Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 23 August 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Wimbo Ulio Bora4...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na nyinyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu;
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Mungu ndiye shahidi wangu; yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho kwa sababu tu ya kuwahurumieni. Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; nyinyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Bwana arusi
1Hakika u mzuri ewe mpenzi wangu,
hakika u mzuri!
Macho yako ni kama ya hua
nyuma ya shela lako,
nywele zako ni kama kundi la mbuzi
washukao katika milima ya Gileadi.
2Meno yako ni kama kondoo majike waliokatwa manyoya
wanaoteremka baada ya kuogeshwa.
Kila mmoja amezaa mapacha,
na hakuna yeyote aliyefiwa.
3Midomo yako ni kama utepe mwekundu,
kinywa chako chavutia kweli.
Nyuma ya shela lako,
mashavu yako ni kama nusu mbili za komamanga.
4Shingo yako ni kama mnara wa Daudi,
uliojengwa ili kuhifadhia silaha,4:4 uliojengwa … silaha: Makala katika Kiebrania si dhahiri.
ambako zimetundikwa ngao elfu moja
zote zikiwa za mashujaa.
5Matiti yako ni kama paa mapacha,
ambao huchungwa penye yungiyungi.
6Nitakaa kwenye mlima wa manemane,
na kwenye kilima cha ubani,
hadi hapo kutakapopambazuka,
na giza kutoweka.
7Tazama ulivyo mzuri ee mpenzi wangu,
wewe huna kasoro yoyote.
8Njoo, bibiarusi wangu tuondoke Lebanoni;
na tuiachilie mbali Lebanoni.
Shuka toka kilele cha mlima Amana,
toka kilele cha Seniri na Hermoni,
toka mapango ya simba,
toka milima ya chui.
9Umefurahisha moyo wangu, dada yangu, bi arusi,
umefurahisha moyo wangu,
kwa kunitupia jicho mara moja tu,
na kwa huo mkufu wako shingoni.
10Dada yangu, bi arusi;
pendo lako ni tamu ajabu.
Ni bora kuliko divai,
marashi yako yanukia kuliko viungo vyote.
11Midomo yako yadondosha asali, ee bibiarusi wangu;
ulimi wako una asali na maziwa.
Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ya Lebanoni.
12Dada yangu, naam, bi arusi,
ni bustani iliyofichika,
bustani iliyosetiriwa;
chemchemi iliyotiwa mhuri.
13Machipukizi yako ni bustani ya mikomamanga
pamoja na matunda bora kuliko yote,
hina na nardo.
14Nardo na zafarani, mchai na mdalasini
manemane na udi,
na mimea mingineyo yenye harufu nzuri.
15U chemchemi ya bustani,
kisima cha maji yaliyo hai,
vijito vitiririkavyo kutoka Lebanoni.
Bibi arusi
16Vuma, ewe upepo wa kaskazi,
njoo, ewe upepo wa kusi;
vumeni juu ya bustani yangu,
mlijaze anga kwa manukato yake.
Mpenzi wangu na aje bustanini mwake,
ale matunda yake bora kuliko yote.

Wimbo Ulio Bora4;1-16

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: