Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 2 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 18...Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru na kumsifu..

Mungu wetu Baba yetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Baba wa Mbinguni,Mfalme wa Amani,Baba wa huruma,Mungu wa
wajane,Baba wa yatima,Mponyaji wetu,Mlinzi wetu,Kimbilio letu..
Uhimidiwe Yahweh,Uabudiwe milele,Utukuzwe Baba wa Mbinguni,
Usifiwe Mungu wetu,Unastahili sifa,Mwimbieni Mungu sifa,Mwimbieni.!
Mwimbieni Mfalme wetu sifa Mwimbieni..!
Mshangilieni, Mwimbieni Mungu sifa,simulieni matendo yake ya ajabu..!
Uniwezeshe kusema, ee Bwana,
Midomo yangu itangaze sifa zako..!Imbeni juu ya Utukufu wa jina lake,
Mtoleeni sifa tukufu..!
Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,wakiimba
daima sifa zako..!!


Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; wakauliza, “Yuko wapi?” Kulikuwa na minongono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “La! Anawapotosha watu.” Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda hekaluni, akaanza kufundisha. Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?” Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma. Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe. Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote. Je, Mose hakuwapeni sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Hapo watu wakamjibu, “Una pepo wewe! Nani anataka kukuua?” Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia. Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa nyinyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato. Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi sheria isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato? Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki.”

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha,na kujiachilia mikononi mwako Jehovah..
Yahweh tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni
utufunike kwa damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nzareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu? Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo? Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!” Basi, Yesu alipokuwa anafundisha hekaluni alipaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?”

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu..
Yahweh ukatupe neema ya ubunifu,maarifa katika vyote
tunavyoenda kufanya/kutenda na tukatende kama inavyokupendeza wewe
Jehova tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu 
ukatupe neema ya uvumilivu,kusameheana,
kuchukuliana,kuhurumiana,kusaidiana,kuelimishana kwa amani,
Upendo ukadumu na kila mmoja akajue jukumu lake na kazi yake..
Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako watoto,wazazi wetu
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu sisi na vyote tunavyovimiliki
Baba wa Mbinguni ukatawale katika maisha yetu,ukatamalaki na kutuatamia,tuka nene yaliyo yako Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya kusimamia neno lako Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Yahweh ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Mafarisayo waliwasikia watu wakinongona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni. Yesu akasema, “Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma. Mtanitafuta lakini hamtaniona, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika.” Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? Ana maana gani anaposema: ‘Mtanitafuta lakini hamtanipata, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika?’” Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalumu. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, “Aliye na kiu na aje kwangu anywe. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: ‘Anayeniamini mimi, mito ya maji ya uhai itatiririka kutoka moyoni mwake!’” (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado).

Yahweh tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu wote
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokata tamaa ukawape tunaini,wagonjwa ukawaponye,wenye njaa Baba ukawatendee
na kubariki kazi zao,mashamba na wakapate mahitaji ya kutosha na akiba...
walio katika vifungo mbalimbali vya yule mwovu Baba ukawafungue na kuwaweka huru,ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo ziwaweke huru..


Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, “Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!” Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine walisema, “Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya? Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: ‘Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!’” Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu. Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata. Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, “Kwa nini hamkumleta?” Walinzi wakawajibu, “Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!” Mafarisayo wakawauliza, “Je, nanyi pia mmedanganyika? Je, mmekwisha kumwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini? Lakini umati huu haujui sheria ya Mose; umelaaniwa!” Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia, “Je, sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?” Nao wakamjibu, “Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!” 
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Bwana asanteni kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama
inavyompendeza yeye..
Nawapenda..

Makabila mengine yanagawiwa nchi

1Baada ya kuishinda ile nchi, jumuiya yote ya Waisraeli ilikusanyika huko Shilo na kulisimika hema la mkutano. 2Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ambayo hayakuwa yamegawiwa sehemu yao ya nchi. 3Kwa hiyo, Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtakawia mpaka lini kwenda kuimiliki nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapeni? 4Chagueni watu watatu kutoka kila kabila niwatume nchini kote wachunguze na kuchora ramani kulingana na makabila yao, kisha waniletee taarifa. 5Nao wataigawanya nchi hiyo sehemu saba. Kabila la Yuda litabaki na sehemu yake ya kusini na kabila la Yosefu kaskazini. 6Tayarisheni maelezo kamili juu ya sehemu zote saba na kuniletea. Hapo, nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kuhusu sehemu ya kila kabila lenu. 7Lakini Walawi hawatapata sehemu yoyote kati yenu, maana sehemu yao ni kuwa makuhani wa kumhudumia Mwenyezi-Mungu. Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase walikwisha pata sehemu yao upande wa mashariki wa mto Yordani. Walipewa sehemu hii na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu.”
8Basi, watu hao wakaanza safari ya kwenda kuichunguza nchi. Kabla hawajaenda, Yoshua akawapa maagizo: “Nendeni nchini kote mkaandike maelezo kamili juu ya hiyo nchi, kisha mrudi mnieleze, nami nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu hapa hapa Shilo kuhusu sehemu mtakayopewa.” 9Wanaume hao wakazunguka nchini kote, wakachora maelezo kamili juu ya sehemu zake saba pamoja na miji yake, kisha wakarudi kwa Yoshua kule kambini Shilo. 10Huko Shilo, Yoshua akazipigia kura sehemu hizo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawagawia Waisraeli; kila kabila na sehemu yake.

Nchi ya kabila la Benyamini

11Kura ya kwanza ililipata kabila la Benyamini kulingana na koo zake. Eneo walilopewa watu hao lilikuwa katikati ya lile la kabila la Yuda na lile la kabila la Yosefu. 12Mpaka wake wa kaskazini ulianzia mto Yordani na kupitia kaskazini mwa Yeriko na nchi ya milima ukaelekea magharibi hadi kwenye nyika ya Beth-aveni. 13Kutoka huko, mpaka wake ulikwenda kusini kuelekea Luzu kupitia upande wa kusini wa Luzu (yaani Betheli) hadi Ataroth-adari, kwenye mlima ulioko kusini mwa Beth-horoni ya Chini. 14Upande wa magharibi wa mlima huo ulio kusini mwa Beth-horoni mpaka uligeuka ukaelekea kusini hadi Kiriath-baali, uitwao pia Kiriath-yearimu, mji ambao ni mali ya kabila la Yuda. Huu ndio uliokuwa mpaka wake upande wa magharibi. 15Upande wa kusini mpaka wake ulianzia kwenye viunga vya mji wa Kiriath-yearimu, ukafika Efroni na kwenda hadi kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa. 16Kisha ulielekea chini kupitia pembeni mwa mlima ulioko karibu na bonde la mwana wa Hinomu, ambalo lilikuwa katika sehemu ya kaskazini zaidi ya bonde la Warefai. Halafu mpaka uliteremka kuelekea bonde la Hinomu, kusini mwa kilima cha Wayebusi, ukaendelea kuteremka hadi En-rogeli. 17Huko, mpaka uligeuka kwenda kaskazini kuelekea En-shemeshi, ukapitia Gelilothi unaokabili mwinuko wa Adumimu na kuteremka hadi kwenye jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. 18Kutoka hapo, mpaka ulizunguka kaskazini kwenye ukingo wa juu wa Araba na kuishia huko Araba. 19Tena, ukaendelea kwa upande wa kaskazini wa kilima cha Beth-hogla na kuishia kaskazini kabisa ya ghuba ya Bahari ya Chumvi, mahali unapoingilia mto Yordani. Huu ni mpaka wake kwa upande wa kusini. 20Mto Yordani ndio uliokuwa mpaka wake upande wa mashariki. Ndivyo zilivyowekewa mipaka nchi zilizopewa koo za kabila la Benyamini.
21Miji ya koo za kabila la Benyamini ni Yeriko, Beth-hogla, Emek-kesisi, 22Beth-araba, Zemaraimu, Betheli, 23Avimu, Para, Ofra, 24Kefar-amoni, Ofni na Geba. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na miwili pamoja na vijiji vyake. 25Miji mingine ni Gibeoni, Rama, Beerothi, 26Mizpa, Kefira, Moza, 27Rekemu, Irpeeli, Tarala, 28Zela, Ha-elefu, Yebusi, yaani Yerusalemu, Gibea na Kiriath-yearimu. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na minne pamoja na vijiji vyake. Hiyo yote ni sehemu waliyopewa watu wa kabila la Benyamini na koo zao.

Yoshua 18;1-28

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: