Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 10 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 24...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Alfa na Omega,Muweza wa yote hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni,
Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu..!
Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Unastahili
Kuhimidiwa,Unastahili ee Mungu wetu,Unatosha Mfalme wa Amani..!
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Sifa na Utukufu ni kwako ee Mungu wetu..

Tunakuja mbele zako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
tulizozifanya kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea...
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu nguvu za mpinga Kristo
zishindwe katika jina lililokuu jina la Bwana wetu Yesu Kristo..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba
utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaoneshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde. “Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.” Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona, nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionesha mambo hayo, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!” Tena akaniambia, “Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia. Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.” “Sikiliza!” Asema Yesu, “Naja upesi pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake. Mimi ni Alfa na Omega, wa kwanza na wa mwisho, mwanzo na mwisho.” Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, wapate kuwa na haki ya kula tunda la mti wa uhai, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake. Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji. “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!” Roho na Bibi arusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Aliye na kiu na aje; anayependa, na achukue maji ya uhai bila malipo.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh ukatupe ubunifu,maarifa katika kufanya/kutenda
na tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitahiji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe
sawasawa na mapenzi yako..



Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo. Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu. Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote. Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote. Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu. Msimpinge Roho Mtakatifu; msidharau unabii. Pimeni kila kitu: Zingatieni kilicho chema, na kuepuka kila aina ya uovu. Mungu mwenyewe anayetupatia amani awatakase nyinyi kabisa kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu – roho, mioyo na miili yenu – mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye anayewaita nyinyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu. Ndugu, tuombeeni na sisi pia. Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo. Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii. Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na
wote wanaotuzunguka,Mungu wetu tunaomba baraka zako,
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na vyote tunavyovimiliki..
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh maisha
yetu tunayaweka mikononi mwako,Mungu wetu ukatupe neema
ya kusimamia Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



“Nyinyi ni chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu. “Nyinyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Tazama wenye shida/tabu Mungu wetu,wagonjwa,wenye njaa,wanaotaabika na kuelemewa na mizigo,Mungu wetu walio kata tamaa,Yahweh waliokataliwa ,walio katika vifungo mbalimbali,
wanyonge,waliodhurumiwa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,
waliopotea/kuasi,walioanguka na wote wasiyo ijua kweli..
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu.
Yahweh tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia..
Jehovah tunaomba ukawape neema ya kukujua wewe na kufuata
njia zako,Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea na kusimama
tena,Baba ukawape macho ya rohoni na masikio ya kusikia sauti yako..
Mungu wetu ukawasamehee pale walipokwenda kinyume nawe..
Yahweh ukabariki maisha yao na Nuru yako ikaangaze..
Mungu wetu ukawape maarifa/ubunifu katika utendaji wao
Ukabariki mashamba yao na wakapate mavuno ya kutosha
na kuweka akiba,Yahweh ukaonekane katika maisha yao..
Mungu wetu ukawafungue na kuwawekahuru,Yahweh ukawatendee
sawa sawa na mapenzi yako,Wafiwa ukawe mfariji wao..
Ee baba ukasikie kuomba kwetu na ukapokee sala/maombi yetu.
Tukiamini na kukushuru daima Mungu wetu..




Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza. “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anapenda kumfunulia. Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina.

wapendwa katika Bwana asanteni sana kwakuwa nami..
Baba wa huruma,upendo na amani akawatendee
kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.

Waisraeli wanaamua kumtumikia Mwenyezi-Mungu

1Kisha Yoshua akayakusanya makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maofisa wa Israeli, nao wakaja mbele ya Mungu. 2Taz Mwa 11:27 Yoshua akawaambia watu wote, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Hapo zamani, wazee wenu waliishi ngambo ya mto Eufrate, wakaitumikia miungu mingine. Mzee mmoja alikuwa Tera, baba yao Abrahamu na Nahori. 3Taz Mwa 12:1-9; 21:1-3 Mimi Mungu nilimwondoa babu yenu Abrahamu kutoka huko ngambo ya mto Eufrate na kumleta hapa Kanaani, ambako nilimpatia wazawa wengi. Nilimpa Isaka, 4Taz Mwa 25:24-26; 36:8; 46:1-7; Kumb 2:5 naye Isaka nikampa Yakobo na Esau. Nilimpa Esau milima ya Seiri aimiliki. Lakini Yakobo na watoto wake walikwenda Misri. 5Taz Kut 3:1–12:42 Baadaye niliwatuma Mose na Aroni, nikailetea nchi ya Misri mapigo, na baadaye nikawatoa nyinyi nchini humo. 6Taz Kut 14:1-31 Niliwatoa wazee wenu kutoka Misri na kuwaleta hadi kwenye bahari ya Shamu. Wamisri waliwafuatia wakiwa na magari na askari wapandafarasi. 7Waisraeli waliponililia mimi Mwenyezi-Mungu, niliweka giza kati yao na Wamisri na kuifanya bahari iwafunike Wamisri. Nyinyi wenyewe mlijionea yale niliyowatendea Wamisri. Mliishi jangwani muda mrefu. 8Taz Hes 21:21-35 Kisha niliwaongoza hadi katika nchi ya Waamori ambao waliishi upande mwingine wa mto Yordani. Walipigana nanyi, lakini mimi niliwapeni ushindi juu yao mkawaangamiza na kuiteka nchi yao. 9Taz Hes 22-24 Naye Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akaja na kuwashambulia Waisraeli. Akamwalika Balaamu mwana wa Beori aje kuwalaani nyinyi. 10Lakini mimi sikumsikiliza Balaamu, naye ikambidi kuwabariki, nami nikawaokoa nyinyi mikononi mwa Balaki. 11Taz Yosh 3:14-17; 6:1-21 Halafu mkavuka mto Yordani, mkafika Yeriko. Wakazi wa Yeriko walipigana nanyi, hali kadhalika na Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi. Hao mimi nikawatia mikononi mwenu. 12Taz Kut 23:28; Kumb 7:20 Nilituma manyigu mbele yenu ambayo yaliwatimua wafalme wawili wa Waamori. Hamkufanya haya kwa kupania mapanga wala pinde zenu.
13 Taz Kumb 6:10-11 “Niliwapeni mashamba ambayo hamkuwa mmeyalima, na miji ambayo hamkuijenga ambamo sasa mnaishi, na kula matunda ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuipanda.
14“Sasa, basi, mcheni Mwenyezi-Mungu na kumtumikia kwa moyo mnyofu na uaminifu. Acheni kabisa miungu ile ambayo wazee wenu waliiabudu ngambo ya mto Eufrate na nchini Misri. Mtumikieni Mwenyezi-Mungu. 15Kama hamtaki kumtumikia Mwenyezi-Mungu, basi chagueni leo hii ni nani mtakayemtumikia: Kwamba ni miungu ile ambayo wazee wenu waliitumikia ngambo ya mto Eufrate, au miungu ya Waamori ambao sasa mnaishi nchini mwao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu.”
16Hapo watu wakamjibu, “Hatutaweza kamwe kumwacha Mwenyezi-Mungu na kuitumikia miungu mingine. 17Maana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ndiye aliyetutoa sisi pamoja na wazee wetu katika nchi ya Misri tulikokuwa watumwa, tukayaona kwa macho yetu wenyewe matendo ya ajabu aliyotenda. Akatulinda katika safari zetu zote na miongoni mwa watu wote ambao tulipita kati yao.
18“Mwenyezi-Mungu alituondolea watu wote yaani Waamori wote waliokaa nchini. Kwa hiyo, nasi tutamtumikia Mwenyezi-Mungu, maana ndiye Mungu wetu.”
19Lakini Yoshua akawaambia, “Nyinyi hamwezi kumtumikia Mwenyezi-Mungu, maana yeye ni Mungu Mtakatifu. Yeye ni Mungu mwenye wivu, naye hatawasamehe makosa na dhambi zenu. 20Mkimwacha Mwenyezi-Mungu na kuitumikia miungu ya kigeni, atawaadhibu na kuwaangamiza kabisa, hata ingawa amewatendea mema haya yote.” 21Nao watu wakamwambia Yoshua, “La, hasha! Sisi tutamtumikia Mwenyezi-Mungu tu.” 22Hapo Yoshua akawaambia, “Nyinyi wenyewe ni mashahidi wa nafsi zenu kwamba mmechagua kumtumikia Mwenyezi-Mungu.” Nao wakamjibu, “Sisi tu mashahidi.” 23Naye akawaambia, “Basi, ondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mkamfuate Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wenu wote.” 24Nao, wakasema, “Tutamtumikia na kumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.” 25Hivyo, Yoshua akafanya agano na Waisraeli huko Shekemu, akawapa masharti na maagizo ya kufuata. 26Yoshua akayaandika haya yote katika kitabu cha sheria ya Mungu; kisha, akachukua jiwe kubwa na kulisimika chini ya mwaloni katika hema ya Mwenyezi-Mungu. 27Halafu akawaambia watu wote, “Jiwe hili ndilo litakalokuwa shahidi kwetu, maana limesikia maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu ametuambia. Kwa hiyo, litashuhudia dhidi yenu, ili msije mkamkana Mungu wenu.” 28Halafu Yoshua akawaruhusu watu waondoke; nao wakaenda kila mmoja kwake.

Kifo cha Yoshua

29Baada ya mambo hayo, Yoshua, mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, akafariki akiwa na umri wa miaka 110. 30Taz Yosh 19:49-50 Nao wakamzika kwenye eneo ambalo alikuwa amegawiwa kuwa sehemu yake, huko Timnath-sera, katika milima ya Efraimu, kaskazini ya mlima wa Gaashi.
31Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu muda wote wa uhai wa Yoshua, na baada ya kifo chake, waliendelea kumtumikia kwa muda walioishi wale wazee waliokuwa wameona kwa macho yao mambo yale Mwenyezi-Mungu aliyowatendea Waisraeli.
32 Taz Mwa 33:19; 50:24-25; Kut 13:19 Yoh 4:5; Mate 7:16 Mifupa ya Yosefu ambayo Waisraeli walikuwa wameileta kutoka Misri waliizika huko Shekemu katika eneo ambalo Yakobo alikuwa amelinunua kutoka kwa wana wa Hamori, baba yake Shekemu, kwa vipande 100 vya fedha. Ardhi hii nayo ikawa mali yao wazawa wa Yosefu.
33Naye Eleazari, mwana wa Aroni, akafariki na kuzikwa Gibea, mji ambao alikuwa amepewa mwanawe Finehasi katika nchi ya milima ya Efraimu.


Yoshua 24;1-33

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: