Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 27 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 21...
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa vyote vilivyomo
vinavyoonekana na visivyoonekana,Mungu mwenye nguvu,
Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mume wa wajane,Baba wa Yatima
Muweza wa yote hakuna kama wewe,wewe ni Alfa na Omega...

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Wengi walitamani Baba wa Mbinguni lakini haikuwezekana
Si kwasababu wao ni waovu na si kwamba wao wametenda mabaya sana
zaidi ya sisi uliyetupa nafasi hii/uhai na kuwa wazima mpaka leo hii..
Si kwa uwezo wetu si kwa nguvu zetu si kwamba sisi ni wema sana au
sisi ni wazuri mno sikwamba sisi niwajuaji na tuna akili sana
hapana ni kwa neema/rehema zako ni kwa mapenzi yako Mungu wetu
sisikuwa hivi tulivyo leo hii...
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu.....!!


Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nenda katika ikulu ya mfalme wa Yuda, uwape watu ujumbe huu: Wewe mfalme wa Yuda unayekikalia kiti cha enzi cha mfalme Daudi, pamoja na watumishi wako na watu wako wanaopita katika malango haya, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tendeni mambo ya haki na uadilifu. Mwokoeni mikononi mwa mdhalimu mtu yeyote aliyenyanganywa mali zake. Msiwatendee vibaya au ukatili wageni, yatima na wajane wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia mahali hapa. Kama mkishika neno hili nililowaambia basi, wafalme wanaokikalia kiti cha enzi cha Daudi wataendelea kuingia kwa kupitia malango ya ikulu hii. Watapita pamoja na watumishi wao na watu wao, wakiwa wamepanda farasi na magari ya farasi. Lakini kama hamtatii maneno haya, mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwa nafsi yangu kwamba mahali hapa patakuwa magofu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi kuhusu ikulu ya mfalme wa Yuda: “Ingawa waonekana kuwa mzuri kama nchi ya Gileadi kama kilele cha Lebanoni, Lakini naapa kuwa nitakufanya uwe jangwa, uwe mji usiokaliwa na watu. Nitawatayarisha waangamizi dhidi yako, kila mmoja na silaha yake mkononi. Wataikata mierezi yako mizuri, na kuitumbukiza motoni. “Kisha watu wengi wa mataifa watapita karibu na mji huu, na kila mmoja atamwuliza mwenzake: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameutenda hivi mji huu mkubwa?’ Wenzao watawajibu, ‘Ni kwa sababu waliliacha agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaiabudu miungu mingine na kuitumikia.’”


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akaili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kuwa huru...

Msimlilie mtu aliyekufa, wala msiombolezee kifo chake. Bali mlilieni kwa uchungu yule aendaye mbali, kwa kuwa hatarudi tena kuiona nchi yake. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Shalumu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, aliyetawala baada ya Yosia baba yake, na ambaye aliondoka mahali hapa: “Shalumu hatarudi tena mahali hapa, bali atafia hukohuko walikomchukua utumwani. Kamwe hataiona tena nchi hii.


Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Baba wa Mbinguni nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji...
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu
Mungu wetu tunaomba ukawabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tunaomba 
ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukabariki
vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah ukavitakase na ukavifunike
kwa Damu ya mwanao mpendwa bwana na Mwokozi wetu Yesu kristo
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Jehovah ukaonekane 
popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Tukanene yaliyo yako,tukapate kutambua/kujitambua Mungu wetu tukawe salama moyoni Yahweh tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote
za maisha yetu,Jehovah ukatupe macho ya kuona Yahweh ukatupe masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu amani,furaha,
upendo kati yetu ukadumu....
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe.....
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


“Ole wako Yehoyakimu wewe unayejenga nyumba kwa dhuluma na kuiwekea ghorofa bila kutumia haki. Unawaajiri watu wakutumikie bure wala huwalipi mishahara yao. Wewe wasema: ‘Nitalijenga jumba kubwa, lenye vyumba vikubwa ghorofani.’ Kisha huifanyia madirisha, ukafunika kuta zake kwa mbao za mierezi, na kuipaka rangi nyekundu! Unadhani umekuwa mfalme kwa kushindana kujenga kwa mierezi? Baba yako alikula na kunywa, akatenda mambo ya haki na mema ndipo mambo yake yakamwendea vema. Aliwapatia haki maskini na wahitaji, na mambo yake yakamwendea vema. Hii ndiyo maana ya kunijua mimi Mwenyezi-Mungu. Lakini macho yako wewe na moyo wako, hungangania tu mapato yasiyo halali. Unamwaga damu ya wasio na hatia, na kuwatendea watu dhuluma na ukatili. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: Wakati atakapokufa, hakuna atakayemwombolezea akisema, ‘Ole, kaka yangu!’ ‘Ole, dada yangu!’ Hakuna atakayemlilia akisema, ‘Maskini, bwana wangu!’ ‘Maskini, mfalme wangu!’ Atazikwa bila heshima kama punda, ataburutwa na kutupiliwa mbali, nje ya malango ya Yerusalemu.”

Tazama wenye shida/tabu,Wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,walio kata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka,walio katika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,waliorudinyuma/walioanguka,wenye uchungu moyoni,wanaotafuta watoto,wanaotafuta kazi,wanaotaka kurudi shule,waliokwama kibiashara,walio umizwa rohoni,walio dhulumiwa na wote  wanaokuita/kuhitaji,wanaokutafuta kwa bidii na imani....
 Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Yahweh ukawasamehe na kuwasimamisha tena,Mungu wetu ukabariki
kazi za mikono yao,mashamba yao,masomo yao na ukawape unachoona kinawafaa Baba wa Mbinguni....
Ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako Mungu wetu
Nuru yako ikaangze katika maisha yao,ukaonekane Mungu wetu katika
maisha yao,ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni ukawafute machozi yao
Mungu wetu ukasikie,ukapokee sala/maombi yetu Baba wa Mbinguni ukajibu na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele..
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Mungu wetu akawatendee na kuwabariki katika yote sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Wazawa wa Shauli wanauawa

1Wakati mmoja kulitokea njaa kali nchini Daudi akiwa mfalme. Njaa hiyo ilidumu miaka mitatu mfululizo. Daudi alimwomba Mwenyezi-Mungu shauri. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Shauli na jamaa yake wana hatia ya kumwaga damu kwa sababu aliwaua Wagibeoni.” 2Hivyo, mfalme Daudi akawaita Wagibeoni21:2 Wagibeoni: Makala ya Kiebrania: Wagibeoni na akawaambia. (Wagibeoni hawakuwa Waisraeli ila walikuwa mabaki ya Waamori. Ingawa watu wa Israeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Shauli alijaribu kuwaua wote kwani alikuwa na bidii ya upendeleo kwa watu wa Israeli na wa Yuda). 3Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitalipaje kwa maovu mliyotendewa ili mpate kuibariki nchi hii na watu wake Mwenyezi-Mungu?” 4Wagibeoni wakamwambia, “Kisa chetu na Shauli pamoja na jamaa yake si jambo la fedha au dhahabu. Wala si juu yetu kumwua yeyote katika nchi ya Israeli.” Mfalme akawauliza tena, “Sasa mnasema niwatendee nini?” 5Wao wakamwambia mfalme, “Shauli alikusudia kutuua sisi na kutuangamiza, asiache mtu wetu yeyote katika eneo lote la Israeli. 6Basi, tukabidhi watu saba kati ya wanawe wa kiume, nasi tuwanyonge mbele ya Mwenyezi-Mungu mlimani Gibea, kwa Shauli aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu.” Mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”
7Lakini mfalme alimnusuru Mefiboshethi mwana wa Yonathani kwa sababu ya kiapo ambacho Daudi na Yonathani mwana wa Shauli walikuwa wamekula kati yao kwa jina la Mwenyezi-Mungu. 8Lakini mfalme aliwachukua wana wawili ambao Rispa binti Ahiya alimzalia Shauli, Armoni na Mefiboshethi,21:8 Mefiboshethi: Au Meri-baali. pamoja na watoto wote watano wa kiume wa Mikali, binti Shauli ambao alimzalia Adrieli mwana wa Barzilai Mmeholathi. 9Watoto hao saba wa kiume Daudi aliwakabidhi kwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele ya Mwenyezi-Mungu, wote saba wakafa pamoja. Watoto hao waliuawa mwanzoni mwa mavuno ya shayiri.
10Kisha, Rispa binti Aya alichukua nguo ya gunia, akajitandikia mwambani. Alikaa hapo tangu mwanzo wa mavuno mpaka wakati wa mvua ulipowadia na kuinyeshea maiti. Wakati huo wote, aliwafukuza ndege wa angani na wanyama wa porini, usiku na mchana, ili wasifikie maiti hizo. 11Daudi aliposikia yale aliyofanya Rispa binti Aya, suria wa Shauli, 12alikwenda na kuichukua mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka wakazi wa Yabesh-gileadi, waliokuwa wameiiba kutoka mtaani huko Beth-sheani, ambako Wafilisti walikuwa wamemtundika Shauli na Yonathani siku ile Wafilisti walipomuua Shauli mlimani Gilboa. 13Basi, Daudi akairudisha mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka huko; halafu wakakusanya mifupa ya vijana saba waliotundikwa. 14Basi, watu wa Daudi wakaizika mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Sela katika kaburi la Kishi baba yake Shauli. Walifanya kila kitu ambacho mfalme aliamuru. Baada ya hayo, Mungu akayasikiliza maombi kuhusu nchi yao.

Vita dhidi ya majitu ya Wafilisti

(1Nya 20:4-8)

15Kisha Wafilisti walifanya vita tena na Waisraeli. Naye Daudi na watu wake wakaenda kupigana na Wafilisti. Daudi alichoka sana siku hiyo. 16Ishbi-benobu, mmojawapo wa wazawa wa majitu ambaye mkuki wake wa shaba ulikuwa na uzito wa karibu kilo tatu na nusu na aliyekuwa amejifunga upanga mpya alisema atamuua Daudi. 17Lakini Abishai mwana wa Seruya, alikwenda kumsaidia Daudi. Abishai alimshambulia yule Mfilisti na kumwua. Hivyo, watu wakamwapia Daudi wakisema, “Hutakwenda tena nasi vitani, la sivyo utaizima taa ya ufalme katika Israeli.”
18Baada ya hayo, kulitokea tena mapigano na Wafilisti huko Gobu. Huko Sibekai, Mhushathi, alimuua Safu aliyekuwa mmojawapo wa wazawa wa Warefai. 19Kulitokea tena mapigano na Wafilisti huko Gobu. Naye Elhanani mwana wa Yaareo-regimu, Mbethlehemu, alimuua Goliathi Mgiti, ambaye mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumanguo. 20Baadaye kulitokea tena vita huko Gathi ambako kulikuwa na mtu mmoja alikuwa mkubwa kwa kimo, na mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake vidole ishirini na vinne. Yeye pia alikuwa mzawa wa majitu. 21Alipowadhihaki Waisraeli, Yonathani mwana wa Shimei, nduguye Daudi, alimuua. 22Hao wanne walikuwa wazawa wa majitu huko Gathi, nao waliuawa na Daudi pamoja na watumishi wake.


2Samweli21;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: