Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 28 December 2012

Jikoni Leo,Afya na Jamii; Na Kaka John Haule-Jinsi ya kutengeneza maziwa ya soya.


Jinsi ya kutengeneza maziwa ya soya.

Baba karudi ni makala fupi fupi ambazo zitakuwa zinatoa mwanga kwa jamii kujifanyia mambo yahusuyo afya na maisha bora kwa ujumla wa ustawi wa jamii ya watanzania kila wiki katika uwanja huu. Lakini la kufurahisha zaidi ni kuwa, hata kama unakusudia kufanya kitu Fulani lakini hujui namna ya kufanya basi kutakuwa na fursa kwako msomaji kutuletea maswali ambayo naahidi yatajibiwa yote ili kuharakisha maendeleo ya Taifa letu. Uwanja huu utaitwa “Baba Karudi” ukiwa na maana nitakuwa natoa kile nilichopata katika safari zangu duniani kote ambako shughuli yangu kubwa ni kukutana na wataalamu wa mambo mbali mbali na kufanya mahojiano nao halafu nakuja kuwaletea watanzania wangu hapa vile vile nitakuwa nayapeleka maswali yenu wasomaji juu ya yale mnayotaka kuyafanya lakini hamjui yanafanywaje.. Nakuomba usiende mbali.
Leo nimekutana na Bi Carole Bruzzano toka www.eHow.com. Nimefunga safari kuja Canada kupata ukweli juu ya Soya kuwa maziwa safi na bora kwa afya za walaji. Yeye anasema:

Soya inatumika duniani kote katika mapishi mengi mbalimbali ikiwemo kutengeneza maziwa na kuungia kitoweo kama nyama na samaki au kama mbadala wa vitoweo hivyo kiafya kwa mlaji.
Anasema kutengeneza maziwa ya unga ya soya ni kazi ndogo sana ambayo inaweza kukugharimu kama dakika 60 tu. Wenye viwanda vikubwa hupitia hatua nyingi kutengeneza maziwa hayo ya unga ya soya. Lakini wewe unaweza tu ukatengeneza mwenyewe nyumbani kwako tena kwa kutumia vifaa rahisi vinavyopatikana bila kuazima kwa jirani.
Wewe unatakiwa uanze na kuzisafisha soya kwanza, halafu weka juani zinyauke kidogo ili ngozi ya soya ilegee na kasha umenye ngozi zote, uoshe tena na uzikaushe mpaka zikauke kau! Hapo tayari utakuwa umeshaandaa soya kusagwa na kuwa maziwa ya unga tayari kupeleka mahotelini na majumbani kwa matumizi.
Bi Carole anasema unahitaji kuwa na vifaa hivi:
1.     Lazima uwe na kikaango ili uzikaange soya zako kabla ya kusagwa.
2.     Unatakiwa pia uwe na blenda au kinu cha kutwangia na chekecheke ili soya iwe unga laini sana
3.     Mwisho tayarisha vikombe viwili au vitatu vya soya
4.     Maziwa halisi japo nusu kikombe kwa ladha na harufu.
Kaanga soya yako katika kikaango angalia zisiungue.zikaange kwa dakika 10 hadi 15 na utaona kuwa zimeiva kwa kubadilika rangi na kuwa kahawia basi ipua na ziache zipoe kidogo kabla ya kuanza kuzisaga.
Saga soya zako, chekecha mpaka upate unga laini sana, ukimaliza weka katika chombo kikavu na kisafi. Sasa chukua maziwa HALISI nusu kikombe na tia katika soya halafu changanya na anika mpaka mchangavyiko huo umekauka.
Mwisho utaona unga umekauka lakini bado una madonge. Yapukuchue kwa mikono safi  halafu tia soya katika mkebe safi tayari kwa matumizi kama maziwa halisi.
Faida za Maziwa ya soya
Unaweza kuanzisha biashara ya kuuza maziwa kama wewe ni mama ntilie au una hoteli au aina zingine za biashara ya vyakula na ukapata faida kubwa bila kuwa na wasiwasi wa kupata hasara.
Maziwa ya soya ni mazuri ukilinganisha nay a wanyama kwa kuwa hayana sukari asilia iitwayo Lacoste ambayo sio nzuri kwa afya hivyo wenye aleji na maziwa ya kawaida basi ndio muda wao wa kujidai na maziwa haya.
Maziwa ya soya yana protini karibu sawa kabisa na ya wanyama lakini haya yana protini ya mimea tofauti na ile ya wanyama ambayo si nzuri kwa afya. Protini ya mimea ni nzuri mwilini kwa kuzuia upotevu wa calsiam kwenye mkojo na kukusaidia usipatwe na magonjwa ya maumivu ya mifupa. Wenye kisukari ndio maziwa yao haswa.
Maziwa ya soya hayana mafuta yenye sumu (saturated fats) wala lehemu. Hivyo ni maziwa yanayowafaa wagonjwa wenye maradhi ya moyo sana.
Maziwa haya bado Bi Carole anadai kuwa ni kinyonya sumu mwilini kijulikanacho kama “isoflavones” ambacho huzuia uzee wa kizembe, maraghi ya mifupa na kansa za aina nyingi mwilini.
Mtu akinywa kikombe kimoja cha maziwa ya soya basi ajue kuwa ana 20%ya isoflvones ambayo katika maziwa ya wanyama hamna!
Hivyo leo tunaishia hapa kwa kuwaasa kujitengenezea maziwa ya soya badala ya kuharibu pesa ambayo ni ngumu sana hasa kwa kipindi hiki. Lakini pia tumefungua rasmi ukurasa ambao tutautumia wasomaji kuuliza namna ya kufanya jambo lolote ulitakalo. Wiki ijayo nitakuja na “JINSI YA KUJITENGENEZEA SODA YOYOTE” au kwa lugha ya wataalamu ni “how to carbonated drinks” ambayo itatusaidia kupunguza manunuzi ya soda kipindi hiki cha jua kali na pia tutaongelea faida na hasara za kunywa soda pia.
Asanteni kwa kunisoma na tuonane juma lijalo.

John Haule ni mpelelezi binafsi (Private investigator) anayejihusisha na tafiti zenye suluhisho kwa matatizo ya kijamii. Unaweza kumpigia kwa miadi ya ushauri juu ya tatizo lolote linalokusumbua kibinadamu. Anapatikana Car Painters - Temeke Stereo, Sandawe Street, jirani na Dr. Massawe. Simu: 0768 215 956 au email rumoursafrica@gmail.com


        "Swahili NA Waswahili" Pamoja Sana.

No comments: