Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 14 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 12...
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana...

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu...
Utukuzwe ee Baba wa Mbinguni,Usifiwe Mungu wetu,Uhimidiwe Jehovah,Uabudiwe Yahweh,Neema yako yatutosha Mungu wetu, Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha,Unatosha Yahweh,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,wewe ni alfa na omega...!!

Huu ni ufunuo aliotoa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa awaoneshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe mtumishi wake Yohane mambo hayo. Naye Yohane ameshuhudia yote aliyoyaona kuhusu ujumbe wa Mungu na ushahidi wa Yesu Kristo. Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki chenye maneno ya ujumbe wa kinabii; na heri yao wanaosikia na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati wa mambo haya umekaribia.

Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni
Yahweh tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Mfalme wa amani tunaomba ututakase miili yetu Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...

Mimi Yohane nayaandikia makanisa saba yaliyoko Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi, na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka kwa wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia. Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu, akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina. Tazama! Anakuja na mawingu! Kila mtu atamwona, na hata wale waliomtoboa. Makabila yote duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina. “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu Mwenye Nguvu , aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Jehovah tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji,Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Yahweh tukawe salama moyoni,Baba wa Mbinguni ukatubariki tuingiapo/tutokapo Jehovah ukatuongoze popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni...
Mungu wetu ukatupe macho ya rohoni Yahweh ukatupe masikio ya kusikia sauti yako na kuitii,Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Mungu wetu tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,Neema yako ikawe nasi,amani ikatawale,upendo ukadumu kati yetu,Nuru yako ikaangze katika maisha yetu,ukatuguse na mkono wako wenye nguvu Baba wa Mbinguni na ukatuponye roho na mwili..
Yahweh ukatufanye  chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Mimi ni Yohane, ndugu yenu, ambaye kwa kuungana na Yesu, nashiriki pamoja nanyi mateso na ufalme wake na uvumilivu thabiti. Mimi nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa sababu ya kuhubiri neno la Mungu na kumshuhudia Yesu. Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta. Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yale unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamumu, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea.” Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu, na katikati yake kulikuwa na kitu kama Mwana wa Mtu , naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na mkanda wa dhahabu kifuani. Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba nyeupe, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto; miguu yake kama shaba iliyong'arishwa iliyosafishwa katika tanuri ya moto, na sauti yake ilikuwa kama sauti ya poromoko la maji. Katika mkono wake wa kulia alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling'aa kama jua kali kabisa.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu Yahweh tunaomba ukawaponye Wagonjwa na ukawape nguvu ,uvumili na imani wanaowauguza,Jehovah tunaomba ukawape chakula wenye njaa Yahweh ukabariki mashamba/vyanzo vyao wakapate mazao/chakula cha kutosha kuweka akiba na kusaidia wenye kuhitaji...
Mungu Baba tunaomba ukawavushe salama wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawe tumaini kwa walio kata tamaa,walio kataliwa,wenye hofu na mashaka..
Yahweh tunaomba ukawafariji wafiwa Mungu wetu tunaomba ukawafungue wale walio katika vifungo vya yule mwovu Baba wa Mbinguni tazama walio magerezani pasipo na hatia Mungu wetu tunaomba haki ikatendeke,Yahweh tunaomba ukawasamehe watoto wako waliokwenda kinyume nawe nao wakatambua na kurudi nyumbani mwako Mungu wetu na ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako,wakasimamie neno lako nalo likawaweke huru...

Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho. Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni hai milele na milele. Ninazo funguo za kifo na kuzimu. Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye. Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia na siri ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu, ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni makanisa saba.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse na ukawaponye wale wenye uchungu moyoni,wasioweza kusamehe,waliobeba mizigo,wenye kisasi,walio umizwa/tendwa Yahweh ukatue mizigo yao na ukawape amani moyoni,Mungu wetu neema yako ikawe nao Baba wa Mbinguni Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..Ee Baba tunaomba ukasikie kuomba kwetu Yahweh ukapokee sala/maombi yetu Mungu wetu ukajibu sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele....
Amina..!!

Wapendwa katika Bwana Yesu asanteni sana kwakuwa nami/kunisoma
Baba wa Mbinguni akawaguse kwa mkono wake wenye nguvu,amani ya Kristo Yesu ikawawe nanyi daima..
Nawapenda.

Nathani anamkemea Daudi

1Basi Mwenyezi-Mungu akamtuma nabii Nathani kwa Daudi. Nathani alimwendea Daudi, akamwambia, “Kulikuwa na wanaume wawili katika mji mmoja; mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. 2Yule tajiri alikuwa na kondoo wengi na ng'ombe wengi. 3Lakini yule maskini alikuwa na mwanakondoo mdogo mmoja jike, ambaye alikuwa amemnunua. Alimtunza, naye akakua nyumbani mwake pamoja na watoto wake. Alimlisha mwanakondoo huyo chakula kilekile kama chake na kunywea kikombe chake naye pia alikuwa akimpakata kifuani. Mwanakondoo huyo alikuwa kama binti kwa yule mtu maskini. 4Siku moja, yule tajiri alifikiwa na mgeni. Basi, tajiri huyo hakutaka kuchukua mmoja wa kondoo wake mwenyewe au ng'ombe wake, amchinjie mgeni wake, ila alikwenda na kumnyanganya yule maskini mwanakondoo wake, akamchinjia mgeni wake.” 5Daudi aliposikia hayo, akawaka hasira dhidi ya yule tajiri. Akamwambia nabii Nathani, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai kwamba mtu aliyefanya jambo hilo anastahili kufa! 6Ni lazima amlipe yule maskini mwanakondoo huyo, tena mara nne, kwani ametenda jambo baya na hakuwa na huruma!”
7Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Mimi nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli na kukuokoa mikononi mwa Shauli. 8Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake zake wawe wako, tena nikakupa watu wa Israeli na wa Yuda uwatawale. Na kama haya yangekuwa kidogo mno kwako ningekuongezea mara mbili zaidi ya hayo. 9Kwa nini basi, umedharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu ukafanya uovu huu mbele yangu? Umemuua Uria Mhiti, kwa upanga, ukamchukua mke wake kuwa mkeo. Umewatumia Waamoni kumwua Uria vitani! 10Kwa hiyo basi, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria Mhiti, kuwa mkeo, mauaji hayataondoka katika jamaa yako’. 11Sikiliza, Mwenyezi-Mungu asema, ‘Tazama, nitazusha maafa katika jamaa yako mwenyewe. Nitawachukua wake zako ukiona kwa macho yako mwenyewe na kumpa jirani yako, naye atalala nao hadharani.12:11 hadharani: Au Mbele ya jua hili. 12Wewe ulifanya jambo hilo kwa siri, lakini mimi nitayafanya haya mbele ya Waisraeli wote hadharani.’”
13Basi, Daudi akamwambia Nathani, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu.” Nathani akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amekusamehe dhambi yako, nawe hutakufa. 14Hata hivyo, kwa kuwa kwa tendo lako umemdharau kabisa Mwenyezi-Mungu,12:14 Umemdharau kabisa Mwenyezi-Mungu: Makala ya Kiebrania: Umewadharau sana adui za Mwenyezi-Mungu. mtoto wako atakufa.” 15Kisha Nathani akarudi nyumbani kwake.

Mtoto wa Daudi anakufa

Mwenyezi-Mungu alimpiga mtoto ambaye Bathsheba mkewe Uria alimzalia Daudi, naye akawa mgonjwa. 16Daudi alimwomba Mungu mtoto apate nafuu. Alikwenda chumbani kwake, na usiku kucha akalala sakafuni. 17Wazee waliokuwa wanamwangalia katika jumba hilo walimfuata na kumsihi aamke, lakini yeye alikataa, na hakula chakula chochote pamoja nao. 18Juma moja baadaye, mtoto huyo akafa. Watumishi wa Daudi waliogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwani walifikiri, “Mtoto huyo alipokuwa hai, tulizungumza naye, lakini hakutusikiliza. Sasa, tutamwambiaje kuwa mtoto wake amekufa? Huenda akajidhuru.”
19Daudi alipowaona watumishi wake wananongonezana, akagundua kuwa mtoto wake amekufa. Hivyo, akawauliza, “Je, mtoto amekufa?” Nao wakamjibu, “Naam! Amekufa.” 20Kisha, Daudi aliinuka kutoka sakafuni, akaoga, akajipaka mafuta na kubadilisha mavazi yake. Halafu akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu. Kisha akarudi nyumbani na alipotaka chakula, akapewa, naye akala. 21Ndipo watumishi wake wakamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilofanya? Mtoto alipokuwa hai, wewe ulifunga na kumlilia. Lakini alipokufa, umeinuka, ukala chakula.” 22Daudi akawajibu, “Ni kweli mtoto alipokuwa hai, nilifunga na kulia. Nilifanya hivyo kwani nilifikiri, ‘Nani anajua? Huenda Mwenyezi-Mungu akanirehemu ili mtoto aishi’. 23Lakini sasa amekufa, ya nini nifunge? Je, mimi naweza kumrudisha duniani? Siku moja, nitakwenda huko alikokwenda, lakini yeye hawezi kurudi kwangu.”

Kuzaliwa kwa Solomoni

24Halafu Daudi akamfariji Bathsheba mkewe. Akalala naye, naye akapata mimba na kujifungua mtoto wa kiume, ambaye Daudi alimwita Solomoni. Mwenyezi-Mungu alimpenda mtoto huyo, 25naye akamtuma nabii Nathani kwa Daudi kuwa amwite mtoto huyo Yedidia12:25 Yedidia: Anayependwa na Mwenyezi-Mungu. kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.

Daudi anauteka mji wa Raba

(1Nya 20:1b-3)

26Wakati huo, Yoabu aliushambulia Raba mji wa Waamoni, naye akauteka huo mji wa kifalme. 27Yoabu akatuma ujumbe kwa Daudi, “Nimeushambulia mji wa Raba, nami nimelikamata bwawa lao la maji. 28Sasa wakusanye watu wote waliosalia, upige kambi kuuzunguka na kuuteka. La sivyo, nikiuteka, utaitwa kwa jina langu.” 29Hivyo, Daudi akakusanya watu wote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka mji huo. 30Kisha akachukua taji ya mfalme12:30 mfalme: Au Malkomu. wao kutoka kichwani pake. Uzito wa taji hiyo ya dhahabu ulikuwa kilo thelathini na tano; na ndani yake mlikuwamo jiwe la thamani. Naye Daudi akavikwa taji hiyo kichwani pake. Pia aliteka idadi kubwa sana ya nyara katika mji huo. 31Halafu aliwachukua watu wa mji huo, akawaweka wafanye kazi wakitumia misumeno, sururu za chuma, mashoka ya chuma na kuwatumia kufanya kazi katika tanuri ya matofali; hivyo ndivyo alivyoitenda miji yote ya Waamoni. Hatimaye Daudi na watu wote walirudi Yerusalemu.


2Samweli12;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: