Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 4 February 2021

Kikombe Cha Asubuhi;Waroma...8

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Nawachukia watu wanafiki, lakini naipenda sheria yako. Wewe ni ngao yangu, kwako napata usalama; naweka tumaini langu katika neno lako.

Zaburi 119:113-114

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Ondokeni kwangu, enyi waovu, ili nipate kushika amri za Mungu wangu. Uniimarishe ulivyoahidi, nami nitaishi; usikubali niaibike katika tumaini langu. Unitegemeze, niwe salama; niwe daima msikivu kwa masharti yako.

Zaburi 119:115-117

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Unawakataa wote wanaokiuka masharti yako; mawazo yao maovu ni ya bure. Waovu wote wawaona kuwa takataka, kwa hiyo mimi napenda maamuzi yako. Natetemeka kwa kukuogopa wewe; nimejaa hofu kwa sababu ya hukumu zako.

Zaburi 119:118-120

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.


Kuishi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu
1Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo. 2Maana, sheria ya Roho iletayo uhai kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo. 3Mungu ametekeleza jambo lile ambalo sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu wa binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi. 4Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho. 5Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho. 6Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uhai na amani. 7Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii. 8Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
9Lakini nyinyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo. 10Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmefanywa kuwa waadilifu. 11Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu ataipa uhai miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.
12Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu. 13Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi. 14Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu. 15Kwa maana, hamkumpokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watumwa tena na kuwatia hofu, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watoto wa Mungu, na kwa Roho huyo, sisi tunamwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!” 16Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. 17Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.
Utukufu ujao
18Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19Viumbe vyote vinangojea kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake. 20Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini, 21maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu. 22Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto. 23Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukingojea tufanywe watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe. 24Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa. Lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona? 25Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu.
26Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. 27Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu.
28Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake. 29Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake.
Upendo wa Mungu
31Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? 32Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote? 33Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia! 34Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka kwa wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea! 35Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? 36Taz Zab 44:22 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
“Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha;
tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.”
37Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. 38Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; 39wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Waroma8;1-39
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: