Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 12 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 10...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana Tumshukuru katika yote...

Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi tumetenda mema sana,Si kwamba sisi ni wazuri mno,si kwa uwezo wetu wala si kwa nguvu zetu na si kwa akili zetu sisi kuwa hivi tulivyo ni kwa neema/rehema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu....
Utukuzwe ee Mungu wetu,Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu mwenye kuokoa,Mungu mwenye kuponya,Mungu mwenye huruma,Mungu mwenye kusamehe,Mume wa Wajane,Baba wa Yatima,Baba wa Baraka,Baba wa Upendo,Muweza wa yote,Alfa na Omega, Neema yako yatutosha Mungu wetu..!!!


“Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake. Akapatana nao kuwalipa fedha denari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi. Akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.’ Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo. Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, ‘Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?’ Wakamjibu: ‘Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.’ Naye akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ “Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, ‘Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.’ Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja fedha dinari moja. Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja. Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnungunikia yule bwana. Wakasema, ‘Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?’ “Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa dinari moja? Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni.....
Jehovah tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,Kwakunena,Kwakutenda,Kwakujua/Kutojua
Mfalme wa amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote walio tukosea
Yahweh utuepushe katika majaribu Jehovah utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Yesu alipokuwa anakwenda juu Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe. Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa.”
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe sawasawa na mapenzi yako....

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Yahweh tunaomba utubariki tuingiapo/tutokapo,Mungu wetu tukawe salama moyoni Baba wa Mbninguni ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii,Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu,upendo ukadumu kati yetu,furaha na shangwe zikatufuate
Yahweh tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Jehovah ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Yahweh ukatuokoe na kiburi,majivuno,fitina,makwazo,unafiki na vyote vinavyokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni tunaomba neema yako ikawe nasi,Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu...
Yahweh ukatufanye chombo chema Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu. Yesu akamwuliza, “Unataka nini?” Huyo mama akamwambia, “Ahidi kwamba katika ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto.” Yesu akajibu, “Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?” Wakamjibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu.” Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili. Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote; na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu. Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”
Mungu wetu tunarudisha shukrani sifa na utukufu una wewe Baba wa Mbinguni
Yahweh asante kwa uponyaji,Asante kwa baraka zako,neema zako,uwepo wako,Tulikuita Mungu wetu nawe ukaitika,Tulikuomba Baba wa Mbinguni nawe ukatupa kile kinachotufaa,Tulikulilia Yahweh ukafuta machozi yetu
Umekuwa mwema sana Baba wa Mbinguni umetenda mambo makuu juu yetu,Mkono wako wenye nguvu umegusa watoto wako Yahweh umeokoa,umebariki,umefariji,umeleta amani,upendo,furaha Jehovah matendo yako ni makuu mno,matendo yako yanatisha,matendo yako ni ya ajabu hakuna lililogumu mbele zako hakuna linaloshindakana mikononi mwako,ukisema utabariki unabariki ukisema utatenda unatenda....
Mungu si mtu, aseme uongo, wala si binadamu, abadili nia yake! Je, ataahidi kitu na asikifanye, au kusema kitu asikitimize? Tazama, nimepewa amri ya kubariki, naye amebariki wala siwezi kuitangua. Mwenyezi-Mungu hajaona ubaya kwa wana wa Yakobo, wala udhia kwa hao wana wa Israeli. Mwenyezi-Mungu Mungu wao yuko pamoja nao, Yeye husifiwa kwa vifijo miongoni mwao, yeye huzipokea sifa zao za kifalme. Mungu aliyewachukua kutoka Misri, huwapigania kwa nguvu kama za nyati. Hakika ulozi hauwezi kuwapinga watu wa Yakobo, wala uchawi dhidi ya watu wa Israeli. Sasa kuhusu Israeli, watu watasema, ‘Tazameni maajabu aliyotenda Mungu!’

Ee Baba wa Mbinguni hakuna kama wewe..!!

Yahweh tunaomba ukawaguse na wengine wanaokutafuta kwa bidii na imani,Jehovah ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako,Nuru yako ikaangaze katika maisha ya watoto wako wanaokuabudu kwa haki na kweli,Yahweh ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawaongoze na kuwabariki Yahweh ukawatakase na kuwafunika kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo....
Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata. Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” Wakamjibu, “Bwana, tunaomba macho yetu yafumbuliwe.” Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake
Nawapenda. 

Daudi awashinda Waamori na Waashuru

(1Nya 19:1-19)

1Baada ya hayo mfalme Nahashi wa Waamori akafa, na mwanawe aliyeitwa Hanuni akawa mfalme badala ya baba yake. 2Mfalme Daudi akasema, “Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi kama baba yake alivyonitendea.” Hivyo, Daudi alituma wajumbe kumpelekea salamu za rambirambi. Nao wajumbe wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamori, 3wakuu wa Waamori walimwambia bwana wao, Hanuni, “Je, unadhani kwamba Daudi kwa kukutumia watu wa kukufariji anamheshimu baba yako? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kwako ili kuuchunguza na kuupeleleza mji halafu wauteke?”
4Basi, Hanuni aliwachukua wajumbe hao wa Daudi akamnyoa kila mmoja nusu ya ndevu zake, akayapasua mavazi yao katikati mpaka matakoni, kisha akawaacha waende zao. 5Waliona aibu mno kurudi nyumbani. Daudi alipopashwa habari alituma watu kuwalaki kwani hao wajumbe waliona aibu sana. Naye mfalme aliwaambia, “Kaeni mjini Yeriko, hata mtakapoota ndevu, kisha mrudi nyumbani.”
6Waamoni walipoona kuwa wamemchukiza Daudi, walikodi wanajeshi Waaramu 20,000 waendao kwa miguu, kutoka Beth-rehobu na Soba; wanajeshi 12,000, kutoka Tobu, na mfalme Maaka akiwa na wanajeshi 1,000.
7Naye Daudi aliposikia habari hizo, alimtuma Yoabu kwenda na jeshi lote la mashujaa. 8Waamoni walitoka na kujipanga tayari kwa vita kwenye lango la mji wa Raba, mji wao mkuu; nao Waaramu kutoka Soba na Rehobu na watu kutoka Tobu na Maaka walijipanga nyikani.
9Yoabu alipoona kuwa vita ni vikali dhidi yake, mbele na nyuma, aliwateua baadhi ya wanajeshi Waisraeli hodari zaidi akawapanga kukabiliana na Waaramu. 10Wale wanajeshi wengine waliobaki aliwaweka chini ya uongozi wa ndugu yake Abishai, naye akawapanga ili wakabiliane na Waamoni. 11Yoabu akamwambia Abishai, “Ikiwa Waaramu wananizidi nguvu, utanisaidia lakini kama Waamoni wanakuzidi nguvu, nitakuja kukusaidia. 12Lakini jipe moyo! Tupigane kiume kwa ajili ya watu wetu na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye Mwenyezi-Mungu atutendee lile analoona ni jema kwake.”
13Basi, Yoabu na watu wake walisonga mbele kwenda kupigana na Waaramu, nao Waaramu walikimbia. 14Waamoni walipoona kuwa Waaramu wamekimbia, nao pia walimkimbia Abishai na kuingia mjini. Yoabu akaacha kupigana na Waamoni, akarudi Yerusalemu.
15Lakini Waaramu walipoona kwamba wameshindwa na Waisraeli, walijikusanya pamoja. 16Hadadezeri aliagiza Waaramu waliokuwa ngambo ya mto Eufrate waletwe, wapelekwe huko Helamu wakiongozwa na Shobaki kamanda wa jeshi la Hadadezeri. 17Daudi alipopata habari, aliwakusanya pamoja Waisraeli wote, akavuka mto Yordani na kwenda mpaka Helamu. Nao Waaramu walijipanga tayari kwa vita dhidi ya Daudi, wakaanza kupigana naye. 18Lakini Waaramu walikimbia mbele ya Waisraeli. Daudi aliwaua Waaramu 700 waliokuwa madereva wa magari ya vita, wapandafarasi 40,000. Pia alimwumiza Shobaki kamanda wa jeshi lao, naye akafia papo hapo. 19Kisha wafalme wote waliokuwa watumishi wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Waisraeli, walifanya mapatano ya amani na Israeli, nao wakawa watumishi wa Israeli. Hivyo Waaramu hawakuthubutu kuwasaidia Waamoni tena.


2Samweli10;1-19

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: