Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 15 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 3...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu Mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu..

Asante Baba wa Mbinguni kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa mpumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhihidiwe Jehovah,
Uabudiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..!!


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako Yahweh...
Mungu wetu tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua...
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea....
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu
 Baba  utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Wastahili sifa, ee Mungu, huko Siyoni, watu watakutimizia wewe ahadi zao, maana wewe wajibu sala zetu. Binadamu wote watakujia wewe. Tunapolemewa na makosa yetu, wewe mwenyewe watusamehe. Heri wale unaowachagua na kuwaleta karibu, waishi katika maskani yako. Sisi tutatoshelezwa na mema ya nyumba yako; mema ya hekalu lako takatifu. Kwa matendo yako makuu watuitikia na kutuokoa, ewe Mungu wa wokovu wetu; wewe ndiwe tumaini la viumbe vyote, duniani kote na mbali baharini. Kwa nguvu yako uliisimika milima mahali pake. Wewe una nguvu mno! Watuliza mshindo wa bahari na wa mawimbi yake, wakomesha ghasia za watu. Ulimwengu wote washangazwa na matendo yako. Wasababisha furaha kila mahali, toka mashariki hata magharibi. Wewe waitunza nchi kwa kuinyeshea mvua, waijalia rutuba na kuistawisha; mto wako umejaa maji tele, waifanikisha nchi na kuipatia mavuno. Hivi ndivyo uitengenezavyo nchi: Mashamba wayanyeshea mvua kwa wingi, na kuyalowanisha kwa maji; ardhi wailainisha kwa manyunyu, na kuibariki mimea ichipue. Wautunukia mwaka wote mema yako, kila ulipopitia pamejaa fanaka. Mbuga za majani zimejaa mifugo, milima nayo imejaa furaha. Malisho yamejaa kondoo, mabonde yamefunikwa kwa ngano. Kila kitu kinashangilia kwa furaha.




Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendeji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
ukatupe kama inavyokupendeza wewe..



Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu; kwake naliweka tumaini langu. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika. Wokovu na fahari yangu vyatoka kwa Mungu; mwamba wangu mkuu na kimbilio langu ni Mungu. Enyi watu, mtumainieni Mungu daima; mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu. Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu. Binadamu wote ni kama pumzi tu; wote, wakubwa kwa wadogo, hawafai kitu. Tena ukiwapima uzito hawafikii kilo, wote pamoja ni wepesi kuliko pumzi. Msitegemee dhuluma, msijisifie mali ya wizi; kama mali zikiongezeka, msizitegemee. Mungu ametamka mara moja, nami nimesikia tena na tena: Kwamba enzi ni mali yake Mungu; naam, nazo fadhili ni zake Bwana; humlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.

Mtalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatawale,ukatamalaki na kutuatamia
Yahweh tunaomba ulinzi wako wakati wote kwetu na kwa vyote
tunavyovimiliki,Mungu wetu ukatupe neema ya kutambua/kujitambu,
kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote
za maisha yetu,Yahweh tukawe wanyenyekevu kwa watu wote,
wepesi wa kusamehe Baba ukatupe amani ya moyo,upendo wa kweli,
kusaidiana,kuchukuliana,kuonyana/kuelimishana kwa amani na upendo
Mungu wetu ukatufanye barua njema nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




Tunakushukuru, ee Mungu, tunakushukuru! Tunatangaza ukuu wa jina lako na kusimulia juu ya matendo yako makuu. Mungu asema: “Mimi nimeweka wakati maalumu! Wakati huo nitahukumu kwa haki. Nchi ikitetemeka na vyote vilivyomo, mimi ndiye ninayeitegemeza misingi yake. Nawaambia wenye kiburi: ‘Acheni kujigamba’; na waovu: ‘Msioteshe pembe za kiburi! Msijione kuwa watu wa maana sana, wala kusema maneno ya majivuno.’” Hukumu haitoki mashariki au magharibi; wala haitoki nyikani au mlimani. Mungu mwenyewe ndiye hakimu; humshusha mmoja na kumkweza mwingine. Mwenyezi-Mungu, anashika kikombe mkononi, kimejaa divai kali ya hasira yake; anaimimina na waovu wote wanainywa; naam, wanainywa mpaka tone la mwisho. Lakini mimi nitafurahi milele, nitamwimbia sifa Mungu wa Yakobo. Atavunja nguvu zote za watu waovu; lakini nguvu za waadilifu ataziimarisha.

Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wote wataabikao na kuelemewa na mizigo,Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa ,wenye njaa ukawapatie chakula,waliokataliwa na kukata tamaa Mungu wetu ukawape tumaini,wanaopita katika magumu/majaribu
Mungu wetu ukawavushe salama,waliokatika vifungo vya yule mwovu
Baba wa Mbinguni ukawafungue na kuwaweka huru,Yahweh ukawape
neema ya kujiombea,kufuata njia zako,ukawape macho ya kuona
na masikio ya kusikia sauti yako na kutii,Baba tunaomba ukapokee
sala/maombi yetu na ukawafute machozi ya watoto wako
wanaokutafuta kwa bidii na imani,Ee Baba utusikie..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwakuwa nami
Mungu awe nanyi daima na msipungukiwe katika mahitaji yenu
Baba wa Mbinguni akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

1Mwenyezi-Mungu aliyaacha nchini mataifa yafuatayo ili kuwajaribu Waisraeli ambao walikuwa hawajapigana vita katika nchi ya Kanaani 2(alifanya hivyo ili awape watu wa vizazi hivyo ujuzi wa kupigana kwani hawakuwa wameona vita): 3Wakuu watano wa Wafilisti, Wakanaani wote, Wasidoni na Wahivi waliohamia katika milima ya Lebanoni kutoka mlima Baal-hermoni mpaka kufikia Hamathi. 4Mwenyezi-Mungu alikusudia kuwatumia hao ili awajaribu Waisraeli, aone kama watatii amri zake alizowaamuru wazee wao kwa njia ya Mose. 5Basi, Waisraeli waliishi pamoja na Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 6Wakaoa binti zao na kuoza binti zao kwa vijana wa mataifa hayo na kuiabudu miungu yao.
Othnieli
7Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; wakamsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaabudu Mabaali na Maashera. 8Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia, nao wakamtumikia kwa muda wa miaka minane. 9Waisraeli wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawapelekea mtu wa kuwakomboa yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. 10Basi, roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Othnieli, naye akawa mwamuzi wa Waisraeli. Othnieli alikwenda vitani naye Mwenyezi-Mungu akamtia Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia mikononi mwake. 11Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini. Kisha Othnieli mwana wa Kenazi, akafariki.
Ehudi
12Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akampa nguvu mfalme Egloni wa Moabu awashambulie Waisraeli, kwa sababu walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. 13Egloni akawakusanya Waamoni na Waamaleki, akaenda kupigana na Waisraeli, akawashinda. Akauteka Mji wa Mitende yaani Yeriko. 14Waisraeli wakamtumikia Egloni mfalme wa Moabu, kwa muda wa miaka kumi na minane.
15Lakini Waisraeli walipomlilia Mwenyezi-Mungu, yeye aliwapelekea mtu wa kuwakomboa, yaani Ehudi mwana wa Gera, mwenye mkono wa shoto, wa kabila la Benyamini.
Waisraeli walimtuma apeleke zawadi zao kwa Egloni mfalme wa Moabu. 16Ehudi akajitengenezea upanga wenye makali kuwili; urefu wake sentimita hamsini. Akaufunga kiunoni mwake upande wa kulia ndani ya mavazi yake. 17Kisha akampelekea Egloni zile zawadi. Egloni alikuwa mtu mnene sana. 18Ehudi alipomaliza kutoa zawadi, akawaambia watu waliobeba zawadi, waondoke. 19Lakini yeye alipofika kwenye sanamu za mawe yaliyochongwa karibu na Gilgali, alimrudia Egloni akasema, “Nina ujumbe wa siri kwako, ee mfalme.” Mfalme akawaamuru watumishi wakae kimya, nao wakatoka nje. 20Naye Ehudi akamkaribia pale alipokaa katika chumba chake chenye baridi barazani, akamwambia “Nina ujumbe wako kutoka kwa Mungu.” Mfalme akainuka kitini mwake na kusimama. 21Ehudi akauchomoa upanga wake kwa mkono wake wa kushoto kutoka paja lake la kulia, akamchoma nao tumboni mwake. 22Upanga ukaingia ndani pamoja na mpini wake, mafuta yakaufunika upanga huo kwani Ehudi hakuutoa tena; ukawa umetokea kwa nyuma.3:22 ukawa umetokea kwa nyuma: Maana ya neno la Kiebrania si dhahiri. 23Kisha, Ehudi akatoka nje barazani baada ya kuifunga milango ya chumba hicho kwa ufunguo.
24Ehudi alipoondoka, watumishi wa mfalme wakarudi. Walipoona milango yote ya chumba imefungwa, walifikiri amekwenda kujisaidia chooni humo ndani ya nyumba. 25Wakangojea mpaka wakaanza kuwa na wasiwasi. Walipoona hafungui, wakachukua ufunguo na kufungua mlango. Wakamwona mfalme wao sakafuni, naye amekufa.
26Walipokuwa wanangoja, Ehudi alitoroka akipitia kwenye sanamu za mawe, akaenda Seira. 27Alipofika huko alipiga tarumbeta katika nchi ya milima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka huko milimani naye akawatangulia. 28Akawaambia, “Mnifuate, maana Mwenyezi-Mungu amewatia adui zenu Wamoabu mikononi mwenu.” Wakamfuata mpaka kivuko cha Yordani na kukiteka toka mikononi mwa Wamoabu, wakazuia mtu yeyote kupita. 29Siku hiyo, wakawaua Wamoabu wapatao 10,000; watu wote wenye afya na nguvu, wala hakuna hata mmoja aliyenusurika. 30Siku hiyo Waisraeli wakawashinda Wamoabu. Nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka themanini.
Shamgari
31Baada ya Ehudi mwana wa Anati, Shamgari alishika nafasi yake. Yeye aliwaua Wafilisti 600 kwa fimbo ya kuchungia ng'ombe. Naye pia aliwakomboa Waisraeli.


Waamuzi 3;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: