Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 5 February 2021

Kikombe Cha Asubuhi;Waroma...9


Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Nimefanya mambo mema na adili; usiniache makuchani mwa maadui zangu. Uahidi kunisaidia mimi mtumishi wako; usikubali wenye kiburi wanidhulumu. Macho yangu yanafifia nikingojea uniokoe, nikingojea utimize uliyoahidi.

Zaburi 119:121-123

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Unitendee mimi mtumishi wako kadiri ya wema wako, unifundishe masharti yako. Mimi ni mtumishi wako, unipe maarifa, nipate kujua maamuzi yako.

Zaburi 119:124-125

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Ee Mwenyezi-Mungu, sasa ni wakati wa kufanya kitu, kwa maana watu wanavunja sheria yako. Mimi, nazipenda amri zako, kuliko hata dhahabu safi kabisa. Kwa hiyo, nafuata kanuni zako zote; kila njia potovu naichukia.

Zaburi 119:126-128


Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Mungu na taifa lake teule

1Nasema ukweli tupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia. 2Nataka kusema hivi: Nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu 3kwa ajili ya ndugu zangu walio wa taifa langu! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo. 4Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; alifanya nao maagano, akawapa sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake. 5Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina.
6Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu. 7Wala si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Wazawa wake watatokana na Isaka.” 8Ndiyo kusema, si wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake. 9Maana ahadi yenyewe ni hii: “Wakati maalumu nitarudi, naye Sara atapata mtoto.”
10Tena si hayo tu, ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu. 11Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya, 12Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu. 13Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia.”
14Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo! 15Maana alimwambia Mose: “Nitamhurumia mtu yeyote ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka.” 16Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au mapenzi ya mtu. 17Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao: “Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina langu litangazwe popote duniani.” 18Ni wazi basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo.
Ghadhabu na huruma ya Mungu
19Labda utaniuliza: “Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?” 20Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: “Kwa nini umenitengeneza namna hii?” 21Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida.
22Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake. Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa. 23Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake. 24Maana sisi ndio hao aliowaita, si kutoka miongoni mwa Wayahudi tu bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine. 25Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea:
“Wale waliokuwa ‘Si watu wangu’
nitawaita: ‘Watu wangu!’
Naye ‘Sikupendi’
ataitwa: ‘Mpenzi wangu!’
26Na pale walipoambiwa:
‘Nyinyi si wangu’
hapo wataitwa:
‘Watoto wa Mungu aliye hai.’”
27Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaza sauti: “Hata kama wazawa wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa; 28maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote.” 29Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: “Bwana wa majeshi asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa kama Gomora.”
Israeli na Habari Njema
30Basi tuseme nini? Watu wa mataifa ambao hawakutafuta wafanywe waadilifu, wamejaliwa kuwa waadilifu, kwa njia ya imani, 31hali watu wa Israeli ambao walitafuta sheria ya kuwafanya kuwa waadilifu, hawakuipata. 32Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa 33kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Tazama, nitaweka huko Siyoni jiwe likwazalo,
mwamba utakaowafanya watu waanguke.
Lakini atakayemwamini hataaibishwa!”

Waroma9;1-33
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: