua sanduku na kutoboa tundu kwenye kifuniko chake, kisha akaliweka kwenye madhabahu upande wa kulia, mtu anapoingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani waliokuwa katika zamu langoni waliweka fedha zote zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 10Kila walipoona kuwa mna fedha nyingi sandukuni, katibu wa mfalme na kuhani mkuu waliingia na kuhesabu na kuzifunga katika vifurushi fedha zote zilizopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 11Kisha baada ya kuzipima waliwapa wafanyakazi waliosimamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao wakawalipa maseremala na wajenzi, waliorekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu; 12pia waashi na wakata-mawe, zikatumiwa kununulia mbao na mawe yaliyochongwa ili kufanyia marekebisho nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kutimiza mahitaji mengine yote ya marekebisho ya nyumba. 13Lakini pesa hizo hazikutumiwa kwa kulipia utengenezaji wa mabirika ya fedha, mikasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, tarumbeta, wala kwa vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au vya fedha. 14Zote zilitumiwa kwa kuwalipa wafanyakazi waliozitumia kufanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 15Wafanyakazi waliosimamia kazi hii walikuwa waaminifu kabisa, kwa hiyo hapakuwa na haja ya kuwataka watoe hesabu ya matumizi ya fedha hizo. 16Fedha zilizotolewa kuwa sadaka za hatia na sadaka za kuondoa dhambi hazikuingizwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; hizo zilikuwa ni mali ya makuhani.
17Wakati huo Hazaeli mfalme wa Aramu akaushambulia mji wa Gathi na kuuteka. Lakini Hazaeli alipoelekea Yerusalemu ili aushambulie, 18Yoashi mfalme wa Yuda alichukua sadaka zote zilizowekwa wakfu na babu zake wafalme wa Yuda: Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia, na kuongeza zile zake, pamoja na dhahabu yote iliyokuwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika ikulu, akazituma kwa Hazaeli mfalme wa Aramu. Naye Hazaeli akatoka Yerusalemu.
19Matendo mengine yote ya mfalme Yoashi yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.
20Maofisa wake walikula njama dhidi yake, wakamuulia katika nyumba ya Milo kwenye barabara inayoelekea Sila. 21Waliomuua ni Yozakari mwana wa Shimeathi na Yehozabadi mwana wa Shomeri watumishi wake. Halafu walimzika katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi; naye Amazia, mwanawe, akatawala mahali pake.


2Wafalme12;1-21


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.No comments: