Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 29 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 13...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo.
Wewe si Mungu wa wafu bali ni Mungu wa walio hai,Mungu wa majeshi
Mungu mwokozi,si Mungu wa fujo ni Mungu wa amani..
Unatosha Baba wa Mbinguni,Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako
ni ya ajabu,hakuna kama wewe,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho..!



Ee Mungu, sisi tumesikia kwa masikio yetu, wazee wetu wametusimulia mambo uliyotenda nyakati zao, naam, mambo uliyotenda hapo kale: Kwa mkono wako mwenyewe uliyafukuza mataifa mengine, na mahali pao ukawakalisha watu wako; uliyaadhibu mataifa mengine, na kuwafanikisha watu wako. Watu wako hawakuitwaa nchi kwa silaha zao, wala hawakupata ushindi kwa nguvu zao; ila uliwasalimisha kwa mkono wako mwenyewe, kwa kuwaangazia uso wako, kwani wewe uliwapenda. Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu! Wawajalia ushindi wazawa wa Yakobo. Kwa nguvu yako twawashinda maadui zetu, kwa jina lako twawakanyaga wanaotushambulia. Mimi siutegemei upinde wangu, wala upanga wangu hauwezi kuniokoa. Wewe ndiwe uliyetuokoa na maadui zetu; uliwavuruga wale waliotuchukia. Daima tutaona fahari juu yako, ee Mungu; tutakutolea shukrani milele.

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..
Asante kwa ulinzi wako kwetu..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..



Ole wenye majivuno na walevi wa Efraimu, fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka! Naam, fahari iliyotawala bondeni kwenye rutubarutuba; na vichwani kwao walio watu walevi kupindukia! Bwana amejichagulia mtu wake shujaa na mwenye nguvu, ambaye ni kama mvua ya mawe na dhoruba kali, kama tufani ya mafuriko makubwa; kwa mkono wake atawatupa chini ardhini. Majivuno na fahari ya walevi wa Efraimu yatakanyagwakanyagwa ardhini, fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka; fahari iliyotawala bondeni kwenye rutuba itakuwa kama tini za mwanzo kabla ya kiangazi; mtu akiziona huzichuma na kuzila mara moja. Siku ile Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuwa taji tukufu, kama kilemba kizuri kwa watu wake watakaobaki hai. Waamuzi mahakamani atawaongoza kutenda haki, nao walinzi wa mji atawapa nguvu.
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Lakini wako wengine waliolewa divai na kuyumbayumba kwa sababu ya pombe; naam, makuhani na manabii wamelewa mvinyo, wamevurugika kwa divai. Wanayumbayumba kwa pombe kali; maono yao yamepotoka, wanapepesuka katika kutoa hukumu. Meza zote zimetapakaa matapishi, hakuna mahali popote palipo safi. Wao wananidhihaki na kuuliza: “Huyu nabii ataka kumfundisha nani? Je, anadhani atatueleza sisi ujumbe wake? Je, sisi ni watoto wachanga walioachishwa kunyonya juzijuzi? Anatufundisha kama watoto wadogo: Sheria baada ya sheria, mstari baada ya mstari; mara hiki, mara kile!” Haya basi! Mwenyezi-Mungu ataongea na watu hawa kwa njia ya watu wa lugha tofauti wanaoongea lugha ngeni. Hata hivyo yeye alikuwa amewaahidi: “Nitawaonesheni pumziko, nitawapeni pumziko enyi mliochoka. Hapa ni mahali pa pumziko.” Lakini wao hawakutaka kunisikiliza. Kwa hiyo kwao neno la Mwenyezi-Mungu litakuwa tu: Sheria sheria, mstari mstari; mara hiki, mara kile! Nao watalazimika kukimbia lakini wataanguka nyuma; watavunjika, watanaswa na kutekwa.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu..
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe
sawasawa na mapenzi yako...


Basi, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wenye madharau mnaotawala watu wa Yerusalemu, “Nyinyi mnajidai mmefanya mkataba na kifo, mmefanya mapatano na Kuzimu! Nyinyi mwasema eti balaa lijapo halitawapata, kwa sababu mmefanya uongo kuwa tegemeo lenu, na udanganyifu kuwa kinga yenu!” Basi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu: “Tazama! Naweka mjini Siyoni jiwe la msingi, jiwe ambalo limethibitika. Jiwe la pembeni, la thamani, jiwe ambalo ni la msingi thabiti; jiwe lililo na maandishi haya: ‘Anayeamini hatatishika.’ Nitatumia haki kama kipimo changu, nitatumia uadilifu kupimia.” Mvua ya mawe itaufagilia mbali uongo mnaoutegemea, na mafuriko yataharibu kinga yenu. Hapo mkataba wenu na kifo utabatilishwa, na mapatano yenu na Kuzimu yatafutwa. Janga lile kuu litakapokuja litawaangusheni chini. Kila litakapopitia kwenu litawakumba; nalo litapita kila asubuhi, mchana na usiku. Kusikia ujumbe huu tu kutakuwa kitisho. Kwenu itakuwa kama ajinyoshaye juu ya kitanda kifupi mno, au kujifunika kwa blanketi lililo dogo mno! Maana Mwenyezi-Mungu atainuka kama kule mlimani Perazimu; atawaka hasira kama kule bondeni Gibeoni. Atatekeleza mpango wake wa ajabu; atatenda kazi yake ya kustaajabisha. Basi, nyinyi msiwe na madharau vifungo vyenu visije vikakazwa zaidi. Maana nimesikia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameazimia kuiangamiza nchi yote.

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako

Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu ukatuepushe na roho za 
dharau,masengenyo,kuumizana,kukwazana,kiburi na vyote vinavyokwenda kinyume nawe..
Jehovah ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie
Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Tegeni sikio msikilize ninayowaambieni; sikilizeni kwa makini hotuba yangu. Je, alimaye ili kupanda hulima tu? Je, huendelea kulima na kusawazisha shamba lake? La! Akisha lisawazisha shamba lake, hupanda mbegu za bizari na jira, akapanda ngano na shayiri katika safu, na mipakani mwa shamba mimea mingineyo. Mtu huyo huwa anajua la kufanya, kwa sababu Mungu wake humfundisha. Bizari haipurwi kwa mtarimbo wala jira kwa gari la ng'ombe! Ila bizari hupurwa kwa kijiti na jira kwa fimbo. Mkulima apurapo ngano yake, haendelei kuipura mpaka kuvunja punje zake. Anajua jinsi ya kuipura kwa gurudumu, bila kuziharibu punje za ngano. Ujuzi huu nao watoka kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mipango yake Mungu ni ya ajabu, hekima yake ni kamilifu kabisa.

Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia
magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya yule mwovu
waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka na wote
walioanguka/potea Mungu wetu tunaomba ukawaguse na mkono wako
wenye nguvu,Yahweh tunaomba ukawaponye kiroho na kimwili pia
Mungu wetu ukawavushe salama,Baba ukawaokoe na kuwasimamisha tena,Yahweh ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawafunike kwa Damu ya Mwokozi wetu Yesu Kristo
Baba ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na Nuru ikaangaze
katika maisha yao..
Mungu wetu tunaomba upokee sala/maombi yetu..
Ee Baba tunayaweka haya yote mikononi mwako,kwa imani
tunashukuru na kukusifu daima..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Nawapenda.


Kuzaliwa kwa Samsoni

1Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye akawaacha watawaliwe na Wafilisti kwa miaka arubaini.
2Kulikuwa na mtu mmoja huko Sora, wa kabila la Dani, jina lake Manoa. Mke wake alikuwa tasa. 3Siku moja, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea huyo mwanamke, akamwambia, “Wewe ni tasa, huna watoto. Lakini utapata mimba na kumzaa mtoto wa kiume. 4Kwa hiyo uwe mwangalifu, usinywe divai au kileo wala usile kitu chochote kilicho najisi, 5kwa maana utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Nywele za mtoto huyo kamwe zisinyolewe, maana atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake.13:5 Masharti na majukumu yanayotajwa hapa (taz 4-5) kwa kawaida yahusu mtu aliyewekwa wakfu kwa Mungu kwa nadhiri fulani (taz Hes 6:1-8). Naye ataanza kuwakomboa Waisraeli mikononi mwa Wafilisti.” 6Mwanamke huyo akaenda kumwambia mume wake, “Mtu wa Mungu ambaye sura yake ilikuwa kama ya malaika wa Mungu alinijia. Sikumwuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake. 7Lakini aliniambia kwamba nitachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Aliniamuru nisinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi, maana mtoto huyo atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake mpaka atakapokufa.”
8Kisha Manoa akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Nakuomba ee Mwenyezi-Mungu, umtume tena yule mtu wako uliyemtuma ili atufundishe mambo tunayopaswa kumtendea huyo mtoto atakayezaliwa.” 9Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi la Manoa, na yule malaika wa Mungu akamwendea tena yule mwanamke alipokuwa ameketi shambani. Lakini mumewe, Manoa, hakuwa pamoja naye. 10Mwanamke akakimbia upesi, akamwambia mumewe, “Tazama! Yule mtu aliyenijia siku ile amenitokea tena.” 11Manoa akafuatana naye mpaka kwa mtu huyo, akamwuliza, “Je, wewe ni yule mtu aliyezungumza na mwanamke huyu?” Yule mtu akamjibu, “Ni mimi.” 12Kisha Manoa akasema, “Sasa maneno yako yatakapotimia ni mambo gani tutakayofuata kwa ajili ya huyo mtoto? Tutafanya nini kwa ajili yake?” 13Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Mkeo atapaswa kushika yote niliyomwambia: 14Asionje mazao yoyote ya mzabibu, wala asinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi. Yote niliyomwamuru, ayafuate.”
15Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tafadhali, ukae kidogo tukutayarishie mwanambuzi.” 16Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Hata kama mkinilazimisha kukaa sitakula chakula chenu. Lakini kama ukipenda, tayarisha sadaka ya kuteketezwa, mtolee Mwenyezi-Mungu.” Manoa hakujua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. 17Basi, Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tuambie jina lako ili tukuheshimu wakati maneno yako yatakapotimia.” 18Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa nini unataka kujua jina langu, kwa kuwa jina langu ni la ajabu?” 19Hapo Manoa akatayarisha mwanambuzi na tambiko, akaviweka juu ya mwamba amtolee Mwenyezi-Mungu afanyaye maajabu. 20Basi, wakati Manoa na mkewe walipokuwa wanatazama miali ya moto ikipanda juu mbinguni kutoka madhabahuni, walimwona malaika katika miali hiyo akipanda kwenda mbinguni. Basi Manoa na mkewe wakasujudu. 21Manoa akajua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Malaika hakumtokea tena Manoa na mkewe.
22Basi, Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, maana tumemwona Mungu.” 23Lakini mkewe akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu angetaka kutuua hangepokea sadaka yetu ya kuteketezwa na ya nafaka; wala hangetuonesha mambo hayo wala kutuambia maagizo.”
24Kisha mkewe Manoa akajifungua mtoto wa kiume, naye Manoa akampa jina Samsoni. Mtoto huyo akakua naye Mwenyezi-Mungu akambariki. 25Roho ya Mwenyezi-Mungu ikaanza kumsukuma akiwa huko Mahane-dani, kati ya Sora na Eshtaoli.



Waamuzi 13;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: