Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 13 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Tumemaliza kitabu cha Yoshua na Leo Tunaanza Kitabu cha Waamuzi 1...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Wapendwa/Waungwana tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha
kumaliza kupitia/kusoma kitabu cha "YOSHUA"
Natumaini tumejifunza na kuongeza kitu...
Leo tunaanza kitabu cha "WAAMUZI"Tunaomba Mungu akatuongoze
vyema katika kusoma na tukaelewe na kufuata yaliyomo na tukasimamie
Neno lake na likawe msaada kwetu na kwa  wengine..
Ee Mungu tusaidie tukawe na kiu/shauku ya kusoma zaidi na kuzingatia


Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli ambayo wewe umeyafuata. Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uhai katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja. Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa. Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini. Wape maagizo hayo na mafundisho hayo. Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: Katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi. Tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani Maandiko Matakatifu, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. Usiache kukitumia kile kipaji cha Kristo ndani yako ulichopewa kwa maneno ya manabii na kwa kuwekewa mikono na wazee. Fikiri kwa makini juu ya hayo yote na kuyatekeleza kusudi maendeleo yako yaonekane na wote. Angalia sana mambo yako mwenyewe na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo, maana ukifanya hivyo, utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.
Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana tunamshukuru
katika yote...
Asante Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu
Nchi na vyote vilivyomo,vinavyoonekana na visivyoonekana..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu wa wote walio hai..
Muweza wa yote,Baba wa upendo,Mungu wenye huruma,Mponyaji
Jehovah Jireh,Jehovah Nissi,Jehovah Rapha,Jehovah Raah,Jehovah Shammah,Jehovah Shalom,Emanueli-Mungu pamoja nasi..
Unastahili Sifa,Unastahili kutukuzwa,Unastahili kuabudiwa,
Unastahili kuhimidiwa,Unastahili ee Baba...!Unatosha Mungu wetu..



Basi, ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, ameketi upande wa kulia wa Mungu. Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani. Maana nyinyi mmekufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Uhai wenu halisi ni Kristo, na wakati atakapotokea ndipo nanyi pia mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
Asante kwa kwa ulinzi wako wakati wote Mungu wetu..
Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari katika majukumu yetu..

Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Mungu wetu
tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti,Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Baba ukatupe
ubunifu,maarifa katika kufanya/kutenda nasi tukatende sawasawa
na mapenzi yako,Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo,Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya
kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu,Jehovah ukatupe
sawasawa na mapenzi yako...



Basi, ueni chochote kilicho ndani yenu ambacho ni cha kidunia: Uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu). Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi. Wakati mmoja nyinyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo. Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: Hasira, tamaa na uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwani nyinyi mmekwisha vua ule utu wa kale pamoja na matendo yake yote, mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu. Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote. Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo, kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili. Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo nyinyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani! Ujumbe wa Kristo na ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani. Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote
wanaotuzunguka,Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Baba tunaomba ukatubariki na ukatupe neema ya kusimamia
Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo. Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, upendo, subira na unyenyekevu. Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uhai wa milele uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi. Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato, nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo. Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana. Yeye peke yake anaishi milele katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina. Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie. Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao. Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uhai ambao ni uhai wa kweli. Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa. Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile wanachokiita watu wengine “Elimu.” Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo yake wamepoteza imani. Nawatakieni nyote neema!

Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wagonjwa,ukawape uponyaji,wenye njaa ukawape chakula
na ukabariki mashamba yao wakapate mavuno mengi na
wakawe na akiba,waliokatika magumu/majaribu Baba wa
Mbinguni tunaomba ukawavushe salama,waliokatika vifungo
mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawafungue na ukawape
wote neema ya kujiombea,kufuata njia zako ukawaweke huru
na Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Wafiwa ukawe mfariji wao..
Kwa imani tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu Hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na Upendo wa Kristo
Amani na furaha iwe nanyi Daima..
Nawapenda.



Waisraeli baada ya kifo cha Yoshua

1Baada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli walimwuliza Mwenyezi-Mungu: “Mwenyezi-Mungu, ni kabila gani litakwenda kupigana kwanza na Wakanaani?” 2Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Kabila la Yuda litakwenda kupigana nao kwanza, maana nimeitia nchi hiyo mikononi mwao.” 3Watu wa kabila la Yuda wakawaambia ndugu zao, watu wa kabila la Simeoni, “Shirikianeni nasi tunapokwenda kuitwaa nchi hiyo ambayo tumepewa. Nasi, pia tutashirikiana nanyi kwenda kuitwaa nchi mtakayopewa.” Hivyo kabila la Simeoni likakubali kushirikiana nao. 4Basi, watu wa kabila la Yuda wakaenda kufanya mashambulio, naye Mwenyezi-Mungu akawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, wakawaua watu 10,000 katika vita huko Bezeki. 5Katika mji huo walimkuta mfalme Adoni-bezeki, wakapigana naye na kuwashinda Wakanaani na Waperizi. 6Adoni-bezeki akakimbia, lakini walimfuatia, wakamkamata, wakamkata vidole gumba vya mikono na miguu. 7Adoni-bezeki akasema, “Wafalme sabini waliokatwa vidole gumba vya mikono na miguu waliokota makombo chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa kama nilivyotenda.” Wakampeleka Yerusalemu, akafia huko.
8Watu wa kabila la Yuda waliushambulia mji wa Yerusalemu na kuuteka. Waliwaua wakazi wake kwa mapanga na kuuteketeza mji kwa moto. 9Baadaye, watu wa kabila la Yuda walikwenda kupigana na Wakanaani walioishi kwenye nchi ya milima, Negebu na kwenye nchi tambarare. 10Waliwashambulia pia Wakanaani walioishi katika mji wa Hebroni ambao hapo awali uliitwa Kiriath-arba, wakashinda makabila ya Sheshai, Himani na Talmai.
11Kutoka huko watu wa kabila la Yuda walikwenda kuushambulia mji wa Debiri; ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi. 12Kalebu akatangaza: “Mtu yeyote atakayefaulu kuuteka mji wa Kiriath-seferi, nitamwoza binti yangu Aksa.” 13Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi na mdogo wake Kalebu, akauteka, naye Kalebu akamtoa bintiye Aksa aolewe na Othnieli. 14Aksa alipowasili kwa Othnieli, akamwambia Othnieli amwombe Kalebu baba yake shamba. Aksa alikuwa amepanda punda na aliposhuka chini baba yake alimwuliza, “Ungependa nikupe nini?” 15Akamjibu, “Nipe zawadi! Naomba unipe chemchemi za maji kwani eneo ulilonipa huko Negebu ni kavu.” Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
16Wazawa wa Keni ambaye alikuwa baba mkwe wa Mose, walifuatana na watu wa kabila la Yuda kutoka Mji wa Mitende yaani mji wa Yeriko, mpaka jangwa la Yuda karibu na Aradi, wakafanya makao yao huko pamoja na watu wa Yuda.1:16 watu wa Yuda: Pengine Waamaleki. 17Watu wa kabila la Yuda walishirikiana na ndugu zao, watu wa kabila la Simeoni, wakawashinda Wakanaani waliokaa Sefathi. Waliuangamiza kabisa mji huo na kugeuza jina lake kuwa Horma.1:17 Horma: Jina hili katika Kiebrania linamaanisha “maangamizi”. 18Watu wa kabila la Yuda pia waliteka miji ya Gaza na eneo lake, Ashkeloni na eneo lake, na Ekroni na eneo lake. 19Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na watu wa kabila la Yuda, nao wakaiteka nchi ya milima. Lakini hawakuweza kuwashinda wenyeji wa nchi tambarare kwa sababu magari yao ya vita yalikuwa ya chuma. 20Mji wa Hebroni ukakabidhiwa kwa Kalebu kufuatana na maagizo ya Mose. Kalebu akazifukuza kutoka huko koo tatu za Anaki. 21Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mjini Yerusalemu; ndiyo maana Wayebusi wanakaa pamoja na watu wa kabila la Benyamini mjini Yerusalemu mpaka leo.
22Watu wa makabila ya Yosefu waliushambulia mji wa Betheli, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja nao. 23Kwanza walikuwa wamewatuma wapelelezi kwenda kuupeleleza mji wa Betheli. Mji huo hapo awali uliitwa Luzu. 24Wapelelezi hao walimwona mtu mmoja akitoka mjini, wakamwambia, “Tafadhali, tuoneshe njia inayoingia mjini, nasi tutakutendea kwa wema.” 25Akawaonesha njia ya kuingia mjini. Basi, wakaingia na kuangamiza kila mtu aliyekuwamo. Lakini wakamwacha salama mtu huyo na jamaa yake. 26Mtu huyo akahamia nchi ya Wahiti, huko akajenga mji ambao aliuita Luzu; na mji huo unaitwa hivyo mpaka leo.
27Watu wa kabila la Manase hawakuwafukuza wakazi wa miji ya Beth-sheani na vijiji vyake, Taanaki na vijiji vyake, Dori na vijiji vyake, Ibleamu na vijiji vyake, na Megido pamoja na vijiji vyake. Wakanaani waliendelea kukaa huko. 28Hata Waisraeli walipokuwa na nguvu hawakuwafukuza Wakanaani bali waliwapa kazi za kulazimishwa.
29Watu wa kabila la Efraimu hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Gezeri, na hawa waliishi huko pamoja na watu wa Efraimu.
30Watu wa kabila la Zebuluni hawakuwafukuza wakazi wa mji wa Kitroni, wala wale wa mji wa Nahalali, waliendelea kukaa pamoja nao wakiwafanyiza kazi za kulazimishwa.
31Watu wa kabila la Asheri hawakuwafukuza wakazi wa miji ya Ako, Sidoni, Alabu, Akzibu, Helba, Afeka na Rehobu. 32Watu wa kabila la Asheri walikaa pamoja na Wakanaani wenyeji wa nchi hiyo kwani hawakuwafukuza.
33Watu wa kabila la Naftali hawakuwafukuza wakazi wa mji wa Beth-shemeshi au wakazi wa Beth-anathi, lakini walikaa pamoja nao. Hata hivyo wenyeji wa miji hiyo, walilazimishwa kuwafanyia Waisraeli kazi za kulazimishwa.
34Waamori waliwafukuzia watu wa kabila la Dani milimani. Hawakuwaruhusu kuja kuishi katika nchi tambarare. 35Waamori waliendelea kuishi katika miji iliyokuwa katika kilima cha Heresi, Aiyaloni na Shaalbimu. Lakini watu wa makabila ya Manase na Efraimu waliwatawala Waamori na kuwafanya wafanye kazi za kulazimishwa. 36Mpaka wa Waamori ulikuwa kaskazini ya Sela, kupitia pitio la Akarimu.


Waamuzi 1;1-36

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: