Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 9 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 9...Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyo onekana
Mungu wetu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mume wa Wajane,Baba wa Yatima,Jehovah Nissi,Jehovah Jireh,Jehovah Rapha,Jehovah Raah,Jehovah Shammah,Jehovah Shalom,Emanuel-Mungu pamoja nasi...!!

Asante kwa wema na fadhili zako Mungu wetu
Asante kwa ulinzi wako wakati wote Baba wa Mbinguni
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu...
Utukuzwe ee Baba wa Mbinguni,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu mno,Neema yako yatutosha Yahweh..!!!


Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu. Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanauamini ujumbe huu. Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu. Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni. Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo.


Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya Yahweh na kesho ni siku nyingine Jehovah..
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Mungu wetu utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Mfalme wa amani tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Baba wa mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba utupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe kwenye mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa. Nyinyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu. Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, “Mtu yeyote asiyependa kufanya kazi, asile chakula.” Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine. Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe. Lakini nyinyi ndugu, msichoke kutenda mema. Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye, kusudi aone aibu. Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu.
Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama moyoni Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Yahweh ukatuongoze tuingiapo/tutokapo Baba wa Mbinguni tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah ukavifunike kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Baba wa Mbinguni ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu Yahweh ukawe nasi popote tupitapo na ukajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni,Neema/rehema zako ziwe nasi,Upendo ukadumu kati yetu,Ukatuepushe na roho za kiburi,majivuno,kujisifu na yote yanayokwenda kinyume nawe..
Jehovah ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakafifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii, lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu, akamteua avimiliki vitu vyote. Yeye ni mngao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwatakasa binadamu dhambi zao, ameketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu. Mwana ni mkuu kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu kuliko jina lao. Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: “Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa Baba yako.” Wala hakusema juu ya malaika yeyote: “Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu.” Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae, mzaliwa wa kwanza, ulimwenguni alisema: “Malaika wote wa Mungu na wamwabudu.” Lakini kuhusu malaika, alisema: “Amewafanya malaika wake kuwa upepo, na wahudumu wake ndimi za moto.” Lakini kuhusu Mwana, Mungu alisema: “Kiti chako cha enzi, ee Mungu, chadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki. Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako, amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa kuliko wenzako.” Na tena: “Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi. Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma.” Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: “Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.” Malaika ni nini ila roho wanaomtumikia Mungu na ambao hutumwa kuwasaidia wale watakaopokea wokovu?
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wenye shida/tabu,wagonjwa ukawe mponyaji wao,Yahweh tunaomba ukawape chakula wenye njaa,Mungu wetu ukawavushe salama wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Jehovah tunaomba ukawafungue walio katika vifungo vya yule mwovu Mungu wetu ukawatendee walio magerezani pasipo na hatia haki ikatendeke
Jehovah ukafungue matumbo ya wanaotafuta watoto Baba wa Mbinguni tazama wanaohitaji wenza/mke ukawape wanaowafaa
Mungu wetu tunaomba ukafungue milango kwa wanaotafuta kazi Yahweh ukawape ubunifu na maarifa wanaoanza biashara
Yahweh tazama waliokwama kwa sababu ya kukosa ada za masomo
Mungu wetu ukawatendee na kuwabariki wanaowasomesha
Yahweh ukawaongoze watoto wetu katika masomo yao Mungu wetu wakawe kichwa na si mkia Jehovah wakapate kuelewa na kukumbuka yote wanayofundishwa Mungu wetu ukawaongoze katika ujana wao Yahweh ukawe ndani yao nao wakawe ndani yako Baba wa Mbinguni wasiionee haya Injili ya BWANA..
Jehovah ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako nazo ziwaweke huru
Neema na baraka zako ziwe nao Nuru ikaangze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukapokee sala/maombi yetu Jehovah ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Sifa na utukufu ni wako Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Mielele..
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwa nami/kunisoma
Mungu Baba akawabariki na kuwaongoza katika yote
Msipungukiwe katika mahitaji yenu Jehovah akawape kinacho wafaa..
Nawapenda.
Daudi na Mefiboshethi

1Siku moja, Daudi aliuliza, “Je, kuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani.” 2Kulikuwa na mtumishi wa jamaa ya Shauli aliyeitwa Siba. Siba aliitwa kwenda kwa Daudi. Mfalme Daudi alimwuliza, “Je wewe ndiye Siba?” Naye akamjibu, “Naam, mimi mtumishi wako ndiye.” 3Mfalme akamwuliza, “Je, hakuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema wa Mungu.” Siba akamjibu, “Yuko mwana wa Yonathani, lakini yeye amelemaa miguu.” 4Mfalme akamwuliza, “Yuko wapi?” Siba akamjibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari.” 5Basi, mfalme Daudi akatuma watu, naye akaletwa kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari.
6Basi, Mefiboshethi mwana wa Yonathani, na mjukuu wa Shauli akaenda kwa mfalme Daudi, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme Daudi, akasujudu. Daudi akamwita, “Mefiboshethi.” Naye akamjibu, “Naam! Mimi hapa mtumishi wako.”
7Daudi akamwambia, “Usiogope. Mimi nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Ile ardhi yote iliyokuwa ya babu yako Shauli nitakurudishia. Nawe, daima utakula mezani pangu.” 8Mefiboshethi akasujudu, na kusema, “Mimi ni sawa na mbwa mfu; kwa nini unishughulikie hivyo?”
9Kisha, mfalme Daudi akamwita Siba mtumishi wa Shauli, akamwambia, “Ile mali yote iliyokuwa ya Shauli na jamaa yake nimempa mjukuu wa bwana wako. 10Wewe, watoto wako na watumishi wako mtakuwa mnamlimia Mefiboshethi na mtamletea mavuno ili mjukuu wa bwana wako awe daima na chakula. Lakini yeye atakula mezani pangu.” Wakati huo, Siba alikuwa na watoto wa kiume kumi na watano na watumishi ishirini.
11Kisha, Siba akamwambia mfalme, “Mimi mtumishi wako, nitafanya yote kulingana na amri yako.” Basi, Mefiboshethi akawa anapata chakula chake mezani pa Daudi,9:11 mezani pa Daudi: Makala ya Kiebrania: Mezani pangu. kama mmojawapo wa watoto wa mfalme. 12Mefiboshethi alikuwa na mtoto mdogo wa kiume aliyeitwa Mika. Watu wote wa jamaa ya Siba wakawa watumishi wa Mefiboshethi. 13Hivyo, Mefiboshethi aliyekuwa amelemaa miguu yake yote akawa anaishi mjini Yerusalemu, na kupata chakula chake mezani pa mfalme daima.2Samweli9;1-13

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: