Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 9 February 2021

Kikombe Cha Asubuhi;Waroma...11


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni mwadilifu; na hukumu zako ni za haki. Umetoa maamuzi yako, kwa haki na uthabiti. Upendo wangu kwako wanifanya niwake hasira, maana maadui zangu hawajali maneno yako.

Zaburi 119:137-139

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Ahadi yako ni hakika kabisa, nami mtumishi wako naipenda. Mimi ni mdogo na ninadharauliwa; hata hivyo sisahau kanuni zako.

Zaburi 119:140-141

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Uadilifu wako ni wa haki milele; sheria yako ni ya kweli. Taabu na huzuni vimenipata, lakini amri zako ndizo furaha yangu. Maamuzi yako ni ya haki daima; unijalie maarifa nipate kuishi.

Zaburi 119:142-144

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.


Huruma ya Mungu kwa Israeli
1Basi, nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? Hata kidogo! Mimi binafsi ni Mwisraeli, mzawa wa Abrahamu, wa kabila la Benyamini. 2Mungu hakuwakataa watu wake aliowateua tangu mwanzo. Mnakumbuka yasemavyo Maandiko Matakatifu juu ya Elia wakati alipomnungunikia Mungu kuhusu Israeli: 3“Bwana, wamewaua manabii wako na kubomoa madhabahu yako. Ni mimi tu peke yangu niliyebaki, nao wanataka kuniua!” 4Je, Mungu alimjibu nini? Alimwambia: “Nimejiwekea watu 7,000 ambao hawakumwabudu Baali.” 5Basi, ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: Ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu aliwateua kwa sababu ya neema yake. 6Uteuzi wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena.
7Sasa, je? Watu wa Israeli hawakukipata kile walichokuwa wanakitafuta; lakini wote walioteuliwa walikipata. Wengine walipumbazwa, 8kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Mungu ameifanya mioyo yao kuwa mizito,
na mpaka leo hii hawawezi kuona kwa macho yao
wala kusikia kwa masikio yao.”
9 Taz Zab 69:22-23 Naye Daudi anasema:
“Karamu zao na ziwe mtego wa kuwanasa,
waanguke na kuadhibiwa.
10Macho yao yatiwe giza
wasiweze kuona.
Migongo yao ipindike kwa taabu daima!”
11Basi, nauliza: Je, Wayahudi wamejikwaa hata wakaangamia kabisa? Hata kidogo! Kutokana na kosa lao ukombozi umewajia watu wa mataifa mengine, ili Wayahudi wapate kuwaonea wivu. 12Kosa la Wayahudi limesababisha baraka nyingi kwa ulimwengu, na utovu wao wa kiroho umeleta baraka nyingi kwa watu wa mataifa mengine. Basi, ni dhahiri kwamba kuingizwa kwa idadi yao kamili kutakuwa ni baraka zaidi.
Ukombozi wa watu wa mataifa mengine
13Basi, sasa nawaambieni nyinyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu, 14nipate kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee nyinyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa baadhi yao. 15Maana ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka!
16Ikiwa kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia. 17Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Nyinyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini. 18Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si nyinyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza nyinyi.
19Lakini utasema: “Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake.” 20Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari. 21Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe? 22Ona, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa. 23Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena. 24Nyinyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao.
Kuongoka kwa Israeli
25Ndugu zangu, napenda mjue ukweli huu uliofichika msije mkajiona wenye akili sana. Ukaidi wa Wayahudi ulikuwa ni wa muda tu, mpaka watu wa mataifa mengine watakapokuwa wamemfikia Mungu. 26Hapo ndipo taifa lote la Israeli litakapookolewa, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
“Mkombozi atakuja kutoka Siyoni,
atauondoa uovu wa wazawa wa Yakobo.
27Hili ndilo agano nitakalofanya nao
wakati nitakapoziondoa dhambi zao.”
28Kwa sababu wanaikataa Habari Njema, Wayahudi wamekuwa maadui wa Mungu, lakini kwa faida yenu nyinyi watu wa mataifa. Lakini, kwa kuwa waliteuliwa, bado ni marafiki wa Mungu kwa sababu ya babu zao. 29Maana Mungu akisha wapa watu zawadi zake na kuwateua, hajuti kwamba amefanya hivyo. 30Hapo awali nyinyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmepata huruma yake kutokana na kuasi kwao. 31Hali kadhalika, kutokana na huruma mliyojaliwa nyinyi, Wayahudi wanamwasi Mungu sasa ili nao pia wapokee sasa huruma ya Mungu. 32Maana Mungu amewafunga watu wote katika uasi wao ili apate kuwahurumia wote.
Mungu asifiwe
33Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na njia zake hazieleweki! Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
34“Nani aliyepata kuyajua mawazo ya Bwana?
Nani awezaye kuwa mshauri wake?
35Au, nani aliyempa yeye kitu kwanza
hata aweze kulipwa tena kitu hicho?”
36Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, vyote vipo kwa uwezo wake na kwa ajili yake. Utukufu na uwe kwake hata milele! Amina.
Waroma11;1-36
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: