Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 8 August 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Mhubiri 5...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana nyinyi ni watoto wake wapenzi. Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Kwa vile nyinyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu. Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mchoyo, (ambao ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Ahidi kwa tahadhari
1 5:1 Kiebrania: Ni 4:17. Uwe mwangalifu uendapo katika nyumba ya Mungu, na kukaribia ili kusikiliza kwa makini kuliko kutambika kama watambikavyo wapumbavu, watu wasiopambanua kati ya jema na ovu. 25:2 Kiebrania: Ni 5:1.Fikiri kabla ya kusema, wala usiwe mwepesi kusema chochote mbele ya Mungu, kwa maana Mungu yuko mbinguni na wewe uko duniani. Kwa hiyo usiseme mengi.
3Kadiri mtu anavyohangaika zaidi, ndivyo atakavyoota ndoto;
sauti ya mpumbavu ni maneno mengi.
4Ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuitimiza; na Mungu hapendezwi na wapumbavu. Tekeleza ulichoahidi. 5Ni afadhali kutoweka nadhiri kuliko kuweka nadhiri kisha usiitimize. 6Angalia mdomo wako usikuingize dhambini, halafu ikupase kumwambia mjumbe wa Mungu kwamba hukunuia kutenda dhambi. Ya nini kumfanya Mungu akukasirikie na kuiharibu kazi yako? 7Ndoto zikizidi, kuna maangamizi na maneno huwa mengi. Jambo la maana ni kumcha Mungu.
Maisha ni bure kabisa
8Usishangae ukiona katika nchi watu fukara wanakandamizwa, wananyimwa haki zao na maslahi yao. Kila mwenye cheo anayewadhulumu wanyonge yupo chini ya mkuu mwingine, na juu ya hao wote kuna wakuu zaidi. 9Hata hivyo, mfalme akijishughulisha na kilimo ni manufaa kwa wananchi wote.
10Apendaye fedha hatatosheka na fedha; wala atamaniye mali hata akiipata hatatosheka. Hilo nalo ni bure kabisa. 11Ongezeko la mali huleta ongezeko la walaji, naye mwenye mali yamfaa nini isipokuwa kuitazama tu mali yake? 12Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe ameshiba au amekula kidogo tu. Lakini usingizi wa tajiri ni wa wasiwasi daima, maana ziada ya mali yake humsumbua usiku kucha.
13Tena, nimeona jambo moja ovu sana duniani: Mtu alijirundikia mali ikawa hatari kwake. 14Kwa bahati mbaya, mali hiyo iliharibiwa katika matumizi mabaya, mwisho, mtu huyo hakuwa na chochote mkononi na alikuwa na mwana. 15Kama vile binadamu alivyokuja duniani uchi toka tumboni mwa mama yake, ndivyo atakavyorudi uchi huko alikotoka. Hataweza kuchukua hata sehemu ndogo ya mapato ya kazi yake. 16Hili nalo ni jambo baya sana. Atarudi kama alivyokuja. Amejisumbua kufukuza upepo, akatoka jasho bure. 17Aliishi maisha yake yote katika giza na huzuni; katika mahangaiko, magonjwa na hasira.
18Basi, haya ndiyo niliyogundua: Jambo zuri na la kufaa kwa binadamu ni kula, kunywa na kufurahia matunda ya jasho analotoa katika kazi anayoifanya hapa duniani, siku hizo chache za maisha aliyojaliwa na Mungu, maana hivyo ndivyo alivyopangiwa. 19Kama Mungu anampa mtu utajiri na mali na kumjalia fursa ya kufurahia hayo, basi binadamu ashukuru na avifaidi hivyo alivyojipatia kwa jasho lake. Hiyo ni zawadi kutoka kwa Mungu. 20Na kwa kuwa Mungu amemruhusu kuwa na furaha, binadamu hatakuwa na wasiwasi mwingi juu ya maisha yake mafupi.


Mhubiri5;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: